Kama umenifahamu kwa muda mrefu, namaanisha kama umekuwa unasoma makala ninazoandika, utakuwa unaujua msimamo wangu ambao uko wazi kabisa.
HAKUNA KULALAMIKA, kama kitu hukipendi kibadili, kama huwezi kukibadili achana nayo. Hii ni njia rahisi sana ya kuishi. Ukiweza kuitekeleza vyema, utajipunguzia mizigo mingi na msongo wa mawazo.
Lakini utaniambia siwezi kuacha kulalamika au kumlaumu mtu ambaye ameharibu maisha yangu, mtu ambaye amenifanyia vibaya. Hapa ni pale watu waliokuwa wana uhusiano fulani, labda wa kindoa au wa kidugu au wa kikazi na kibiashara, wanaposhindwa kuendelea na uhusiano huo kutokana na makosa ya mmoja.
Kama wewe ndio umetendewa ubaya si ni lazima utakuwa na haki ya kulalamika? Kwa wewe mwenyewe utajijibu ndiyo. Lakini mimi nakuambia hapana, huna haki yoyote ile ya kulalamika au kumlaumu mwingine, hata kama umekuta ana njama za kukuua.
Kwa nini unasema nisimlalamikie?
Swali zuri. Ni kwa sababu nusu ya matatizo ambayo mmekuwa nayo umesababisha wewe. Amini usiamini, kaa chini fanya tathmini, nusu ya matatizo yote ambayo unayo na mtu yeyote, umesababisha wewe na sio mtu mwingine.
Utaniambia ulimwamini mtu mkaingia kwenye biashara na sasa amekutapeli, hapo ni matatizo gani nimesababisha mimi?
Haya orodha ya matatizo yako ni hii hapa…..
Kwanza tu kumwamini hilo ni tatizo laki, hakuna aliyekulazimisha, ulimwamini mwenyewe, tatizo lako.
Pili wakati mnaendelea na biashara kuna viashiria ulianza kuviona ya kwamba mwenzako sio makini au sio mwaminifu, wewe hukuchukua hatua mapema, ulijipa moyo atabadilika au hataweza kufanya vibaya, kosa lako tena….
Makosa tapo mengi, tukianza kuchimba, nusu ya matatizo ni wewe umeyasababisha.
SOMA; Hakuna Anayejua Anachofanya, Na Huo Ndio Uzuri Wa Maisha.
Unapoingia kwenye matatizo na mtu, badala ya kupoteza muda wako kumlalamikia na kuhesabu mabaya yake, hebu kaa chini na kuhesabu nusu ya matatizo uliyosababisha wewe, halafu jiambie kwamba hutayarudia tena matatizo hayo kwa wengine ambao unaendelea nao.
Maisha ni rahisi kama hivyo, unachagua ni nini unataka na unafanyia kazi, hakuna KULALAMIKA wala KULAUMU.
TAMKO LANGU;
Najua nusu ya matatizo yote ambayo yanatokea kati yangu mimi na mtu mwingine nimesababisha mimi mwenyewe. Pale ninapokuwa na matatizo na mtu, badala ya kulalamika ni jinsi gani amenifanyia ubaya, nitajiuliza ni nusu ipi ya matatizo nimechangia mimi na nitayarekebisha kwenye mahusiano yangu na wengine ili nisipate tena matatizo kama hayo.
NENO LA LEO.
You’re either part of the solution or you’re part of the problem.
Eldridge Cleaver
Unawezakuwa sehemu ya suluhisho, au unaweza kuwa sehemu ya tatizo.
Kwa maneno mengine kama wewe sio sehemu ya suluhisho, basi ni sehemu ya tatizo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
