Kila mmoja wetu anapenda kuwa na maisha mazuri, maisha bora kulingana na vigezo vyake.

Na kila mtu ana picha ya maisha mazuri kwake yana maana gani. Na picha hizi zinatofautiana.

Lakini pia hakuna anayepata maisha yanayoendana na ile picha yako moja kwa moja, hasa wakati wa mwanzoni. Kuna baadhi ya vitu mtu anaweza kuwa anataka lakini hapati.

MAISHA BORA YANAANZIA NDANI YAKO.
MAISHA BORA YANAANZIA NDANI YAKO.

Katika hali kama hii kuna watu ambao maisha yao yanakwenda vizuri na wanayafurahia. Na kuna wengine ambao maisha yao yanakwenda hovyo sana na kuona hayana maana.

Hawa ambao maisha yao yanakwenda vizuri na kuyafurahia japo hawajapata kila walichotaka, wanakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata kile wanachotaka.

Wale ambao maisha yao yanakuwa ya hovyo sana kutokana na kupata kila walichotaka, wanajiondolea kabisa nafasi ya kupata kile wanachotaka.

Je wewe upo upande upi?

Leo nataka nikupe sababu moja kwa nini kuna ambao maisha yao yanakuwa hovyo sana kwa kukosa baadhi ya vile wanavyotaka. Hawa ni wale watu ambao wanajiangalia wao wenyewe tu. Wanaangalia maisha yao kwa kujiangalia wao wenyewe na hivyo wanapokosa hata kidogo wanaona maisha yao hayafai.

Wale ambao maisha yao yanakuwa bora licha ya kukosa vile wanavyotaka huwa hawajiangalii wao wenyewe tu, bali pia huwaangalia wale wanaowazunguka. Kupitia kile wanachofanya, wanaona ni jinsi gani wameweza kusaidia wengine na hii inawapa faraja kubwa. Wanaona hata kama hawana kila wanachotaka, bado wana mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine na hii inawasukuma kufanya zaidi na zaidi na ndio maana wana nafasi kubwa ya kupata kila wanachotaka.

SOMA; Ishi Maisha Haya Kila Siku Na Utakuwa Na Furaha Na Mafanikio.

Acha kujiangalia wewe mwenyewe tu. Anza kuangalia na wale wanaokuzunguka, wanakuchukuliaje wewe na kile ambacho unafanya. Unaweza kuwa unaboresha maisha ya wengine kwa kiasi kikubwa sana, hata kwa kuwa tu mtu mwema.

TAMKO LANGU;

Najua chanzo cha kuona maisha yangu ni mabaya ni kujiangalia mimi mwenyewe na kujipima kwa kile ambacho nilikuwa nataka. Kuanzia sasa nitaacha kujiangalia mimi mwenyewe na kuangalia pia wale wanaonizunguka. Nitaangalia maisha yangu na kile ninachofanya vina mchango gani kwa wengine wanaonizunguka. Najua kupitia wao nitaona jinsi gani maisha yangu yalivyo muhimu kwa wengine, hata kama mimi sioni hilo kwa haraka. Hii itanisukuma kufanya zaidi na zaidi na hivyo kunisogeza karibu zaidi na kile ninachotaka.

NENO LA LEO.

Very little is needed to make a happy life; it is all within yourself, in your way of thinking.

Marcus Aurelius

Unahitaji vitu vidogo sana kuweza kuwa na maisha yenye furaha; na vitu hivi vipo ndani yako, na vinatokana na fikra unazoweka kwenye akili yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.