Unasoma hapa kwa sababu unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako. kama hutaki mafanikio ni vyema ukaacha kuwa unasoma makala hizi fupi za kurasa kila siku.
Tumekuwa tunajadili mengi sana kuhusiana na safari yetu ya mafanikio. Mbinu za kufikia, changamoto za kuvuka na kadhalika.
Leo tutaangalia moja ya changamoto, ambayo wengi bado hatujaijua vizuri.
Changamoto hii ni kwamba hujui ambacho hujui. Sijui kama unaelewa hiyo sentensi vizuri.
Iko hivi, kuna vitu vingi ambavyo huvijui kuhusu mafanikio, na mbaya zaidi wewe mwenyewe hujui kama huvijui vitu hivyo. Hivyo hujui, na wakati huohuo hujui kama hujui.
Inakuwaje?
Unapoweka malengo na mipango yako, unajaribu kujibu kila kitu kuhusiana na unapokwenda, unajaribu kuziangalia changamoto unazoweza kukutana nazo na kuziwekea njia ya kuzitatua.
Lakini pamoja na malengo na mipango hii mizuri, bado utakapoanza kutekeleza utakutana na changamoto ambazo hata hukuzifikiria kwenye mipango yako. utajifunza vitu vingi sana kwenye utekelezaji kuliko ulivyokuwa unafikiri wakati unaweka mipango yako.
Kwa nini hii ni vizuri sana kwako?
Kwa sababu inakusaidia kuanza, hata kama huna uhakika. Moja ya vitu vinavyowazuia watu wengi kuanza kutekeleza mipango yao ni kujiona kwamba bado hawajakamilika.
Watu hujidanganya kwamba nikishakamilisha hiki ndio nitafanya kile, wakiamini wanaweza kujiandaa kwa ubora zaidi. Lakini hata ungejiandaa kwa ubora kiasi gani, bado hujui ambacho hujui na njia pekee ya kujua kile ambacho hujui ni kuanza kufanya.
SOMA; MUDA; Nusu Ya Muda Wa Maisha Yako Unaipoteza Na Hujui Inapotelea Wapi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kuna vitu vingi ambavyo sivijui, na mbaya zaidi sijui kama sijui. Pia nimejua njia bora ya kujua ambacho sijui kwamba sijui ni kuanza utekelezaji wa malengo na mipango yangu. Najua hata nikijiandaa vizuri kiasi gani, bado kwenye utekelezaji nitakutana na changamoto ambazo sikuwahi kuzifikiria. Nitaanza utekelezaji wa mipango yangu mara moja nikijua ya kwamba nina nafasi ya kujua ambavyo sijui kwamba sijui.
NENO LA LEO.
“True wisdom is knowing what you don’t know”
― Confucius
Hekima ya kweli ni kujua kile ambacho hukijui.
Yaani kujua kuna vitu hujui na ni vitu gani hivyo ambavyo huvijui. Na njia bora ya kujua kwamba kuna vitu huvijui ni kufanyia kazi mipango yako. Anza sasa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.