Kama utakuwa na ujasiri wa kutosha, na ukafanya kitu kikubwa, ambacho hakijawahi kufanywa na ambacho kinaweza kuwasaidia wengi. Watu hawataacha kusema, na haya ndiyo yatakayosemwa..

Kuna makumi ya watu watasema ningeweza kufanya vizuri kuliko wewe. Hawa watasema wangeweza kufanya vizuri na kwa ubora kuliko ulivyofanya wewe. Lakini cha kushangaza hawakufanya, mpaka wewe umefanya, na bado hawatafanya. Achana nao.

Kuna mamia ya watu watasema wewe ni nani ufanye hivi. Hawa ni wale ambao hawatajali umefanya nini ila wanataka wajue wewe ni nani kwanza. Na hivyo hawatakubali ulichofanya kama hawatakubali wewe ni nani. Achana nao pia.

Kuna maelfu watasema hata mimi nilikuwa na mpango wa kufanya hivyo. Lakini hawakufanya, mpaka wewe umefanya. Achana nao.

Na kuna makumi na mamia elfu ambao hawatajali kabisa, hawatajua hata kama umefanya kitu kikubwa. Usiumizwe na hili pia.

Katika wote hawa kuna wachache sana ambao watajali, ambao watapokea kile ulichotoa, ambao watashukuru wamekipata na ambao watabadili maisha yako. hawa ndio wa wewe kuwajali, hawa ndio wa kuwaangalia na hawa ndio wa kukusukuma ufanye zaidi.

Hongera kwa ujasiri wa kuweza kufanya kitu kikubwa cha kubadili na kuboresha maisha ya wengine. Usihangaike na wale ambao hawajali, hangaika na wale ambao wanajali. Huwezi kumridhisha kila mtu.

SOMA; UKURASA WA 35; Usijaribu Kumfurahisha Kila Mtu.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba jambo lolote kubwa ambalo nitafanya hata liwe zuri kiasi gani sio wote ambao watalipokea kwa mikono miwili. Wengi watatoa kauli za kuonesha kwamba sio muhimu sana au hata wao wangeweza. Watu hawa hawanisumbui mimi kwa sababu mimi najali wale ambao wamelipokea jambo lile kwa njia ya kusaidika.

NENO LA LEO.

You can’t please everyone, and you can’t make everyone like you.

Katie Couric

Huwezi kumridhisha kila mtu, na huwezi kumfanya kila mtu akupende.

Fanya kile ambacho ni muhimu kwako, kile ambacho unajali kweli na utapata wengine wanaojali, ambao wataridhika na kukupenda.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.