Kuna sehemu moja tu ambayo kushindwa kunapatikana na sehemu hiyo ni kaburini.

Ndiyo ni kaburini pekee ambapo kushindwa ndio kunapatikana.

makaburi

Kwa sababu unasoma hapa, naamini hujafika kaburini na hivyo hii ni habari njema kwamba bado hujashindwa.

Mtu pekee ambaye tayari ameshashindwa ni yule ambaye ameshakufa, maana huyu hana njia yoyote anayoweza kutumia kuondoka kwenye kushindwa kwake.

Ila kwa wewe ambaye tayari upo hai, hata kama unapitia magumu kiasi gani, jua ya kwamba bado hujashindwa. Kwa kupata nafasi ya kuendelea kupumua leo tayari una nafasi nyingine nzuri ya kubadili chochote ambacho hakiendi vizuri kwenye maisha yako.

SOMA; THINK AND GROW RICH: Hatua Ya Sita Ya Kuelekea Kwenye Utajiri; Sababu 30 Zinazowafanya wengi Kushindwa.

Magumu yoyote unayopitia jua ya kwamba ni sehemu ya safari na yanakuandaa kwa ushindi mkubwa na wa kishindo uliopo mbele yako. jifunze kupitia hali uliyonayo sasa na kila siku boresha kile unachofanya.

Waliokufa ndio walioshindwa, wewe ambaye bado upo hai una nafasi leo, na sio kesho, ni leo ya kufanya kitu ambacho kitabadili maisha yako. je wewe unachagua kufanya nini leo?

Kumbuka maisha ni lako na chaguo ni lako. Chagua maisha ya ushindi na mafanikio na hakuna kitakachokuzuia. Chagua maisha ya kushindwa na utakuwa umejizika mwenyewe.

TAMKO LANGU;

Kwa sababu bado nipo hai, basi bado sijashindwa. Leo ni siku nyingine nzuri sana ambayo naweza kuitumia vizuri na kuweka misingi ya ushindi na mafanikio. Najua kushindwa kupo kaburini na sitaki kujipeleka kaburini kwa kutaka mimi mwenyewe. Haijalishi napitia nini, mimi ni mwana mafanikio kwa siku zote ambazo nitakuwa naishi. Na kila siku nitachukua hatua ya kunifikisha kwenye mafanikio zaidi.

NENO LA LEO.

The greatest glory in living lies not in never falling, but in rising every time we fall.

Ralph Waldo Emerson

Ufahari mkubwa wa kuishi sio kutokuanguka, bali kusimama tena kila mara unapoanguka.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.