Mpaka sasa unajua ya kwamba furaha sio kitu fulani ambacho unakifikia. Yaani kwa lugha nyingine huwezi kuikimbiza furaha, kwamba ukishafikia kitu fulani tu unakuwa na furaha. Furaha ni kitu ambacho kinaanzia ndani yako mwenyewe na mara nyingi haitegemei sana mazingira ya nje.
Kwa mfano watu wengi hufikiri labda wakiwa na fedha nyingi ndio watakuwa na furaha, wanakazana kupata fedha lakini wanapokuwa nazo nyingi bado wanaona kuna kitu kinakosekana, bado wanaona kuna kitu hakiko sawa. Ile furaha ambayo walikuwa wanafikiri wangeipata hawaioni.
Furaha inaanzia ndani ya mtu mwenyewe, na kuna vitu ambavyo vinaweza kuchangia wewe kuwa na furaha au la bila hata ya kujali ni mazingira gani uliyopo. Leo katika makala hii tutajadili viungo vitatu muhimu sana kwa furaha. Kwa kuvijua na kufanyia kazi viungo hivi vitatu utakuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.

 
Kiungo cha kwanza cha furaha; UBOBEZI.
Kila mmoja wetu kuna kitu ambacho anafanya kwenye maisha yake ili kujiingizia kipato na kutoa mchango wake kwa wengine pia. Inaweza kuwa kazi ya kuajiriwa, kazi binafsi au biashara. Chochote kile unachofanya, kina mchango mkubwa sana kwenye furaha yako na mafanikio yako kwa ujumla.
Kadiri unavyokuwa umebobea kwenye kile unachofanya, ndivyo inavyochangia wewe kuwa na furaha. Yaani kama unaweza kufanya kile unachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana, ukatoa huduma bora sana kwa wale ambao wanakutegemea uwahudumie basi hii itakuwa na mchango mkubwa kwenye furaha yako.
Unapokuwa umebobea na unafanya kwa ubora, unakuwa unajiamini na hivyo kuona unatoa mchango mkubwa sana kwa wengine. Kwa kujiamini na kuona wengine wanakutegemea wewe unaona una mchango mkubwa kwa wale wanaokuzunguka. Hili lina mchango mkubwa sana kwenye furaha yako.
Kama hujabobea kwenye kile unachofanya, kama unafanya tu kwa kawaida au chini ya kiwango, utaona hutoi mchango mkubwa kwa wengine, na huenda ukawa unalalamikiwa. Hili litakufanya ujione huwezi, ujione wa chini na hivyo kukosa furaha kwenye maisha yako.
Na kama kile unachofanya kinakupa changamoto, au hukipendi na hivyo kuwa na matatizo ya mara kwa mara, yataathiri sana maeneo yako mengine ya maisha.
Unawezaje kujijengea ubobevu?
Kwa kuwa kubobea na kufanya kwa ubora ni kiungo muhimu cha furaha kwenye maisha yako, unawezaje kujijengea hili ili uwe na furaha?
Kwanza; penda kile ambacho unafanya, kwa kuanza kwa kupenda unachofanya utakuwa tayari kuweka juhudi za ziada ili kuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Tafuta kitu unachopenda ufanye, au anza kwa kupenda hiko unachofanya sasa, hata kama ni kwa muda mfupi.
Pili; kila siku boresha kile unachofanya, isije hata siku moja ukafanya kwa mazoea, usifanye kwa sababu jana ulifanya, fanya kwa sababu leo unataka kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa jana, na utaona ubora mkubwa kadiri siku zinavyokwenda.
SOMA; Kauli Kumi(10) Zitakazobadili Mtazamo Wako Kuhusu Furaha Na Kukuwezesha Uwe Na Furaha Ya Kudumu.
Kiungo cha pili cha furaha; MAHUSIANO.
Mahusiano yako na wale wanaokuzunguka yana mchango mkubwa sana kwenye furaha yako. Unapokuwa na mahusiano mazuri na wale wanaokuzunguka utakuwa na furaha na kama mahusiano yatakuwa mabaya, utakosa furaha.
Mahusiano ni muhimu sana kwenye furaha yako kwa sababu yanakuonesha ni kiasi gani wewe ni muhimu kwa watu wengine. Hata kama ungekuwa na mali kiasi gani, kama huna mahusiano mazuri na watu wengine huwezi kuwa na furaha, wala kufurahia mali hizo. Hii ni kwa sababu utaona huna umuhimu wowote kwa wengine. Na sisi binadamu ni viumbe wa mahusiano, kadiri tunavyokuwa muhimu kwa wengine ndivyo maisha yetu yanakuwa na maana.
Unapokuwa na mahusiano mazuri na wanaokuzunguka, iwe ni familia, ndugu jamaa na marafiki, watu unaofanya nao kazi, inakufanya ujue kuna watu ambao wako na wewe hata kama unapitia magumu. Hii itakupunguzia wewe uchungu wa yale magumu unayopitia kwa kujihakikishia kwamba kuna watu wapo kwa ajili yako, hata kama hawatakupa msaada wa moja kwa moja.
Unawezaje kujenga mahusiano mazuri?
Ishi vizuri na watu, jua ni mchango gani wako ni muhimu kwao na utoe. Kuwa na mawasiliano mazuri na wale wanaokuzunguka na pia shirikiana nao kwa yale mambo ambayo yanawaleta pamoja.
SOMA; Kama Unafikiri Vitu Hivi Ndivyo Vitakupa Furaha Ya Kweli Katika Maisha Yako, Unajidanganya Mwenyewe.
Kiungo cha tatu cha furaha; UHURU.
Utakuwa na furaha kadiri unavyojua ya kwamba una uhuru mkubwa na maisha yako. pale ambapo unakuwa na uhakika kwamba wewe ndiye kiongozi wa maisha yako, wewe ndiye mwamuzi wa maisha yako, na wewe ndio unaweza kuyapeleka maisha yako mbele zaidi.
Pale unapoona huna mamlaka yoyote na maisha yako, pale unapoona wengine ndio wanaoweza kujenga au kubomoa maisha yako, unakosa furaha na utaona maisha yanaenda tu. Utaona huna nguvu yoyote kwenye maisha yako na lolote litakalotokea utaona ni bahati nzuri kama ni jema au ni bahati mbaya kama sio jema.
Kadiri unavyokuwa huru na maisha yako, kadiri unavyofanya maamuzi muhimu ya maisha yako na kuyasimamia, ndivyo unavyokuwa na furaha.
Unawezaje kujijengea uhuru?
Uhuru unaanza na wewe mwenyewe, unaanzia kwenye fikra zako mwenyewe.
Kwanza huwa unalalamika na kulaumu wengine? Tayari huna uhuru, hivyo acha mambo hayo mara moja. Badala ya kuona wengine ndio wana jukumu la kufanya kitu fulani, jipe wewe jukumu hilo. Kama kuna jambo ambalo hupendi limetokea, jipe jukumu la kurekebisha, hayo ni maisha yako, na wewe ndio mwenye uamuzi wa mwisho.
Pili; chukua hatua. Uhuru hautakuja kama haupo tayari kuchukua hatua. Kwa kusema na kupanga ni vigumu sana kuona mabadiliko. Lakini unapochukua hatua ni njia muhimu ya kuanza kudai uhuru wako. Kitu chochote ambacho unaona ni muhimu kwenye maisha yako, anza wewe kuchukua hatua ya kuhakikisha kinakuwa bora. Kama kipato ulichonacho sasa hakikutoshi, badala ya kukaa na kusema hakitoshi au kulaumu mwajiri wako, anza kuchukua hatua ya kukiongeza wewe mwenyewe. Anza kwa kuangalia ni maeneo gani unaweza kumsaidia mwajiri wako na yeye akakuongeza wewe kipato. Au angalia ni maeneo gani unaweza kufanya wewe na ukaongeza kipato chako. Hii ni njia bora zaidi ya kuhakikisha una uhuru na maisha yako na hata na kipato chako.
SOMA; Kwa Nini Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Na Furaha.
UBOBEVU…… MAHUSIANO…. UHURU……
Hivi ni viungo vitatu muhimu sana kwa maisha yenye furaha. Na uzuri ni kwamba unaweza kuanza kuvifanyia kazi leo bila ya kujali maisha yako wapi kwa sasa na upo kwenye mazingira gani. Hata kama huna fedha kabisa, unaweza kuanzia hapo na vitu hivyo vitatu na siku zijazo maisha yako yakawa mbali zaidi.
Chukua sasa hatua ya kujijengea furaha ya kudumu kwenye maisha yako ili uwe na maisha bora na yenye mafanikio. Kumbuka hatuwi na furaha kwa sababu tumefanikiwa, bali tunafanikiwa kwa sababu tuna furaha. Yaani kati ya furaha na mafanikio, kinachoanza ni furaha na ndio unapata mafanikio ya kudumu. Usifanye kinyume chake, utaharibu maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi hili ulilojifunza leo.
Rafiki na Kocha wako.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS