Watu wengi wana malengo na mipango mizuri sana.

Lakini sio wote wanaofikia malengo na mipango hii. Subiri, sio wote ambao hata wanaanza kuifanyia kazi. Kuna wengi wanaoishia kwenye hatua hii ya kupanga tu, lakini inapofikia utekelezaji wanasogeza mbele, nitafanya kesho, au nikiwa tayari, au kitu fulani kikiisha.

Tabia ya kuahirisha mambo na kuona utafanya baadaye imewazuia wengi sana kuweza kufikia mafanikio kwenye maisha yao.

Nilishakupa mbinu nyingi sana za kuvuka hili, na leo nakupa mbinu nyingine muhimu.

Mbinu hiyo NI LEO TU…

Kwenye jambo lolote kubwa unalotaka kufanya, kwenye mipango yote mikubwa uliyojiwekea, usiangalie ukubwa na kuona unahitaji nguvu za ziada au muda w akutosha. Badala yake gawa kwenye vipande ambavyo unaweza kufanyia kazi kila siku.

Halafu chukua kipande cha leo na anza kukifanyia kazi. Na kwenye mawazo yako chukulia ni leo tu unafanya hivyo. Hata pale unapopata mawazo ya kuacha na kufanya kingine jikumbushe kwamba ni leo tu unahitaji kufanya hivyo, na kesho mengine yataendelea.

Kwa kuweza kufanya leo kile ulichopanga kufanya, ndio njia ya uhakika ya kufikia mafanikio. Kwa sababu mafanikio hayaji mara moja kama mvua, bali ni mkusanyiko wa siku nyingi zenye mafanikio.

Ni leo tu, na fanya kile ambacho ulipanga kufanya leo, usijipe sababu wala usiache, wewe fanya.

SOMA; Ishi Leo, Mafanikio Yako Yapo Hapa…

TAMKO LANGU;

Ni leo tu ambapo ninafanya hiki ambacho nilipanga kufanya. Sizuiwi na kesho wala sifikirii jana, nafikiria leo ambapo nakamilisha sehemu hii muhimu ya malengo na mipango yangu. Leo tu nafanya hivi, bila ya kuacha na bila ya kutafuta sababu.

NENO LA LEO.

The best preparation for good work tomorrow is to do good work today.

Elbert Hubbard

Maandalizi bora ya kazi nzuri ya kesho ni kufanya kazi nzuri leo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.