Faida Ya Kuwa Na Marafiki Wenye Mitizamo Chanya.

Habari za leo, mpenzi msomaji wa makala za Amka Mtanzania. Wiki yako umeimalizaje, yale uliyopanga ufanye, na hujafanya ndio yamekuvunja moyo au bado unaendelea kuweka juhudi?
Nikushauri kwamba usiache kuweka juhudi, unaweza ukafikiri kuacha ila kabla hujafanya hivyo tazama nyuma ulipotoka hata kama mbele hujui umebakiza umbali gani. Nakwambia ulipotoka yaweza kuwa ni mbali kuliko huo umbali wa kufikia malengo yako.

Leo nataka tuongolee kidogo faida ya kuwa na marafiki wasiokubali kushindwa. Hata kama watu wote wataona haiwezekani kabisa, lakini wao hukaa chini kuangalia wafanyaje ili iwezekane.
Moja ya malengo niliyojiwekea mwaka huu niyatimize katika maisha yangu. Ni pamoja na kutengeneza timu kubwa ya marafiki wasiokubali kushindwa.

Kwanini nilifikiri kuwa na marafiki wa namna hii? ni kwa sababu nilijua kuna faida kubwa mno kuzungukwa na watu wengi wa  namna hii. Na nilijua kuna hasara kubwa sana ya kukaa/kushinda na marafiki ambao wao kazi yao ni kukosoa wengine, na kuwasema vibaya wenzao.

KUWA NA MARAFIKI AMBAO WATAKUSAIDIA KUFIKA JUU ZAIDI YA HAPO ULIPO SASA.


Nilichogundua kingine kwa hawa watu, wao huwa hawatafuti njia ya kumaliza tatizo, bali wao hutafuta wa kuendelea kulaumu na kumtupia lawama zote. Pia wao hufurahia zaidi kukwama kwa jambo ili wapate kumpumzika, kama ni kazini na kazi yenyewe inahitaji umeme, ikatokea umeme umekatika wao hufurahia sana kile kitendo.

SOMA; Watu Hawa Wanakurudisha Nyuma, Kuwa Makini Nao.
Pia kundi hili lenye mitizamo hasi, nimegundua ni kundi lenye kujipenda na kujijali sana kwa maneno mengi na matamu ila ni wavivu mno wa kazi. Mkitaka kuingia kwenye kazi yenye kuhitaji umakini na uvumilivu, wao watatafuta mbinu wakufundishe  msifanye vizuri.
Baada ya kuona sitafika pale ninapopataka kwa viwango ninavyotarajia, niliona nipunguze ukaribu na hili kundi. Sio kana kwamba silipendi hili kundi la hasha! nahitaji kuwa vile nataka na si kurudishwa nyuma na watu ambao naweza kuwaepuka.

Nimekuambia hili jambo ili ujifunze kitu hapa, sina maana nimekuandikia haya ili kujivuna kwako. Bali najaribu kukupa mwanga, je hao marafiki ulionao wana mchango gani kukufikisha pale ulipopatarajia?
Labda hunielewi vizuri nazungumzia nini, kama ulikuwa hujui, rafiki yako unayemkubali na kumsikiliza sana, anao uwezo wa kukupandikiza vitu vingi sana vilivyo ndani yake, ujue leo.
Ikiwa rafiki yako anapenda sana story za wanawake/wanaume anaotembea nao kwa kuzini. Hiyo hali bila wewe kujijua utajikuta unaipenda.
Ikiwa rafiki yako muda mwingi anazungumzia habari za starehe kuliko kazi, utajikuta na wewe unakuwa mvivu. Zaidi utataka na wewe uende hizo sehemu mkapumzike, mle, mnywe.

SOMA; Hii Ndio Siri Ya Kupata Marafiki Bora Watakaokuwezesha Kufikia Malengo Yako.
Ndivyo ilivyo katika mafanikio yeyote, yawe kimwili au kiroho. Unapotaka kuwa imara zaidi ya jana kwa kile unachofanya, chenye manufaa ya maisha yako na familia/jamii yako inayokuzunguka. Lazima uwe na mtu/watu watakaokutia hamasa ya kusonga mbele zaidi, hata pale unapojihisi umechoka, hata pale unapojihisi hapa siwezi tena. Rafiki zako watakuambia inawezekana, watakupa maelekezo ya kufuata ili ufike pale unapopataka.
Haijalishi umevunjwa moyo kiasi gani, ila unapopata muda wa kuwatazama wao unajisikia nguvu ndani yako ya kusonga mbele zaidi.

Unatakiwa uwe na marafiki wa namna hii wenye kukuzidi hatua kadhaa mbele, na wale unaowazidi hatua nyingi mbele, lakini wana hamasa nzuri za kufanikiwa zaidi, wao wawe ni kama kinga ya wewe kutokupunguza mwendo kasi. Ukiwa unajua hapa nikichoka tu wenzangu wananipita mbele, na wewe unabaki nyuma.
Na wale walio mbele yako, hawa watakuwa kama chambo yako. Kila wanapokanyaga na kutoa mguu watakuhakikishia kwamba kuna usalama eneo hilo, hata kama huoni mbele. Watakupa ujasiri wa hali ya juu ndani yako, jinsi wao wanavyoendelea kusonga mbele kwa ujasiri, na wewe utapata ujasiri.

Una marafiki wa namna ya kushindwa na si kushinda?
Anza leo kutafuta rafiki ambaye amefanikiwa kwenye eneo unalolihitaji kufanikiwa. Kufanya hivyo sio utaishi maisha anayoishi yeye hapana, itakusaidia kujiona unaweza pale unapojihisi umechoka/kulegea.
Utasukumwa zaidi kwenda mbele, hata pale utakapoona giza nene mbele yako.
Mwenzako nimefanya hivyo, nimeona faida kubwa sana kuliko hasara. Na wewe nakuhakikishia hutojuta kuwa na rafiki/marafiki wenye mitazamo chanya. Mwanzoni utajiona hauendani vizuri na wenzako, wewe jua kwamba tabia ya mwanzo haitoki kwa haraka. Taratibu utajikuta umelingana tabia na wenzako wenye kutegemea kufanikiwa na si kushindwa.

SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
Nikukumbushe pia hili; marafiki zako wa mwanzo watakuona umewasaliti, wataanza kukusema vibaya, kuwa siku hizi umebadilika, unajifanya, hutaki kuzungumza nao vizuri… hilo lisikupe shida, fanya kile amani ya moyo wako inakusukuma ufanye. Utashangaa unaanza kumbadilisha mmoja mmoja maisha yake, kwa matendo yako mema.
Kuna kitu umejifunza? nikushauri kifanyie kazi kwa vitendo na si maneno ya mdomoni tu. Asante sana.
Makala hii imeandikwa na rafiki yako Samson Ernest, unaweza kuwasiliana nami kwa;
0759808081. email; samsonaron0@gmail.com au unaweza kutembelea blog yangu www.mtazamowamaisha.blogspot.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: