Kuna hatua mbili muhimu sana za wewe kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako, na hapa namaanisha kutoka hapo ulipo na kwenda mbali zaidi kimafanikio.
Hatua ya kwanza ni kujijua wewe mwenyewe. Jua ni nini unataka kwenye maisha yako, ni vitu gani unapendelea, ni nini unaweza kufanya vizuri na nini huwezi kufanya vizuri. Jijue vizuri kama unavyoijua simu unayoitumia.
Hii ni hatua muhimu sana kwa sababu kama waswahili wanavyosema, usichokijua ni sawa na usiku wa giza. Hivyo jijue vyema, sana.
Hatua ya pili ni kujipoteza wewe mwenyewe. Jipoteze kwenye kufanya kile ambacho unaweza kukifanya vizuri sana. Jipoteze kwa kufanyia kazi kile ambacho unakitaka kwenye maisha yako. jipoteze kwa kutoa mchango na tamani kubwa sana kwa wengine.
Hii ni hatua muhimu sana ambayo itakuwezesha wewe kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Ninaposema jipoteze simaanishi upotee au ufanye mambo ya hovyo, bali ufanye kitu kwa uwezo wako wote na kuacha kujijali sana wewe. Usiseme mimi siwezi kufanya hivi, kama hiko ndio unachopenda kufanya, weka mawazo hayo kando na anza kuweka juhudi kwenye kile unachotaka. Sahau kuhusu ufahari wako, sahau kuhusu watu watakuonaje au kukuchukuliaje, sahau kuhusu kushindwa na wewe peleka mawazo yako yote kwenye kile unachofanya. Kwa njia hii hakuna chochote ambacho kitakushinda.
SOMA; Jinsi Ya Kujenga Nidhamu Binafsi.
TAMKO LANGU;
Nahitaji kujijua vizuri sana. Na baada ya hapo nahitaji kujipoteza kwenye kufanya kile ambacho naweza kukifanya vizuri, kile ambacho nakitaka sana kwenye maisha yangu. Hizi ni hatua mbili muhimu nitakazozingatia kwenye maisha yangu.
NENO LA LEO.
The best way to find yourself is to lose yourself in the service of others.
Mahatma Gandhi
Njia bora ya kujijua wewe mwenyewe ni kujipoteza kwenye kuwahudumia wengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.