Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotukwamisha kufika kwenye maisha ambayo tunayataka. Kila mmoja wetu kuna changamoto ambazo anakumbana nazo, na kama umeweka hisia zako kwenye changamoto hizo, inakuwa vigumu sana kupata suluhisho.

Jukumu langu hapa ni kukuwezesha kuiangalia changamoto yoyote unayokutana nayo kwa jicho la tofauti na kisha suluhisho linajitokeza lenyewe. Tunashauriana hatua bora kabisa za kuchukua ili kuvuka changamoto unayokutana nayo na uweze kufanikiwa.

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kuangalia jinsi ya kufanya maamuzi ya uanze kipi kati ya biashara au kuoa. Kabla hatujaingia ndani na kujua unafikiaje maamuzi sahihi, msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili alituandikia yafuatayo;

Mimi nina malengo ya kufungua duka mwakani kwa ajili ya kukuza kipato, changu ila kuna mchumba anataka nimuoe je nianze na lipi kati ya kuoa au kukuza kipato mimi ni mwajiriwa. – PASCHAL B. M.

Kama alivyotuandikia mwenzetu Pascal, yupo njia panda kati ya kuanza biashara ambayo itamwezesha kukuza kipato chake na kumuoa mchumba wake. Yote haya ni mambo muhimu kwenye maisha ya mtu yeyote yule. Hivyo bila ya kuwa na msingi sahihi wa kufanya maamuzi, ni vigumu kujua uanze na kipi.

Swali kuu ni je uanze biashara au uoe?

Kwenye mambo mengi ambayo nimekuwa nashauri, mtu anapokuwa njia panda, huwa nasema fanya vyote.

Mfano je niache ajira na kuanza biashara au niendelee na ajira na nisianze biashara? Huwa nasema fanya vyote, endelea na ajira na anzisha biashara yako kwa pembeni.

Hata kwenye masomo na biashara, wapo wanaouliza iwapo waache masomo na kujikita kwenye biashara, huwa nashauri mtu afanye vyote.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Kwa nilichojifunza, sisi binadamu tunao uwezo mkubwa mno, na kadiri mazingira yanavyotutaka tufanye zaidi ndivyo tunavyofanya zaidi. Kwa mfano kama una ajira pekee na huna biashara, utajikuta una vitu vingi vya kupoteza muda. Utajikuta kila jioni una muda wa kukaa na wengine na kubishana. Utajikuta unapata nafasi ya kufuatilia kila habari na kila michezo. Lakini utakapoanza biashara ukiwa bado upo kwenye ajira, vitu hivyo vinapungua vyenyewe.

Hivyo jibu la kwanza, pale unapokuwa njia panda kwa vitu viwili muhimu sana, ni kufanya vyote. Unachagua kufanya vyote, na unajiweka kwenye nafasi ya kuusukuma mwili wako kuliko ulivyozoea.

Lakini inapokuja kwenye swala la kuoa au kuolewa, ushauri wangu wa fanya vyote unasimama kidogo. Pale unapokuwa njia panda kati ya kuoa/kuolewa na kufanya kitu kingine muhimu, sikuambii fanya vyote.

SOMA; USHAURI; Kuendelea Na Masomo, Kuoa Au Kujenga, Kipi Bora Kufanya Kwanza?

Swali la kwanza ninalokuuliza ni je upo tayari? Kuoa au kuolewa siyo swala la umri au wakati, bali ni swala la utayari. Je upo tayari kuendesha maisha yako na mtu mwingine? Upo tayari kuacha kufanya vitu vingi ambavyo umekuwa unafanya kabla ya kuoa au kuolewa na kuanza kufanya viti vinavyokuja na kuoa au kuolewa?

Je upo tayari kuishi na mtu mwingine ambaye atakuja na mapungufu yake, na utahitaji kuyavumilia ili maisha yaweze kwenda?

Jibu ni kama haupo tayari basi usikimbilie kuoa au kuolewa kama vile ni maonesho. Kwa sababu mtaishia kusumbuana na mwishowe utasema ulilazimishwa na hukuwa tayari.

Kama sasa upo tayari, umetafakari na ukaona umeshakuwa tayari na upo tayari kujitoa kwa maisha ya ndoa, basi fanya vyote. Oa na anza biashara yako. Kwa sababu unao uwezo wa kufanya vyote kwa pamoja.

Muhimu ni usipoteze fedha zako nyingi kwenye kufanya sherehe wakati unaoa, maana ukifanya hivyo, utashindwa kuanza biashara yako na mwishowe utasingizia kwamba kuoa kumekuzuia wewe kuanza biashara.

Na kama huwezi kuoa bila ya kufanya sherehe kubwa, basi kuoa inabidi kusubiri kwanza uanze biashara na uanze kutengeneza kipato, au biashara isubiri kwanza uone kisha ujipange kuanza.

Chochote unachoamua, hakikisha unachukua hatua na mwishoni usije kujiambia ningefanya hivi ingekuwa vile. Fanya maamuzi na yasimamie, kwa sababu maamuzi yoyote utakayofanyia kazi yatakusogeza mbele zaidi kuliko ukibaki njia panda.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog