Siku zote maisha ya binadamu  yanaongozwa na uchaguzi tunaoufanya kila siku. Uchaguzi huo ndio unatufanya tuwe na maisha haya au yale. Kama uchaguzi unaoufanya ni mbovu kila siku, basi ni wazi na maisha yatakuwa mabovu vilevile. Na kama uchaguzi wako ni mzuri, halikadharika na maisha yako yatakuwa mazuri vivyo hivyo.
Kitu cha kuwa makini nacho hapa, angalia uchaguzi unaoufanya kila siku na kila wakati. Uchaguzi huo ndio unaoamua maisha yako ya kesho yaweje. Kama ni hivyo, ni lazima kwetu kufanya uchaguzi utakaotupa maisha bora. Jaribu kujiuliza, ni uchaguzi wa mambo gani unaotakiwa kuufanya ili kukupa mafanikio makubwa?
1. Chagua kutumia fursa vizuri.
Kwa fursa yoyote inayojitokeza mbele yako, jifunze kuitumia vizuri. Kama ni fursa ya kibiashara au elimu itumie vizuri mpaka uone mafanikio yake. Acha kucheza na fursa yoyote ya kimafanikio inayojitokeza mbele yako. Ikiwa utafanya hivyo elewa ni lazima ipo siku utakuja kujuta kwa uamuzi ulioufanya leo.
Kuna watu ambao wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokuwa makini na fursa zilizojitokeza kwao. Bila shaka umeshawahi kuwaona watu hawa ambao wana majuto na majonzi makubwa kila wakikumbuka ujinga walioufanya. Hili ni tatizo linalosababisha ndoto za wengi kukwama. Ili ufanikiwe, jifunze kutumia kila fursa vizuri.
CHAGUA KUFANYA MAMBO HAYA, ILI YAKUPE MAFANIKIO.
KILA FURSA ITUMIE VIZURI KUKUFANIKISHA.
2. Chagua kuishi na watu chanya.
Siku zote ukiwa mtu wa kuishi na watu hasi basi ni wazi utapata matokeo wanayopata watu hao. Kama ni kulalamika, kulaumu ama kukosa mafanikio, utapata matokeo kama hayohayo. Hakuna kikubwa utakachoweza kukibadilisha. Mara nyingi maisha yetu yanathiriwa sana na wale watu wanaotuzunguka.
Siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye watu wanaokuzunguka pia. Sio rahisi kuishi na watu hasi, halafu ukategemea mafanikio, sahau hilo. Ni lazima watakurudisha nyuma. Watu wenye mafanikio makubwa wanalijua hili. Hata wewe ukitaka kufanikiwa chagua kuishi na watu chanya. Utajifunza mengi huko na utafika mbali kimafanikio.
3. Chagua kufanya kazi kwa bidii.
Kitu kitakachokutoa hapo ulipo na kukufanikisha ni kufanya kazi kwa bidii. Kazi yoyote unayoifanya jitoe kuifanya kwa nguvu zote mpaka uifanikishe. Acha kufanya kazi kwa mkono mlegevu utajikwamisha kwenye kwa mambo mengi kuliko unavyofikiri. Ile hali ya uvivu uliyonayo jitahidi uitoe na kisha endelea kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii.
Watu wenye mafnikio makubwa siku zote wanafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuona mipango na malengo yao yanatimia. Kumbuka hakuna kitu utakachokipoteza ikiwa utajitoa kwa moyo kufanya kazi zako kwa bidii. Zaidi utajiongezea ujuzi, maarifa na uzoefu mkubwa utakaoutumia leo na kesho kwa maisha yako.
4. Chagua kukabiliana na matatizo na kuyashinda.
Tatizo lolote unalokabiliana nalo unao uwezo wa kulishinda. Hakuna tatizo lilokubwa kwako ambalo linaweza likakushinda. Kwa kulijua hilo chukua jukumu la kuchagua kukabiliana na tatizo lako na acha kuruhusu hata kidogo hilo tatizo likakushinda.
Tumia uwezo wako mkubwa wa akili uliopewa, tafakari kisha tafuta njia sahihi za kuweza kukabilana na tatizo lako. Kwa kufanya hivyo utakuwa mshindi na hakuna ambacho kitashindikana kwao. Wanamafanikio wote siku zote huwa ni watu wakukabiliana na matatizo yao na siyo kuyakimbia.
5. Chagua kujifunza.
Ipo haja ya kutafuta mafanikio huku ukiwa unajifunza. Unapojifunza inakusaidia kujua mambo mengi sana ambayo utayatumia katika safari yako ya mafanikio. Huu ni uchaguzi muhimu sana kuufanya ili kujihakikishia nafasi kubwa ya mafanikio katika maisha yako. Jifunze kupitia vitabu, semina au warsha mbalimbali itakusaidia sana.
Hivi ndivyo ambavyo unaweza ukachagua mambo haya na yakawa nguzo na msaada mkubwa wa mafanikio siku zote.
Nikutakie ushindi katika safari yako ya mafanikio na kumbuka tupo pamoja.
Kwa makala nyingine nzuri pia karibu kwenye DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,