Hakuna kitu kinakunyonya nguvu kama ambacho umefanya na kuishia njiani. Mawazo yako yanabaki kwenye kitu kile na hivyo kushindwa kusonga mbele zaidi.
Kila utakapofikiria kufanya kitu kipya unajikumbusha kwamba kuna kitu hujamaliza.
Na unapokuwa unafanya kitu halafu ukaishia kati kati, ni vigumu sana kuja kuanza tena, kuja kuanza tena kunaonekana ni zoezi gumu ambalo linahitaji nguvu zaidi. Na hivyo wengi kuendelea kuahirisha na kuendelea kupoteza nguvu kufikiria kitu hiko.
Sasa leo nataka tumalize vitu.
Anza kwa kuangalia vitu vyote ambavyo umeanza kufanya lakini hujamaliza, viorodheshe. Halafu angalia ni kipi muhimu, anza kwa kukifanya mara moja, na kifanye mpaka kiishe. Kama kuna ambacho sio muhimu kikate na jiambie hiki sitaendelea kukifanya tena.
Kwa zoezi hili utajipatia uhuru mkubwa sana ambao ulikuwa umeupoteza kwa kuangalia mrundikano wa vitu ambavyo kila siku umekuwa unasema utamalizia ila humalizii.
Baada ya kumalizana na hivyo viporo sasa weka azimio kwamba kila ambacho utakigusa, hutakiacha mpaka kikamilike. Hakikisha unakamilisha kila unachoanza kwa asilimia 100. Hata kama utafanya vichache bado utaenda mbali kwa sababu unaona ulichofanya.
Ni afadhali kufanya vitu viwili kwa kuvikamilisha kuliko kufanya vitu vitano nusu nusu. Hivi viwili vilivyo kalimika ni mafanikio, hivi vitano ulivyofanya nusu nusu ni mzigo ambao utaendelea kukuvuta na kukuzuia kufanya vitu vingine vizuri.
SOMA; Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.
TAMKO LANGU;
Kuanzia leo nimeamua kuwa mmalizaji. Kwa kila kitu ambacho nilishaanza kufanya kazi nitakimaliza au nitaachana nacho. Na kuanzia sasa nitafanya kile nilichopanga mpaka nikimalize, sitaishia njiani na kusema nitamalizia siku nyingine, najua kwa kufanya hivi ni kujibebesha mzigo ambao utanizuia kufanya mambo mengine kwa ubora.
NENO LA LEO.
Whenever you have taken up work in hand, you must see it to the finish. That is the ultimate secret of success. Never, never, never give up!
Dada Vaswani
Pale unapoamua kuanza kazi, ifanye mpaka itakapoisha. Hii ndio siri kubwa ya mafanikio. Kamwe, kamwe, kamwe usikate tamaa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.