Katika wakati wowote kwenye maisha yako unaishi kwenye dunia hizi mbili,

Dunia ya kwanza ni ile inayotengenezwa na maisha yako ya kazi. Hii inatokana na kile unachofanya ili kutengeneza kipato chako cha kuendesha maisha. Inaweza kuwa kuajiriwa, kujiajiri au kufanya biashara.

Dunia ya pili ni ile unayotengenezwa na maisha yako binafsi. hii inatokana na yale maisha yako ya kawaida unayoishi, wewe na wale wanaokuzunguka.

dunia mbili

Sasa maisha yangekuwa mazuri sana kama ungeweza kutenganisha dunia hizi mbili, lakini kwa bahati mbaya sana huwezi.

Huwezi kusema kwamba sasa nimemaliza muda wangu wa kazi na nafuta mawazo yangu yote ya kazi ninapoelekea nyumbani. Ukiwa nyumbani bado utakuwa na mawazo ya kazi yako, huwezi kuondokana nayo kabisa, kiasi kwamba ukirudi tena kazini ndio utaanza kufikiria kazi.

Hivyo pia kwenye maisha binafsi, huwezi kuyaondoa kabisa kwenye kazi yako. huwezi kusema sasa nipo kazini na sitaki kabisa kufikiria kuhusu maisha yangu binafsi.

SOMA; Sababu Namba Moja Kwa Nini Hufanikiwi Kwenye Kazi Unayofanya.

Hizi ni dunia mbili unazoishi na zina uhusiano wa karibu sana.

Sasa kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni kwenye kuzifanya dunia hizo mbili kuwa karibu iwezekanavyo. Kadiri unavyoweza kuzifanya dunia hizi mbili kuwa karibu, kuwa zinaendana ndivyo inavyokuwa rahisi zaidi kwako kufikia mafanikio makubwa.

Kama kile unachofanya kinaendana na maisha yako, yaani ni kitu unachopenda, maisha ya kazi na maisha ya kawaida yanakuwa kitu kimoja, na ni rahisi kufanya vizuri sehemu zote mbili.

Ila kama unachofanya kipo tofauti kabisa na maisha yako, yaani hukipendi, basi maisha yako ya kazi yanaweza kuwa hovyo sana na hii ikaambukiza maisha yako binafsi.

Chochote kitakachovuruga moja ya hizi dunia mbili unazoishi kitaambukiza na dunia nyingine.

Linda sana dunia hizi mbili, na anza kwa kuzifanya kuwa karibu iwezekanavyo.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuna dunia mbili ninazoishi kwenye maisha yangu, dunia ya kazi na dunia ya maisha yangu ya kawaida. Ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio nahitaji kuzifanya dunia hizi mbili kuwa karibu sana. Nahitaji kupenda kile ninachofanya na hii itapelekea kupenda maisha yangu pia. Nitalinda dunia hizi mbili kwa sababu najua matatizo kwenye dunia moja yanaleta matatizo kwenye dunia nyingine.

NENO LA LEO.

You face challenges in your personal life and in your professional life. I continue to be relentlessly optimistic and not focus on the negative.

Norah O’Donnell

Unakutana na changamoto kwenye maisha yako binafsi na maisha yako ya kikazi. Endelea kuwa na mtizamo chanya na epuka kuwaza yale hasi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.