Pamoja na kuishi kwenye dunia yenye uhuru mkubwa, bado watu wengi wanaishi maisha ya kiutumwa.

Watu wengi wanaishi maisha ambayo hawana uhuru wa kuamua wafanye nini na maisha yao.

Jambo lolote ambalo ni muhimu kwao kufanya, hawawezi kulifanya mpaka mtu au watu ambao amechagua kuwa mtumwa kwao walidhibitishe. Kama wakiona linafaa watamruhusu kufanya, na kama wataona halifai basi watamkataza kufanya.

Utumwa huu ni mbaya kuliko hata ule utumwa wa kulazimishwa na kupigwa. Kwa sababu utumwa huu mtu anachagua mwenyewe na mara nyingi haelewi kama yupo utumwani. Vile vile adhabu anayopewa kwenye utumwa huu kama akienda kinyume na wanavyotaka wengine ni adhabu ya kiasaikolojia, lakini ni kali sana.

Je wewe umechagua kuwa mtumwa wa nani?

Ni mtu au watu gani ambao kabla hujafanya jambo ni lazima uwaambie, na ukiwaambia chochote wanachosema wao ndio unafanya?

Ni mtu au watu gani ambao unapenda kila unachofanya wakifurahie, unaogopa ukifanya tofauti watakutenga?

Mtu au watu hawa ndio umeamua kuwa watumwa kwao. Wanaweza kuwa wazazi, wanaweza kuwa ndugu, jamaa na marafiki, pia inaweza kuwa jamii nzima.

Ukishajua wale ambao umeamua kuwa watumwa kwao unafanya nini? Unajiondoa kwenye utumwa huo. Na je unawezaje kujiondoa kwenye utumwa huo? Njia zote ziko hapa, fungua na usome makala hii; Nguvu Kubwa Inayokurudisha Nyuma Na Jinsi Ya Kuishinda.

TAMKO LANGU;

Leo nimejua ya kwamba nilikuwa nimechagua kuwa mtumwa wa…………..(jaza wale ambao umekuwa watumwa kwao). Na kuanzia leo nimeamua kuvunja kabisa utumwa huu, nitayaheshimu maisha yangu na kufanya yale ambayo ni muhimu kwangu. Najua kwa njia hii tutaheshimiana zaidi.

NENO LA LEO.

“Disobedience is the true foundation of liberty. The obedient must be slaves.”
― Henry David Thoreau

Uasi ndio msingi wa kweli wa uhuru. Utii ni msingi wa utumwa.

Unapotaka kufanya kile ambacho kinawapendeza watu lakini sio muhimu kwako, umechagua kuwa mtumwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.