Habari za leo mwanafalsafa?
Karibu tena kwenye kipengele hiki cha FALSAFA MPYA YA MAISHA ambapo tunashirikishana maarifa muhimu ya kuweza kujenga maisha bora sana kwetu. Kama ambavyo wote tunajua, maisha tuliyonayo hapa duniani ni haya tu. Hatutarudi kuja kuishi tena baada ya kuondoka hapa duniani. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha anakuwa na maisha bora na anayoyafurahia.
Leo kupitia falsafa mpya ya maisha tutaangalia eneo muhimu sana ambalo tunahitaji kulifanyia kazi kama tunataka maisha yetu yawe bora sana. Eneo hili ni kuzijua zile tabia za asili za sisi binadamu, halafu kuziepuka. Ukweli ni kwamba kama ukifuata zile tabia za asili kabisa za binadamu, huwezi kupiga hatua kwenye maisha yako. utajikuta unakazana sana lakini unabaki pale pale. Wale wanaofanikiwa ni wanaoweza kuzishinda tabia hizi, japo pia sio kazi rahisi.
Binadamu kama kiumbe hai.
Sisi binadamu ni viumbe hai, na kama viumbe hai tunashirikiana tabia za msingi kabisa za viumbe hai, yaani hapa tunafanana na miti, minyoo na kila aina ya wadudu kwa kuwa wote tunazaliwa na kufa, tunakula, tunapumua, tunatoa uchafu, tunapata hisia na kadhalika.
Tabia hizi za viumbe hai ndio zinatufanya tuendelee kuwepo hapa duniani. Na ni sawa kwa viumbe wote.
Binadamu kama mnyama, mamalia.
Binadamu kama viumbe hai, tupo kwenye kundi la wanyama na ndani ya wanyama tupo kundi la mamalia, kwa lugha rahisi ni wanyama ambao wanazaa na kunyonyesha watoto wao.
Katika kundi hili tunafanana sana na mamalia wengine, hapa namaanisha mbuzi, ng’ombe, panya na kadhalika.
Sisi binadamu tunafanana na mamalia wenzetu kwa karibu kila kitu kasoro kitu kimoja tu.
Yaani kila kitu ambacho unacho wewe, hata mbuzi anacho, ila kuna kitu kimoja cha ziada sisi tunacho na hawa mamalia wengine hawana.
Kitu hiki ni utashi, tunao uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi bora kwetu. Sisi binadamu tunaweza kufanya mambo yetu kwa uhuru, hatufungwi na mazingira kama wanyama wengine, sisi tunao uwezo mkubwa wa kuwatawala hawa wanyama wengine.
Wanyama wengine wanaendesha maisha yao kulingana na mazingira waliyonayo, wanaendeshwa na mahitaji yao ya mwili, wanataka kula wanatafuta chakula, wanataka kulala wanatafuta sehemu ya kulala. Lakini sisi binadamu tuna uwezo mkubwa zaidi ya hapo.
Jambo kubwa na la kushangaza.
Jambo kubwa sana na la kushangaza ni pale ambapo binadamu wengi wanaamua kutokutumia uwezo wao na utashi wao kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yao. Watu wengi wamekuwa wakifanya mambo kwa sababu kila mtu anafanya, hii haimtofautishi mtu na mnyama.
Kwa mfano, kama kuna mbuzi wanapita mahali, kundi kubwa la mbuzi, halafu ukafunga kamba, wale mbuzi wa mwanzo watashindwa kupita na hivyo itawabidi kuruka ile kamba ndio waweze kupita. Mbuzi wanaokuja nyuma watajua kabisa kwamba wakifika pale ni lazima waruke, na wakifika wanaruka. Sasa jambo la kushangaza ni kwamba hata ukiondoa kamba ile, mbuzi wote wanaokuja wataendelea kuruka. Wataendelea kuruka kwa sababu wameona wenzao wanaruka ni hivyo wanajua ndio wanachotakiwa kufanya, hawana haja ya kufikiri zaidi.
Hii ndio hali inayowarudisha watu wengi sana nyuma, kufanya mambo sio kwa sababu ni muhimu kwao, sio kwa sababu wamefikiri na kuona ndio yanawafaa, ila kwa sababu wazazi walifanya, ila kwa sababu marafiki wanafanya, ila kwa sababu kila mtu anafanya.
Hiki ni kifo cha maisha bora na yenye furaha.
Twende kinyume na tabia za asili za binadamu.
Hiyo tuliyoangalia hapo juu ni tabia ya wanyama tu, bado kuna tabia za asili kabisa za binadamu ambazo ni kikwazo sana kwa maisha bora na yenye mafanikio.
Kama kweli tunataka kuwa na maisha bora, kama tunataka maisha ya mafanikio na furaha, tunahitaji kuweka juhudi za ziada kuepuka zile tabia za asili ambazo binadamu tunazo na kwenda kinyume nazo. Tukiweza hili tunakuwa tumevuka kikwazo kikubwa sana cha kuwa na maisha bora na hakuna kinachoweza kutuzuia tena.
Je ni tabia zipi tunahitaji kwenda kinyume nazo?
Zifuatazo ni baadhi ya tabia ambazo binadamu tunazo na zimekuwa zinaturudisha nyuma, wewe kama mtu ambaye umeamua kuwa na maisha bora, unahitaji kuzivuka na kwenda kinyume nazo.
1. Ubinafsi.
Ubinafsi ni tabia ya asili kabisa ya binadamu, tunapenda kujifikiria sisi wenyewe kwanza kabla ya kuwafikiria wengine. Tunahakikisha hali zetu binafsi ni nzuri kwanza kabla hatujafikiri kuhusu wengine. Ndio ubinafsi una faida kwetu kwa sababu ndio umetufanya mpaka leo tumeendelea kuwa hai. Lakini ubinafsi inapokuja kwenye mwingiliano wetu na watu wengine unatunyima fursa nyingi na nzuri za kuwa na maisha bora.
Katika uhusiano na mwingiliano wako na watu wengine, kwenye maisha, kazi na hata biashara, usijifikirie wewe tu, fikiria na wengine pia. Mara zote jiulize mtu mwingine anafaidikaje na kitu hiki.
Kama umeajiriwa jiulize je kile unachotoa kwa mwajiri wako kinamnufaisha au kinanufaisha wale wanaopokea? Badala ya kuangalia wewe unalipwa kiasi gani na kulalamika kwamba kipato hakikutoshi hebu anza kufikiria kile unachotoa kinawanufaishaje wengine.
Kama unafanya biashara pia fikiria hivyo hivyo, kabla hujafikiria ni faida kiasi gani unapata, hebu fikiria kwanza ni thamani kiasi gani unatoa. Fikiria mteja wako anatatuaje tatizo alilonalo kupitia bidhaa au huduma unayotoa. Kwa kufikiri hivi utatoa huduma bora sana na hivyo kujenga biashara nzuri.
2. Uvivu.
Ndio kwa asili sisi binadamu ni wavivu, hatupendi kufanya kazi kwa nguvu, tunapenda kutafuta njia rahisi ya kufanya kazi zetu. Tabia hii pia ni nzuri kwa sababu ni kupitia tabia hii tumeweza kufikiria na kuja na mashine mbalimbali za kurahisisha kazi zetu.
Lakini unachotakiwa kujua ni kwamba, waliogundua mashine za kurahisisha kazi, hawakuwa wamekaa kivivu ndio mashine zikaja, bali walikuwa wanafanya na ndio wakapata njia mbadala ya kurahisisha.
Hivyo wakati wenzako wanaleta uvivu kwenye kazi zao, wewe fanya kwa juhudi kubwa, jitoe kufanya kazi hasa, na wakati unafanya fikiria njia ya kuboresha. Ni lazima uwe tayari kufanya kazi zaidi ya wengine kuliko walivyo wengine. Weka uvivu pembeni.
3. Kutaka kuonekana na kujilinganisha na wengine.
Tabia nyingine ambayo binadamu tunayo, na inaweza isiwe asili ni kupenda kuonekana na kujilinganisha na wengine.
Kila mmoja wetu ana hamu fulani ya kutaka kuonekana ni wa muhimu kwa jamii au pale alipo. Kila mmoja wetu anapenda kuonekana ni mtaalamu wa kitu fulani. Ukitaka kudhibitisha hili, omba mtu akuelekeze mahali ambapo hupajui, ataacha chochote anachofanya na atakuelekeza vizuri sana, tena atakusisitiza kama umeelewa. Kwa nini inakuwa hivi? Kwa sababu anayekuelekeza anajisikia vizuri kwamba anajua kuliko wewe, yeye ni mtaalamu wa eneo hilo kuliko ulivyo wewe.
Watu pia wanapenda kujilinganisha na wengine, kujilinganisha na unaofanya nao kazi, kujilinganisha na uliosoma nao, au mliokuwa pamoja na makundi mengine mengi. Ni katika kujilinganisha huku mtu anajikuta akifanya mambo ambayo sio muhimu kwake ila anafanya tu ili naye aonekane hayupo nyuma.
Unaweza kufanya mambo haya ya kuonekana au kujilinganisha na kwa nje ukaonekana kweli upo, ila ndani yako bado ukawa na upungufu mkubwa sana kwa sababu bado hujatimiza lile ambalo ni muhimu kwako.
Unahitaji kuacha hili la kujilinganisha na kutaka kuonekana, amua ni kitu gani unataka kwenye maisha yako, na anza kukifanyia kazi. Mara kwa mara utajikuta unataka kufanana na wengine, lakini epuka hilo, fanyia kazi kile ambacho kwako ni muhimu, na hata kama kwa nje hutaonekana bali ndani yako utakuwa na furaha kubwa, na haya ndio maisha bora na yenye mafanikio.
4. Kutokupenda kukosolewa.
Watu hatupendi kukosolewa, jaribu kumkosoa mtu, jaribu kumwambia anakosea, na utaona jinsi ambavyo atajitetea kwamba yuko sahihi au sio kosa lake. Hatupendi kabisa kuumizwa ufahari wetu kwamba sisi ni watu muhimu na ni watu wazuri. Tuna kila sababu ya kwa nini mambo hayaendi vizuri na katika sababu hizo hakuna hata moja ambayo inatuhusu sisi wenyewe.
Sasa wewe ondokana na tabia hii, usipinge pale unapokosolewa, usikazane kujitetea, usitake kutoa maelezo, wewe jiulize je hili nililoambiwa ni kweli au lina uhalisia? Kama jibu ni ndio jiulize unawezaje kubadili ili kuwa bora zaidi. Kama jibu ni hapana, achana na yale maelezo ya waliokukosoa na endelea kusonga mbele. Usipoteze muda wako kupinga au kujitetea kama wengine wanavyofanya bali wewe weka juhudi kwenye kile ambacho unakiamini na ulichopanga kufanya.
5. Kupata zaidi ya wengine au kupata zaidi ya unachostahili.
Hii inafanana na ubinafsi ila imeenda ndani zaidi tabia hii. Watu wanapenda kupata zaidi ya wengine au zaidi ya wanachostahili kupata. Na tabia hii ndio inayoleta wizi, ufisadi na mambo mengine ambayo sio ya uaminifu.
Tabia hii pia imesababisha watu wengi kuibiwa au kutapeliwa kwa kuamini kwamba wanaweza kupata zaidi ya wengine au zaidi ya wanachostahili kupata.
Tabia na imani za aina hii zitakupotezea sana muda, kwa sababu mwisho wa siku hutapata na kufurahia chochote ambacho hustahili kupata.
Wewe nenda kinyume na tabia hii, fikiria kile ambacho unastahili kupata, usitafute njia ya mkato ya kupata zaidi, njia ya aina hii ni lazima itakuletea matatizo baadaye. Kuwa mwaminifu na chochote unachotaka, hakikisha unakipata kwa njia ambazo ni halali, hii itakujengea wewe msingi mzuri wa maisha bora na yenye mafanikio.
6. Kuridhika na kile ulichonacho.
Tukishapata yale mahitaji yetu ya msingi, binadamu tuna tabia ya kuridhika, hatupendi kabisa kufikiri zaidi ya pale ambapo tupo sasa.
Angalia wafanyakazi wengi ambao wanapata mshahara wa kawaida na ambao unatosheleza mahitaji yao, husahau kabisa kufikiri nje ya hapo na kuona maisha tayari. Angalia wafanyabiashara wengi ambao biashara zao zinawapa faida ya kawaida, huridhika na kuona maisha tayari yamefika kikomo.
Ni katika hali hii ya kuridhika ambapo mtu anaacha kukua, miaka mingi inaenda na unakuta mtu yuko pale pale alipokuwa. Kama ni kazi yupo kwenye daraja lile lile na anapata kipato ambacho hakina tofauti kubwa sana. Na kama ni biashara unakuta mtu yupo kwenye biashara ile ile kwa miaka mingi.
Sasa wewe unahitaji kuiepuka tabia hii na kwenda kinyume nayo kabisa. Kwa jambo lolote unalofanya usifike mahali na kuridhika kuona ya kwamba wewe ndio umeshayaweza maisha, usione wewe ndio umeshamaliza kila kitu. Kila siku na kila mara fikiria kuwa bora zaidi ya pale ulipo sasa, fikiria kwenda mbele zaidi.
Kufikiria huku kuwa bora au kwenda mbele zaidi hakumaanishi uyaone maisha unayoishi sasa hayafai, badala yake unayakubali maisha ya sasa na kutaka yawe bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Jua utakapoanza kuridhika ndipo umeanza kuchimba shimo la kupotea kabisa.
7. Kusubiri kuambiwa ufanye nini.
Pamoja na uhuru mkubwa ambao sisi binadamu tunao, bado watu wengi hawawezi kujiamulia wao wenyewe wafanye nini. Watu wengi wanasubiri waambiwe ni nini cha kufanya au waone wengine wanafanya nini ndio na wao waanze kufanya.
Kwa tabia hii huwezi kupiga hatua kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako. utabaki nyuma mara zote kwa sababu wakati wewe unasubiri kuambiwa au kuona, wenzako wanachukua hatua na kuzitumia vizuri fursa ambazo zinajitokeza. Unaposubiri kuambiwa au kuona, maana yake unachelewa.
Achana na tabia hii na anza kujituma wewe binafsi, fikiria kile ambacho unataka na mara zote angalia ni fursa gani zinazokuzunguka na ambazo unaweza kuzitumia vizuri kufikia kile unachotaka. Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla. Usisubiri mpaka uambiwe au uone kwa wengine.
Kuweza kutengeneza maisha bora na ya furaha na mafanikio kwako, unahitaji kufanya jitihada za ziada. Sio kitu rahisi lakini pia inawezekana. Angalia yale mambo ambayo watu wanapenda kuyafanya na hayawapeleki mbele na chukua azimio la kutokuyafanya mambo hayo na kufanya kinyume chake.
Ishi maisha ambayo yana maana kwako na sio ambayo kila mtu anaishi, maisha yenyewe tuliyonayo ni haya, usipoyafurahia sasa ni kwamba unayapoteza.
Nakutakia kila la kheri katika kutengeneza falsafa mpya na bora sana kwa maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
Asante sana Kocha kwa Falsafa hii Mpya ya Maisha.
Wiki iliyopita, katika mjadala wetu KISIMANI nilihoji kitu Juu ya “Ni kwanini watu wengi huanza kufikiri sana kiutafutaji baada ya hali kuwa ngumu”.
Tulijadili vizuri mno hili, na Ukaahidi kutupatia njia ya kuepukana na Hili.
Hatimaye Falsafa hii Mpya imetoa suluhisho sasa.
Shukrani sana.
LikeLike
Karibu Malabeja.
LikeLike