Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Naamini falsafa hii mpya ya maisha imeanza kushika kasi kwenye maisha yako, nina imani kabisa ya kwamba sasa unafikiri vyema kabla ya kufanya maamuzi ya maisha yako kwa kuangalia falsafa yetu ya maisha inasemaje. Hongera sana kwa hili kwani ndio linafanya tuweze kuishi maisha tunayoyafurahia na yenye mafanikio.

Karibu tena kwenye mfululizo wetu wa makala za falsafa mpya ya maisha. Juma hili tutajadili eneo muhimu sana kwenye maisha yetu, ambalo tunakutana nalo kila siku. Kwa kuweza kutumia eneo hili vizuri kutatuwezesha kuwa na maisha bora na ya mafanikio. Kushindwa kuelewa na kutumia eneo hili ndio chanzo kikubwa cha matatizo tunayokutana nayo kila siku.

Upacha wa dunia.

Tunaweza kusema kwamba dunia ni pacha, hii ikiwa na maana kwamba vitu vyote vinavyotokea kwenye dunia vipo viwili viwili ambavyo vina uhusiano wa karibu sana. Kila hali tunayopitia kwenye maisha, kila tunachokutana nacho kwenye maisha kipo katika hali ya upacha.

Kwa mfano kuna usiku na kuna mchana, ambapo hii inatokana na kuwepo kwa mwanga au giza. Kuna juu na chini, kuna nyeusi na nyeupe, kuna nzuri na mbaya, kuna kubwa na ndogo, nyembamba na nene, kushinda na kushindwa, kiangazi na masika, kuzaliwa na kufa, upendo na hofu, na mengine mengi. Kila kitu ambacho tunakutana nacho kwenye maisha ni moja kati ya vitu viwili ambavyo ni pacha.

Katika vitu hivi vya upacha, vipo kinyume, na kulingana na uelewa wetu, kulingana na mtazamo wetu tunachagua kimoja kuwa kibaya kwetu na kingine kuwa kizuri kwetu. Hakuna kitu kimoja kizuri kwa wote na kingine kibaya kwa wote, bali mtazamo wetu ndio utatuletea kujua kama kitu ni kizuri au kibaya.

Hali hii ya upacha imekuwepo hivi duniani na itaendelea kuwepo hivi, kwa sisi kuielewa na kuweza kuitumia vyema kutafanya maisha yetu kuwa bora na ya mafanikio.

Jinsi ya kutumia upacha wa dunia kuwa na maisha bora.

Lengo letu kubwa ni kuwa na maisha bora, maisha yenye furaha na kuwa na uhuru na usalama. Lakini ni vigumu kuvipata na kuvifurahia vitu hivi kama hatutajua vizuri dunia inafanyaje kazi. Na kwa kuelewa upacha wa dunia inatuwia rahisi kwetu kuboresha maisha yetu.

Zifuatazo ni njia ambazo unaweza kutumia upacha wa dunia kunufaika nao.

1. Chochote unapitia sasa ni moja ya hali hizo za dunia.

Chochote ambacho unapitia sasa kwenye maisha yako sio kitu kipya, au sio kitu ambacho umekutana nacho wewe kwa mara ya kwanza. Bali ni sehemu ya upacha wa dunia. Kama uko chini maana yake upo kwenye moja ya maeneo mawili, juu na chini. Kama una hofu maana yake upo kwenye upande mmoja wa hofu na upendo.

Kwa kujua upande uliopo na kujua kuna upande mwingine ambao ni bora zaidi kwako, unaweza kuanza kufanya mabadiliko kwenye maisha yako na hatimaye kuboresha maisha yako.

Kuna watu ambao wamekuwa kwenye upande mmoja kwa muda mrefu kiasi kwamba wanaamini ni upande huo tu ndio uliopo, au wanaona walizaliwa kuwa kwenye upande huo tu.

Kwa mfano kuna watu wamekuwa kwenye umasikini maisha yao yote na kuamini wao walizaliwa na watakufa masikini. Kuna watu ambao wamekuwa hawana furaha maisha yao yote na kuamini kwamba walizaliwa kuishi maisha ya kutokuwa na furaha.

Ukweli ni kwamba hali zote hizi mbili za upacha wa dunia, zipo huru kwa kila mtu. Hakuna mtu aliyezaliwa awe upande mmoja tu. Bali kila mtu anaweza kufaidi kila upande kama atajua ni jinsi gani ya kufikia upande ule. Kama kwa sasa upo kwenye upande wa umasikini, jua ya kwamba kuna upande wa pili ambao ni wa utajiri na pia na wewe unaweza kufika upande huo pia. Unachohitaji ni kuzijua mbinu sahihi za kukufikisha upande huo.

2. Kujua ulipo ni sehemu nzuri ya kuanzia.

Katika hali hii ya upacha, kujua ulipo ni sehemu nzuri sana ya kuanzia ili kuboresha maisha yako. ili maisha yako yawe bora, ina maana inabidi yatoke sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Sasa ni sehemu ipi ambapo yanatoka? Na ni wapi yanakwenda? Kwa kujua upacha wa dunia ni rahisi kujibu maswali hayo. Na pia inakuwezesha kujua unaelekea wapi.

Kwa mfano kama upo chini, maana yake unajua ya kwamba hakuna chini zaidi ya hapo unaweza kwenda. Kama huna kazi, maana yake hakuna kibaya zaidi ya hiko kinaweza kutokea. Sasa kazi kubwa kwako ni kuelekea ule upande ambao ni bora kwako. Kama upo kwenye upande ambao sio bora kwako, angalia ule ambao ni bora kwako na anza kuufanyia kazi ili kuupata.

3. Hakuna ubaya kwenye upacha huu wa dunia, sisi ndio tunatakiwa kutafuta mlinganyo.

Kuna watu ambao wanaweza kuona usiku ni mbaya kwao, lakini pia wengi wanaona usiku ni mzuri sana kwao. Labda wewe unafanya biashara ambayo wateja wanapatikana mchana, na mwingine anafanya biashara ambayo wateja wanapatikana usiku.

Kuna ambao wanapenda masika na kuna wengine wanaopenda kiangazi.

Katika hali hizi mbili zilizopo kwenye kila kitu na kila hali, hakuna ambayo ni mbaya na ambayo ni nzuri. Bali kila mmoja wetu ana hali ambayo ni bora kwake na nyingine sio bora. Kwa kujua hivi inakusaidia wewe kujiandaa na kutumia vizuri ile hali ambayo ni bora zaidi kwako.

4. Dunia ni kitu kimoja.

Hali hii ya upacha inatuonesha kwamba dunia ni kitu kimoja na sisi wote tumeunganishwa na nguvu moja. Kwa sababu watu wote duniani tunapitia hali hizi mbili ina maana wote tupo chini ya nguvu moja.

Kutofautiana kwetu kwa jinsi tunavyochukulia ile hali tunayopitia hakutufanyi kuwa na dunia mbili tofauti, bali kunatufanya kuona kwamba kila mmoja wetu ana mahitaji tofauti. Sisi sote ni kitu kimoja ila tuna mitazamo tofauti na matarajio tofauti.

5. Baada ya hali moja inafata hali nyingine.

Baada ya mchana utafuata usiku, huwezi kuzuia hilo, hata ungekuwa unatamani sana mchana uwe mrefu ili ufanye yako, mchana ukiisha unakuja usiku. Hivyo pia kwenye hali zetu za kawaida, baada ya kupanda kunakuja kushuka.

Sasa kulielewa hili kunakufanya wewe ujiandae vizuri sana ili ile hali ambayo ni bora inapokuja upande wako, unahakikisha unaitumia vizuri ili hata inapoondoka haikuachi kwenye hali mbaya.

Kwa mfano kila mmoja kwenye maisha yake ana wakati ambao anatengeneza kipato kikubwa sana, tunasema kipindi chake cha utajiri, lakini kipindi hiki huwa hakidumu milele, yaani hutaendelea kuwa unaweza kutengeneza fedha kwa kiasi hiko kupitia kazi zako wewe mwenyewe. Kwa kujua hili unaanza kujiandaa mapema, wakati ambao upo juu unafanya uwekezaji mzuri ambao hata utakaposhuka bado utakuwa na kipato kizuri na maisha yako kuendelea kuwa bora.

Tumekuwa tukiona mifano ya watu waliokuwa matajiri na mashuhuri kama wanamuziki wakiishia kuwa na maisha mabovu sana. Hii inatokana na wao kutokujua hali hii ya upacha, walipokuwa juu walifikiri watabaki juu milele, na hivyo kujisahau kuandaa kitu kitakachowafanya waendelee kuwa juu kimaisha hata kama sio juu kwenye kile walichokuwa wakifanya.

Hii ndio hali ya upacha ya dunia ambayo tunaishi, kikubwa cha kuelewa na kufanyia kazi ni kwamba hapo ulipo hukuzaliwa uwe hivyo na uendelee kuwa hivyo mpaka utakapokufa, unaweza kwenda upande mwingine. Na pia unapokuwa kwenye ule upande ambao ni bora kwako, hakikisha unautumia vizuri ili maisha yako yaendelee kuwa bora hata pale hali inapobadilika.

Nakutakia kila la kheri katika utekelezaji wa falsafa hii mpya ya maisha yetu, na tukawe na maisha bora sana.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

AMKA CONSULTANTS