Mpenzi msomaji ni wakati mwingine mzuri wa kujipatia kitabu cha kujisomea kwa mwezi huu wa kumi na moja. Kumbuka kila mwezi umekuwa ukipatiwa kitabu kimoja cha kujisomea na kama umeweza kusoma vitabu vyote ambavyo umetumiwa na kufanyia kazi yale uliyojifunza, utakuwa umeanza kuona matunda mazuri ya yale unayojifunza.
Vitabu ni hazina kubwa sana ya kila mmoja wetu kuweza kupata maarifa bora yanayoweza kuyafanya maisha kuwa bora zaidi. Kwa kujipatia kitabu kimoja cha kusoma kila mwezi, hata kama huna muda kiasi gani, ukijiwekea utaratibu wa kusoma kurasa kumi tu kwa siku, ndani ya siku 30 unakuwa umemaliza kitabu.
Ni muda gani unahitaji kusoma kurasa 10? Dakika kumi na tano zinatosha, au kama unasoma taratibu basi dakika 30 zinatosha sana.
Je unapata wapi dakika hizi 30? Angalia ni kitu gani unafanya sasa ambacho sio muhimu sanana acha kukifanya, tumia muda huo kujisomea.
Bado unaona huwezi kupata muda? Basi usiwe na shaka kwa sababu kitabu utakachokwenda kusoma mwezi huu wa novemba kitamaliza kabisa tatizo lako la kukosa muda.

 
Mwezi huu tunakwenda kusoma kitabu kinaitwa TIME WARRIOR, kwa kiswahili tunaweza kusema shujaa wa muda. Kama unavyojua mashujaa, ni watu ambao wanafanya mambo makubwa. Ni watu ambao wanaonekana hawana huruma pale linapokuja jambo sahihi la wao kufanya, huwa wanaacha kila kitu nakuhakikisha wanafanya lile ambalo ni muhimu sana kwao.
Hivi ndivyo na wewe utakavyokuwa baada ya kusoma kitabu hiki, utakuwa shujaa wa muda, utaweza kupangilia muda wako vizuri, utaweza kufanya yale ambayo ni muhimu kwako bila ya kuacha. Na ukishaweza kudhibiti na kutumia muda wako vizuri, basi hakuna kitakachokushinda kwenye dunia hii.
Changamoto kubwa ya muda tuliyonayo sasa.
Pamoja na kwamba kwa sasa tuna vifaa vingi vya kusoma na kutunza muda, bado matumizi ya muda yamekuwa changamoto kubwa kwetu. Katika vizazi vyote ambavyo vimewahi kuwepo hapa duniani, kizazi hiki ndio kinapata shida sana na muda. Na hii inatokana na maendeleo ya kiteknolojia.
Ukiangalia tu simu ya mkononi, hasa hizi simu janja(smart phone) ni kitu kimoja kinachotupotezea muda sana. Sasa hizi mawasiliano yamekuwa rahisi na yamekuwa hayana kikomo. Ni kuwasiliana masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki. Simu hizi zina kila kitu kwenye mtandao, na mitandao ya kijamii. Ambayo inavutia sana kutembelea, lakini haina mchango mkubwa kwenye malengo yetu.
Hii ni changamoto kubwa sana inayowafanya watu kushindwa kutumia muda wao vizuri.
Vitu binafsi vinavyokufanya ushindwe kutumia muda wako vizuri.
Pamoja na vitu hivi vya nje kama simu na teknolojia nyingine kuwa vinakuibia muda, wewe mwenyewe umekuwa unajiibia muda wako mwenyewe, kwa kuchagua kufanya baadhi ya mambo ambayo yanakuzuia wewe kufikia lengo lako.
Katika kitabu hiki tunachokwenda kusoma mwezi huu, kuna baadhi ya vitu ambavyo utakwenda kujifunza vinavyotokana na wewe. Vitu hivyo ni;
1. Tabia ya kuahirisha mambo.
Tabia ya kuahirisha mambo au kwa kizungu wanaita procrastinatio, ni sumu kubwa sana kwako kuweza kufanyia kazi malengo na mipango yako. watu wengi huweka mipango mizuri lakini inapofikia wakati wa utekelezaji wanashindwa kuanza na hivyo kuahirisha.
Katika kitabu hiki, mwandishi ametoa dawa rahisi sana na ya uhakika ya kuondokana na tabia hii ya kuahirisha mambo. Yaani ni rahisi kiasi kwamba ukianza kuitumia utasahau kama ulikuwa na tabia ya kuahirisha mambo, nisikumalizie uzuri huu kwa sababu utausoma na kuelewa vizuri wewe mwenyewe.
2. Kutaka kuwafurahisha watu.
Changamoto nyingine ambayo mwandishi ameielezea vizuri ni tabia ya wewe kutaka kuwafurahisha watu. Unajua kuna neno moja zuri sana ambalo ukilitumia utaweza kutunza muda vizuri sana, neno hilo ni HAPANA. Kama ukiweza kusema hapana kwa mambo yale ambayo sio muhimu kwako, utapata muda mwingi w akufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.
Lakini huwezi kusema HAPANA, kwa sababu unaogopa watu watakuchukia, unaona watakuchukuliaje. Na hapa ni pale mtu anakuomba ufanye jambo ambalo halina umuhimu wowote zaidi ya kupoteza muda, na wewe unasema NDIO ili tu kumfurahisha. Tabia hii inakupotezea muda na heshima pia.
Mwandishi atakufundisha jinsi ya kusema HAPANA kwa heshima, unaweza kumwambia mtu yeyote HAPANA, hata kama ni mzazi wako au bosi wako na akakuheshimu sana kutokana na kile utakachofanya. Unataka kujua njia hiyo bora ya kusema HAPANA? Jibu lipo ndani ya kitabu hiki, kisome.
3. Kutokujiamini.
Hakuna tabia inayofanya mtu ashindwa kuwa na matumizi mazuri ya muda kama kutokujiamini. Kama hujiamini utajikuta unafanya mambo ambayo sio muhimu kwako. Utajikuta unajaribu jaribu vitu vingi na kuviacha. Mwandishi atakupa mbinu ya kuondokana na kutokujiamini ili uweze kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.
4. Kujipa majukumu mengi kwa wakati mmoja.
Kuna watu huwa wanafikiri wakiwa na majukumu mengi kwa wakati mmoja ndio wanatumia muda wao vizuri. Wengine wanafikiri kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ndio kuokoa muda. Kwa taarifa yako hakuna kitu kinakupotezea muda kama kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja.
Katika kitabu hiki mwandishi anakupa mbinu ambayo itakuwezesha kuchagua kile ambacho ni muhimu zaidi, kukifanya mpaka kikamilike halafu kuenda kwenye kingine.
Soma kitabu hiki,
Wewe ni rafiki yangu na naomba nikusisitize sana, soma kitabu hiki. Hiki ni kitabu ambacho kitakupa mbinu rahisi na unazoweza kuanza kuzitumia leo. kwa mfano kuna mbinu rahisi ya kuweza kumfanya mtu abadili tabia zake ambazo wewe huzipendi, na mbinu hiyo haihusishi kumwambia chochote kuhusu tabia zake hizo.
Kitu kimoja kizuri sana kuhusu kitabu hiki ni kwamba kina sura ndogo ndogo 101, na kila sura ni angalau ukurasa mmoja. Hivyo ukigawa kusoma sura hizi ndogo ndogo nne tu kwa siku, kitu ambacho hakitazidi dakika kumi, utamaliza kabisa kitabu hiki.
Kumbuka kusoma sura chache na kufanyia kazi kile ulichojifunza.
Kupata kitabu hiki jiunge na AMKA MTANZANIA kwa kubonyeza haya maandishi na kuweka taarifa zako, kisha subscribe. Baada ya hapo utatumiwa email ya kuconfirm na ukishaconfirm utatumiwa email nyingine yenye kitabu hiki na vitabu vingine vya nyuma kama ulikuwa hujapata nafasi ya kuvisoma. Kama tayari ulishajiunga na AMKA MTANZANIA nenda kwenye email yako na utakuta makala hii hii na mwishoni kuna sehemu ya kubonyeza ili kupakua kitabu hiki.
Mwaka ndio unaisha, kama hujasoma kitabu chochote mwaka huu angalau soma kitabu hiki kimoja tu, na utakuwa umeitendea nafsi yako haki kwa mwaka huu.
N;B Rafiki yetu Daudi Mwakalinga amefanya uchambuzi mzuri sana wa kitabu hiki, unaweza kuusoma hapa ili kupata mwanga zaidi, lakini hakikisha pia umesoma kitabu hiki. Soma uchambuzi wa kitabu hiki kwa kufungua maandishi haya; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha TIME WARRIOR (Shujaa Wa Muda).
Nakutakia usomaji mwema na fanyia kazi yale ambayo umejifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS