Kuna matatizo makubwa mawili pale linapokuja swala la kuchukua hatua ili kuweza kufikia malengo na mipango yako. wengi huwa wanafikiri tatizo ni moja tu na hivyo wanapolivuka wanakuwa hawajajiandaa na tatizo lingine ambalo ni kubwa zaidi.
Tatizo la kwanza ni KUANZA. Ndio watu wengi wana malengo na mipango mizuri sana. Yaani mtu akikueleza mipango hiyo unashangaa kwa nini mpaka sasa hujaanza? Zinakuja sababu, nasubiri hiki kiwe hivi, sijajiandaa vya kutosha, sijapata muda w akutosha, na mengine mengi. Na kwa tatizo hili wengi hawaanzi kabisa, na ni sehemu kubwa sana ya watu wanaishi hapo.
Kuna wachache ambao wanafanikiwa kuanza, na wanaanza na hamasa kubwa sana ya kuleta mabadiliko makubwa. Lakini hawafiki mbali kwa sababu wanakutana na tatizo la pili, ambalo ni kubwa na hawakujiandaa nalo.
Tatizo la pili ni KUACHA. Ndio kuna watu ambao wanakuwa na malengo na mipango mizuri na wanafanikiwa kweli kuanza kuitekeleza mipango hiyo. Lakini inawachukua muda kiasi gani kuendelea kuwepo kwenye mipango yao hiyo? Wengi ni muda kidogo sana, kwa sababu huacha. Wanapokutana na changamoto wengi wanashindwa kustahimili na wanaacha.
Sasa leo nataka ufanye tathmini kama usingeacha leo hii ungekuwa wapi?
kama usingeacha biashara ile uliyoanza kipindi kile, unafikiri leo ungekuwa wapi?
kama usingeacha ule mradi wa kilimo uliokuwa umeanza kuufanya leo ungekuwa hapo ulipo?
Kama usingeacha yale masomo uliyokuwa unachukua ili kuendeleza fani yako, je leo ungekuwa wapi?
Kama usingeacha kuendeleza kipaji chako, je ungekuwa na maisha uliyonayo sasa?
Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu alishaacha kitu ambacho ukikiangalia leo unaona ulikosea. Lengo langu sio wewe ujiumize hapa kwa yaliyopita, bali ufanye maamuzi sahihi sana kwako leo hii.
Na maamuzi hayo ni kwamba kuanzia sasa, hutaacha kile ambacho umeamua kufanya, hata iwe nini, lije jua ije mvua, wewe utaendelea kufanya, mpaka pale utakapopata ulichopanga kufanya.
Wanaofikia mafanikio makubwa, huwa hawaachi.
SOMA; Sababu 5 Kwa Nini Ni Marufuku Wewe Kukata Tamaa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba tabia yangu ya kuanza vitu na kuacha ndio imekuwa inanizuia kufikia yale mafanikio ninayotaka. Kuanzia sasa nimeamua ya kwamba sitoacha tena kile ambacho nimeamua kufanya. Nikishaamua kwamba kitu fulani ni muhimu kwangu na nahitaji kukifanya, basi nitakomaa nacho mpaka pale nitakapokipata, hakuna cha kunirudisha nyuma.
NENO LA LEO.
Never give up. Today is hard, tomorrow will be worse, but the day after tomorrow will be sunshine.
Jack Ma
Usikate tamaa. Leo ni ngumu, kesho itakuwa mbaya zaidi, lakini keshokutwa jua litachomoza na mambo yatakwenda vizuri.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.