Habari za leo mwanafalsafa?
Karibu tena kwenye makala zetu hizi za falsafa mpya ya maisha ambapo tunapata maarifa sahihi ya kuishi maisha yetu kwa furaha na mafanikio. Kila mmoja wetu anastahili maisha bora, ya furaha kwake na mafanikio makubwa. Lakini wengi hawapati nafasi ya kuishi maisha hayo kutokana na kukosa maarifa mazuri ya kuwawezesha kuwa na maisha hayo. Wewe umepata nafasi hii ya kupata maarifa ambayo wengi hawayapati, hivyo hakikisha unayafanyia kazi ili uweze kuona tofauti kubwa kwenye maisha yako.
UTANGULIZI; Kuna Nguvu Inakuzuia.
Leo tutakwenda kuangalia kipengele kingine muhimu sana kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha ambapo tutakwenda kupata uhuru mkubwa sana wa maisha yetu. Pamoja na juhudi kubwa tunazofanya kwenye maisha yetu, kuna nguvu kubwa sana inayoturudisha nyuma. Kuna nguvu kubwa sana inayotuzuia kuchukua hatua. Mara zote tunajua kabisa ni nini tunachotaka, na tunajua hatua za kuchukua, lakini tunapotaka kufanya hivyo nguvu hii kubwa inaturudisha nyuma. Mwisho tunajikuta tuna maisha ambayo hatuyapendi, hatuyafurahii na sio ya mafanikio.
Kabla hatujaangalia nguvu hii kubwa sana ambayo imekuwa inawarudisha wengi nyuma, naomba nikuulize maswali na ujijibu kwa uaminifu kabisa kama imewahi kutokea kwako au umewahi kufanya hivyo.
Je umewahi kuwa unataka kufanya biashara fulani ambayo unaona ni nzuri sana kwako, una hamasa kubwa na unakutana na marafiki zako kuwaambia biashara hiyo. Unakuwa unategemea nao wahamasike kama wewe lakini wanaanza kukuambia una mawazo ya ajabu na haiwezekani? Na wewe ukawasikiliza na kuacha?
Je umewahi kuwa unataka kusoma kitu fulani kwa sababu ulikuwa na ndoto fulani ya maisha yako, lakini mzazi au wazazi wako wakakwambia huwezi kusomea hiko hakina maana, badala yake somea hiki hapa ndio chenye maana na utakuwa na maisha mazuri?
Je umewahi kupata mchumba, ambaye mnapendana sana na mkaona mnaweza kuishi pamoja, lakini ulipompeleka kwa wazazi wako wakakwambia haiwezekani kabisa wewe kuoana na mtu huyo? Au ulipowaambia marafiki zako kuhusu mtu huyo wakakwambia umekosea njia, wala hata hamuendani?
Je umewahi kuamua kufanya kazi zako kwa ustadi mkubwa, kuongeza thamani na kutoa mchango mkubwa na wenzako wakaanza kukusema kwamba una kiherehere, unataka uonekane na mengine mengi hivyo ukalazimika kuacha?
Kama umejibu ndio kwa swali lolote hapo juu au umewahi kuacha kufanya kitu kwa sababu wanaokuzunguka hawajakidhibitisha, basi umeshaathiriwa na nguvu hii kubwa. Na huenda hata hapo ulipo sasa, nguvu hii imekushikilia kwenye mambo mengi sana. Leo utapata dawa ya kumaliza kabisa nguvu hii inayokurudisha nyuma.
SEHEMU YA KWANZA; Nguvu Inayokuzuia Kuwa Na Maisha Ya Furaha Na Yenye Mafanikio.
Ni nguvu gani ambayo inakurudisha nyuma?
Kuna nguvu kubwa sana ambayo inakazana kuturudisha nyuma. Na nguvu hii ni ile hofu ya kukataliwa na wengine na hivyo kutaka kuwaridhisha wengine hata kama sio kitu unachopendelea.
Mara nyingi umekuwa unafanya mambo kwenye maisha yako, sio kwa sababu ni muhimu sana kwako, bali kwa sababu ndio mambo ambayo yanakubalika. Ndivyo wazazi wako wanataka ufanye, hata kama umeshakuwa mtu mzima. Ndivyo ambavyo marafiki zako wanataka ufanye, kwa sababu hata wao wanafanya hivyo pia. Ndivyo ambavyo watu wa elimu yako wanapaswa kufanya.
Nguvu hii imekuwa gereza ambalo limefunga mafanikio ya wengi sana. Ni nguvu ambayo imeua vipaji vingi, imepora uhuru wa wengi, ili tu wakubalike na wale wanaowazunguka.
Chimbuko la nguvu hii.
Nguvu hii ya kutaka kukubalika na wengine, ya kufanya kile ambacho wengine watakikubali, haijaanza leo wala haijaanza na wewe. Ilianza na babu zako wa kale sanaa, zamani mno, miaka mingi kabla hata hatujaanza kuhesabu hii miaka ya baada ya kuja kristo.
Watu hawa wa zamani sana waliishi porini, karibu sana na wanyama, na hivyo kilichowasaidia kupona ni kuwa pamoja, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kwa zama hizo kama ungeamua kufanya unavyotaka mwenyewe, ungeachwa porini na wanyama wangekutafuna au ungekufa kwa hali mbaya ya hewa, kama baridi kali. Hivyo ilikuwa ni lazima ufanye kile ambacho kila mtu anafanya, ili usionekane wa tofauti, na hivyo kuachwa mwenyewe.
Akili zetu zinachelewa kufanya mageuzi.
Pamoja na miaka mingi sana kupita tangu enzi hizi za maisha magumu, bado akili zetu zimesalia kule. Kumetokea mageuzi makubwa sana ya kijamii, lakini akili zetu hazijafikia mageuzi haya makubwa. Hivyo zinaendelea kufanya kazi kwa zama zile za zamani.
Hii ina msaada mkubwa kwa viumbe wachanga, kama watoto wadogo, ambao kuishi kwako kunategemea kile kinachofanywa na watu wazima. Hivyo ni muhimu kwao kufanya kile ambacho kinafanywa na wale waliowatangulia.
Tofauti ya binadamu na wanyama wengine.
Tofauti yetu sisi binadamu na wanyama wengine, tumeshajifunza tena hili, ni uwezo wetu wa kufikiri. Kila kitu tulichonacho, hata mbuzi anacho. Ila akili yetu sisi ina uwezo mkubwa wa kufikiri kuliko wanyama wengine.
Na akili zetu zinafikia uwezo huu mkubwa wa kufikiri katika umri wa utu uzima ambao ni karibu na miaka 20.
Hivyo japo mtoto atahitaji kuishi kwa kuangalia wengine wanafanya nini, akili yake ikishakomaa, anaweza kufanya maamuzi yake mwenyewe, kulingana na maisha anayoyataka.
Lakini jambo kubwa la kushangaza ni kwamba tuna watu wazima wengi ambao bado wanatawaliwa na nguvu hii ya kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, au kile ambacho kinakubalika na wengi, au watu wa karibu.
Kwa sababu sehemu ya akili zetu bado inaishi zama zile, basi wengi wameendelea kuwa watumwa wa matakwa ya watu wengine.
Kushindwa kuishi maisha yako.
Nguvu hii ya kuogopa kukataliwa, kutaka kukubalika imewafanya watu wengi kushindwa kuishi yale maisha ambayo wangependa kuishi. Hii imewafanya watu wengi kuwa watumwa wa tabia, kuwa watumwa wa ndoa, kuwa watumwa wa kazi na hata kuwa watumwa wa jamii kwa ujumla.
Mtu anajua kabisa ya kwamba ni kitu gani anataka kwenye amisha yake, na hata muda mwingi anakifikiria kitu hiko, lakini akitaka kukifanya anaanza kujiuliza, wazazi wangu watanichukuliaje, marafiki zangu watanionaje, jamii itanichukuliaje. Kwa hali hii mtu anaacha kufanya kile ambacho ni muhimu kwake na kuendelea kufanya kile ambacho kinawafurahisha watu wengine wote, kasoro yeye.
Je wewe unaona hii ni sawa? Je unaona ni sawa wewe uwe na maisha magumu na usiyoyapenda ili tu uwaridhishe wengine? Kweli? Umekuja hapa duniani kuridhisha tu wengine?
Nasema haiwezekani, haiwezekani kabisa uwe umekuja hapa duniani kuwaridhisha tu wengine, huku wewe ukikosa furaha ya maisha yako. umekuja hapa duniani na mchango mkubwa sana ambao hutaweza kuutoa kama utaendelea kufanya yale mambo ya kuwafurahisha wengine.
Je upo tayari kuondokana na nguvu hii inayokurudisha nyuma na kuharibu maisha yako? kama ndivyo karibu kwenye sehemu ya pili ya makala yetu ya falsafa mpya ya maisha. Unapoingia kwenye sehemu ya pili, jua kabisa ya kwamba unakwenda kuchukua hatua mara moja, kwa sababu hayo ni maisha yako, na wewe ndio mhusika mkuu.
SEHEMU YA PILI; Jinsi ya kuondokana na nguvu ya kutaka kuwaridhisha wengine.
Mpaka kufika hapa umeshajua kabisa ya kwamba kuna nguvu kubwa sana inayokurudisha nyuma. Na kama umekuwa unayatafakari maisha yako jinsi unavyosoma hapa utakuwa una mifano kabisa ya mambo ambayo umeshindwa kufanya mpaka sasa kutokana na nguvu hii inayokurudisha nyuma. Swali ni je kuna njia yoyote ya kuweza kuishinda nguvu hii? Na jibu lake ni ndio, kama umeamua kwamba unataka kuondokana na nguvu hii, basi inawezekana.
Na hapa unakwenda kujifunza jinsi ya kuondokana na nguvu hii ambayo imeshakuzuia sana wewe kufanya kile ambacho unapenda kwenye maisha yako;
1. Jijue vizuri.
Hatua ya kwanza kabisa ya wewe kushinda nguvu hii ni kujijua vizuri. Inawezekana kutokana na nguvu hii kuwa inakuzuia kwa muda mrefu umeshajisahau kabisa. Hukumbuki tena wewe ni nani, una tofauti gani, ni vitu gani unaweza kufanya kwa ubora na nini ni muhimu zaidi kwako.
Kama umelelewa na wazazi/walezi ambao walikuwa wanakupangia kila kitu, inawezekana ukawa hujawahi kukaa chini na kujijua vizuri wewe mwenyewe.
Hivyo hatua ya kwanza kabisa hapa ni kujijua vizuri. Jijue wewe kama wewe, na sio wewe kama jamii ambavyo inakujua au inataka kukujua.
Jivue vyeo vyote ambavyo jamii imekuvika, weka pembeni hadithi zote ambazo zimezoeleka kuhusu wewe kwenye jamii yako. hata kama una nafasi kubwa popote ulipo, weka pembeni kwa muda na tafakari maisha yako kwa undani.
Jua ni kitu gani muhimu sana kwenye maisha yako. ni jinsi gani maisha yako yangekuwa ungekuwa na furaha sana na ungeona ni mafanikio makubwa. Ni mchango gani unaotaka kutoa kwa wale ambao wanakuzunguka. Je kile unachofanya sasa ndio kinakupa amani ya moyo? Je mahusiano uliyonayo sasa yana mchango wowote kwako kuwa na maisha bora? Je kama ungekuwa na miezi sita tu ya kuishi, ungeendelea na maisha unayoishi sasa au ungetaka kubadili? Je kama fedha isingekuwa tatizo kwako, ungeendelea kufanya unachofanya sasa? Je unataka ukiondoka hapa duniani ukumbukwe kwa lipi?
Kwa kujiuliza na kujipa majibu ya maswali hayo, kunakupa nafasi ya kujijua vizuri. Fanya zoezi hilo ukiwa umetulia na ni vyema ukaandika maswali hayo na kuandika majibu yake kabisa. Hapa utaondoka na kitu kizuri sana unachotaka kwenye maisha yako.
2. Jua hofu ya kukataliwa imejificha wapi.
Baada ya kujijua vizuri, sasa twende kwenye ile nguvu. Jua hofu hasa ya kukataliwa imejificha wapi. Ni maeneo gani ya maisha yako ambayo huwezi kufanya kitu mpaka wengine wawe wamedhibitisha? Ni mambo gani ambayo ukitaka kufanya unaangalia kwanza wengine wanafanyaje au wanachukuliaje? Hili ni eneo muhimu sana kwani ndio chimbuko la hofu kubwa inayozuia maisha yako kusonga mbele.
Hapa pia jua watu ambao wanakurudisha nyuma kwa kutumia nguvu hiyo. Jua ni watu gani ambao huwezi kufanya jambo bila wao kudhibitisha? Ni watu gani ambao ndio kama wamekuwa wanatawala maamuzi yako yote? Je ni wazazi? Ni marafiki? Ni wafanyakazi wenzako? Wajue watu hawa vizuri ili wakati mwingine unapokuwa na wazo kubwa la kufanya, uwaepuke kwanza watu hawa la sivyo wataendelea kukurudisha nyuma.
3. Jua hakuna anayejali sana kuhusu wewe.
Moja ya vitu ambavyo ni vya kushangaza sana kuhusu nguvu hii inayoturudisha nyuma ni kwamba kwa sehemu kubwa ni uongo. Yaani wewe unaweza kuwa na hofu kubwa sana kwamba watu wanakuchukulia vibaya kwa kile ambacho unakifanya, lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayefikiria sana maisha yako kuliko wewe.
Watu wanaweza kukuambia acha kufanya hiko, au fanya hiki, lakini baada ya hapo sio kwamba usiku hawalali wanakufikiria wewe, wanarudi kufikiria mambo yao binafsi. kila mtu ana matatizo yake binafsi na hivyo anatumia muda mwingi kuyafikiri kuliko hata wanavyofikiri kuhusu wewe.
Unaweza kuwa na hofu kwamba watu wanakufuatilia kwa kile unachofanya, wanakuangalia kwa kila hatua unayopiga, lakini huo sio ukweli. Na tena kwenye dunia hii ambayo teknolojia imekua sana, mtu yupo tayari kuangalia simu yake zaidi ya anavyofikiria kuhusu wewe.
Hivyo kwa lolote unalofanya, acha kufikiria dunia nzima imesimama na inakuangalia wewe. Dunia inaendelea kuzunguka na kila mtu anakazana na matatizo yake.
4. Jua huwezi kumridhisha kila mtu.
Ukijua hiki kimoja, leo hii unaanza kuishi maisha yako. kwa sababu katika kutafuta kuwaridhisha wengine, unaacha kuishi yale maisha ambayo ni muhimu kwako na kufanya kile ambacho wengine watafurahia. Lakini hebu niambie ni wote wanaridhika na kile unachofanya? Jibu ni hapana. Katika chochote utakachofanya, kuna watu wataona unakosea au ungeweza kufanya kwa ubora zaidi.
Hivyo badala ya kukazana kumridhisha kila mtu, halafu ukashindwa mara mbili, yaani unashindwa kuwaridhisha wote na unashindwa kujiridhisha wewe mwenyewe, hebu anza na kujiridhisha wewe mwenyewe. Utakapofanya kile ambacho kinakuridhisha, utawavutia wale wanaoendana na kile unachofanya, na maisha yako yatakuwa bora na yenye furaha.
5. Unawavutia wale wanaoendana na wewe.
Kama tulivyoona hapo juu, ukifanya kile ambacho kinakuridhisha wewe, utawavutia wale wanaoendana na wewe. Hivyo usifikiri ukianza kuishi maisha ya kukuridhisha wewe utatengwa na kila mtu. Bali utapata wengi ambao wanapenda maisha ya aina hiyo na mahusiano haya yatakuwa bora sana kuliko hayo ya mwanzo ya kutaka kuridhisha wengine. Unapokuwa kwenye hali ya kuheshimiana kwa kile unachofanya, ni bora sana kuliko kuwa kwenye hali ya kutaka kumridhisha mwingine huku wewe ukiendelea kuwa hovyo.
Na kwa upande mwingine watu hao ambao wanakuvuta nyuma umewavutia wewe mwenyewe kwenye maisha yako kwa kuendelea kuishi vile ambavyo wanataka wao. Ukianza kuwa na maisha bora kwako, watalazimika kubadilika na kukuheshimu au watalazimika kuondoka kwenye maisha yako.
Vipi kama anayenirudisha nyuma ni mzazi? Naye ni hivyo hivyo, kuendelea kufanya kile anachotaka yeye, hakifanyi maisha yako na hata yake kuwa bora. Lakini utakapoanza kufanya kile ambacho ni bora kwako na ukawa na masiha yenye furaha na mafanikio, hatakuwa na namna nyingine bali kufurahi sana. Kwa sababu yeye anakurudisha nyuma sasa akiamini anakujengea maisha bora, kumbe haelewi maisha bora ni yale unayojenga mwenyewe, anza kuyajenga na mtaheshimiana.
6. Mwisho wa siku wote tutakufa.
Unajua nini kitatokea miaka 100 ijayo? Wote tunaosoma hapa tutakuwa tumekufa. Hivyo kama ukiamua kuishi maisha yako kuna watu watachukia sana, kumbuka hawatakuchukia milele, wote mtakufa na kila kitu kinakwisha. Kama mtaenda kukutana baada ya kufa, sina hakika kama mtaendeleza yale mliyoanzisha hapa.
Hivyo kama unaona kuna watu hawatafurahia maamuzi yako ya maisha, kuwa na uhakika na kitu kimoja, muda tunaokaa hapa duniani ni mdogo sana ukilinganisha na muda uliopita na hata utakaokuja. Hivyo ni bora kutumia muda huu mfupi sana kuishi yale maisha ambayo ni bora sana kwako. Maana hayatadumu milele.
7. Amua kuwa wewe.
Mwisho kabisa amua kuwa wewe. Ndio fanya maamuzi hapa ya kwamba unakwenda kuwa wewe. Amua kuachana na maisha ya maigizo, kufanya kitu ili kuwaridhisha wengine huku wewe roho yako ikiwa haipo kabisa.
Umeshajijua vizuri, umeshajua ni kitu gani unataka na maisha yako, umeshajua ya kwamba huwezi kumridhisha kila mtu na una uhakika kwamba wote tutakufa, sasa kilichobaki ni wewe kuishi maisha yako. kuishi yale maisha ambayo yana maana kwako. Kuishi yale maisha ambayo yatakupa amani ya moyo, hata kama wengine wanaona siyo bora.
Na kama utaweza kuwa wewe, kama utaweza kuishi maisha ambayo yana maana kwako, kila mtu atakuheshimu na utakuwa na maisha bora sana.
Je upo tayari?
Kumbuka maisha ni yako na maamuzi ni yako. pia kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama wewe hutafanya kazi. Nikutakie kila la kheri katika kutekeleza msingi huu muhimu wa falsafa mpya ya maisha leo hii. unasoma hapa, unanijua mimi kwa sababu nilichagua kuishi maisha ambayo ni bora kwangu. kama ningefuata vile jamii ilitaka jifanye, vile ambavyo wazazi walitaka niishi, leo hii usingenijua. Je kama nisingechagua kuishi maisha ambayo yana maana kwangu, hakuna kitu wewe ungekosa? Kama jibu ni ndio kuna kitu ungekosa kutoka kwangu, jua kuna kitu watu wanakosa kutoka kwako, hebu chukua hatua leo.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,