Habari za wakati huu mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA? Naamini uko vizuri sana na unaendelea kufanyia kazi yale mengi unayojifunza kupitia mtandao huu na pia kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Hata kama huoni majibu ya haraka usikate tamaa, endelea kuweka juhudi na lazima utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Karibu tena kwenye kipengele hiki kizuri cha ushauri wa changamoto  ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio ambayo tunayataka kwenye maisha yetu. Wote tunajua kwamba maisha sio rahisi, maisha yana changamoto zake na ni changamoto hizi ndio zinafanya maisha yawe bora zaidi.
Hebu fikiri maisha ambayo hayana changamoto! Unaamka, unakula, unalala. Kesho yake tena unarudia hivyo. Je ungeona kuna jambo kubwa kwenye maisha? Jibu ni hapana. Hivyo changamoto ni muhimu sana kwetu, na badala ya kuzikimbia basi tuzikabili ili maisha yetu yaendelee kuwa bora.
Kwa sababu hii kubwa ndio maana mtandao huu wa AMKA MTANZANIA umekuwekea kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Hivyo unapokuwa na changamoto yoyote usisite kutuandikia na sisi tutakuletea ushauri mzuri unaoweza kuufanyia kazi. Kujua jinsi ya kutuandikia angalia mwisho wa makala.

 
Leo katika kipengele hiki tutaangalia ni jambo lipi muhimu kufanya kwanza, kati ya kuendelea na masomo, kuoa au kujenga. Hii imetokana na msomaji mwenzetu aliyetuandikia ili kutaka ushauri. Karibu sana tujifunze.
Kabla hatujaingia kwenye ushauri tupate maoni ambayo msomaji mwenzetu alituandikia;

Nina mambo matatu nashindwa lipi lianze kusoma masters, kuoa na kujenga nyumba.
J. S

Kama tulivyosoma hapo juu, msomaji mwenzetu ana mambo matatu yanayomtatiza ni lipi aanze nalo, kati ya kuendelea na masomo yake, kuoa au kujenga nyumba.
Karibu sana tushauriane kwa pamoja.
Habari ndugu J. S,
Karibu sana na pole kwa changamoto ambazo unapitia. Kabla hatujaingia kwenye nini ufanye napenda uchukue muda na kutafakari, je tangu mwanzo malengo yako yalikuwa ni nini? Tangu upo shuleni, ulipokuwa unaanza shahada ya kwanza na sasa unataka kwenda kusoma shahada nyingine, ni nini yalikuwa malengo yako?
Je malengo hayo uliyaandika chini, na ukayapa muda wa kuyafikia? Mambo haya ni muhimu sana kutafakari kwa sababu kama ungekuwa na malengo ambayo umeyaandika vizuri, leo hii usingekuwa kwenye hii hali ya kutokujua kipi cha kufanya. Leo ungekuwa unafanya kulingana na malengo uliyojiwekea.
Hivyo basi, kabla hata hujaendelea, andika kwanza malengo yako, andika malengo ya muda mfupi na malengo ya muda mrefu. Muda mfupi ikiwa ni ndani ya mwaka mmoja, na muda mrefu miaka mitano, kumi na hata ishirini ijayo. Fikiria picha ya maisha unayoyataka na andika.
Na malengo usiweke ya fedha au kazi tu, weka malengo kwenye maeneo haya matano muhimu sana kwenye maisha yako; MALENGO BINAFSI, MALENGO YA KIFEDHA, MALENGO YA KAZI, MALENGO YA FAMILIA NA JAMII NA MALENGO YA KIAFYA. Kwa kufanya hivi utakuwa na njia ya uhakika ya kufuata kila wakati kwenye maisha yako.
Kujifunza zaidi kuhusu kuweka malengo bonyeza hapa na utafungua makala za malengo.
Karibu sasa tuanze kuchambua mambo haya matatu yanayokutatiza.
1. Kuoa.
Kwanza tuanze na kuoa ambapo panaweza kuwa muhimu zaidi ya huko kwingine. Kuoa sio jambo la kufanya kwa sababu wakati umefika wa kufanya hivyo, labda kiumri au kwamba umeshajiridhisha kimapato au kielimu. Kuoa ni jambo linalotegemea vitu vikubwa viwili;
Cha kwanza ni utayari wako wewe mwenyewe. Je upo tayari kuoa? Upo tayari kuachana na maisha ya kuwa mwenyewe, kufanya maamuzi yako kwa kujifikiria mwenyewe na sasa uanze kufanya maamuzi ukifikiria zaidi? Je upo tayari kuachana na mambo yote ambayo hayaendani na maisha ya ndoa? Kama ndivyo basi unaweza kuingia kwenye ndoa.
Kitu cha pili ni kupata mtu unayeweza kwenda naye. Kuwa tayari kuoa haimaanishi yeyote utakayemwoa mtakwenda vizuri. Ndio maana ni muhimu sana kujua ni mtu wa aina gani unaweza kwenda naye, kumtafuta na hatimaye kuoana naye. Ukiingia kwenye ndoa kwa sababu tu upo tayari na hukumjua vizuri mwenzako inaweza kuwa changamoto kubwa kwako. Ukiingia kwenye ndoa kwa sababu unaamini mwenzako atabadilika ni sawa na kuchukua mtoto wa chui na kumweka na watoto wa mbwa ukifikiri akikua atakuwa mbwa.
Hivyo kama vigezo hivyo viwili umevifikia, upo tayari kuingia kwenye ndoa na umeshampata ambaye mnaweza kwenda pamoja, basi oa.
Jambo jingine muhimu la wewe kuzingatia ni kamba kuoa hakuzuii mambo yako mengine kwenda. Yaani kuoa hakukuzuii wewe kusoma masters na wala kuoa hakukuzuii wewe kujenga. Tena kuoa kunaweza kukupa wewe faida zaidi kuliko kutokufanya hivyo.
Kama una yale mawazo ya kizamani kwamba inabidi ukamilishe kila kitu ndio uoe, unaweza kujikuta unashindwa kukamilisha na unashindwa kuoa pia. Oa kama upo tayari, mengine yatakwenda vizuri. Huwezi kushindwa kusoma kwa sababu umeoa.
Na kama kinachokufanya ufikiri mara mbili kwenye kuoa ni gharama za sherehe kubwa ya harusi, oa bila ya kufanya sherehe kubwa. Andikisha ndoa na funga huku ukiandaa tafrija fupi ya watu wa karibu kwenu na maisha yanaendelea.
2. Kuendelea na masomo.
Kwanza kabisa hongera kwa kuwa na wazo hili la kuendelea na masomo kwa ngazi ya shahada ya uzamili(masters degree). Ni hatua kubwa kwenye maisha yako. Na kama umepata nafasi ya kusoma shahada hii na una uwezo wa kusoma basi ni vizuri sana ukasoma. Maana elimu ni muhimu sana, na uwekezaji pekee unaolipa zaidi na zaidi ni elimu.
Lakini kabla hujaamua kwamba unakwenda kusoma, naomba utafakari kwa kina kwa nini unataka kwenda kusoma. Je unataka kwenda kusoma ili upate ujuzi na maarifa zaidi ambayo yatakufanya uwe bora zaidi katika kile unachofanya? Kama ndio hongera sana na nenda kasome.
Ila kama unataka kwenda kusoma ili urudi na cheti ambacho utakitumia kudai kipato kikubwa zaidi, unaenda kupoteza muda wako na ni bora usifanye hivyo kabisa. Kwa sababu utaangushwa, yaani utakuwa disappointed.
Na kama tulivyoona hapo juu, unaweza kuendelea na masomo huku ukiwa umeoa. Tena haya masomo ya juu kwa ngazi za shahada na shahada nyingine za juu, ni ratiba zako ndio zitakuongoza. Hivyo kama upo tayari kusoma na nafasi ipo soma, hata kama umeoa au una familia. Tena hii itakujengea nidhamu kubwa zaidi.
SOMA; USHAURI; Kipi Bora, Kujenga Au Kuwekeza Kwenye Biashara? Soma Hapa Kujua.
3. Kujenga.
Hapa kwenye kujenga unahitaji kutafakari kwa kina kidogo. Maana kunaweza kuwa na changamoto kubwa kuliko huko kwingine.
Jambo la msingi, unajenga wapi, na unajenga kwa kiasi gani na gharama za ujenzi unazilipaje.
Kama unajenga sehemu ya karibu, ambapo unaweza kuishi na kuendelea na shughuli zako mara baada ya ujenzi, na unaweza kugharamia gharama zote za ujenzi kwa muda mfupi basi jenga.
Ila kama unajenga mbali na maeneo unayofanyia shughuli zako, na unajenga kwa kudunduliza, leo upate mifuko 20 ya sementi, kesho tofali 500, keshokutwa nondo 30, acha kwa sasa, itakuumiza kichwa sana.
Ni bora hiyo fedha ambayo ungeenda kuidunduliza kwenye ujenzi ukaifanyia mambo mengine ya uzalishaji na mahali pa miaka miwili mpaka mitano utakuwa na kiasi kikubwa cha kukutosha kujenga bila ya kuumia mawazo. Kama ujenzi utakuchukua zaidi ya mwaka mmoja kukamilisha gharama zote, utakurudisha nyuma, achana nao.
Tafakari kwa kina haya tuliyojadili hapa, na amua mara moja ni yapi unafanyia kazi na kisha chukua hatua. Huenda kuna wengine hamkuuliza swali hili lakini mmekuwa kwenye hali za aina hii, basi fanyia kazi yale ambayo yanaendana na hali yako. na kama una changamoto nyingine tuandikie kwa kufuata maelekezo hapo chini. Na kama unahitaji ushauri wa moja kwa moja kwa mazungumzo tuwasiliane kwa 0717396253. Karibu sana.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.