Mafanikio ya biashara yoyote ile yanaanza na mafanikio ya mfanyabiashara mwenyewe. Biashara itakuwa kwa kiasi kile ambacho mmiliki wake amekua, na haiwezi kwenda zaidi. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kukuza biashara zao kwa sababu wao wenyewe hawakui. Na hili limekuwa tatizo kubwa la biashara nyingi kushindwa au hata kudumaa kabisa.
Unakuta biashara imeanzishwa na inafanyika ila miaka nenda miaka rudi ipo pale pale. Kama ni duka basi ni duka lili lile moja, kama ni huduma basi huduma inatolewa vile vile miaka yote. Hakuna mabadiliko makubwa na wala hakuna ukuaji. Na vibaya zaidi mfanyabiashara anakuwa amesharidhika. Inapokuja kutokea changamoto ambayo ni tofauti na vile alivyozoea, ndipo matatizo yanapokuwa makubwa na kupelekea biashara kufa kabisa.
Leo katika makala hii ya kona ya mjasiriamali nataka ujiulize swali moja muhimu sana. Je wewe unajenga biashara au unafanya biashara? Swali hili ni muhimu sana kwa sababu jibu utakalotoa ambalo ni kile unachofanya litakuambia kama utafanikiwa kupitia biashara hiyo au utaendelea kufanya tu kawaida. Najua hujawahi kujiuliza swali hili, na huenda hukuwahi kufikiria kuna tofauti kati ya kujenga biashara na kufanya biashara. Leo utayajua vizuri hayo mawili.
Kufanya biashara.
Kuna wafanyabiashara wengi ambao wapo kwenye biashara kwa lengo tu la kufanya biashara. Wafanyabiashara hawa wao huangalia kitu kimoja tu, ni faida kiasi gani wanaopata. Chochote wanachofanya kwenye biashara zao ni kuangalia faida tu. Wapo tayari kufanya chochote kile kuhakikisha wanapata faida.
Kwa wafanyabiashara wa aina hii, hawajali sana kuhusu wateja wanaowahudumia. Kama wanapata faida wanafanya biashara, kama hawapati faida hawafanyi. Na hata ikitokea mteja hawezi kunufaika na kile wanachomuuzia, wao hawajali hilo, kikubwa kwao ni faida, na wanachotaka ni kuipata, kwa njia yoyote ile.
Kwa kujali faida tu, wafanyabiashara hawa wamekuwa wanashindwa kuyaona matatizo hasa ya wateja wao na hivyo kukosa fursa kubwa zaidi ya kuwahudumia. Na hata ile huduma wanayotoa kwa wateja wao inakuwa sio nzuri na hivyo hii huwafanya wateja kutokuvutiwa kurudi tena kwenye biashara zao. Hii ndio maana halisi ya wao kufanya biashara, ni kama pata potea.
Wafanyabiashara hawa, wanapomhudumia mteja, na ikatokea baadae mteja amepata changamoto kutokana na kile walichomhudumia, wao hawahusiki, wakishauza basi imetoka, kama mteja atapata tatizo atajijua mwenyewe.
Mteja hawezi kujisikia vizuri kuendelea kufanya biashara na wafanyabiashara wa aina hii. Ndio maana wafanyabiashara hawa hupata wateja mara moja tu na hawarudi tena. Vibaya zaidi wafanyabiashara hawa wanaweza kutumia nguvu nyingi kuwavutia wateja wapya lakini wateja wanapofika pale, hawarudi tena wakati mwingine.
Kujenga biashara.
Kujenga biashara ni pale ambapo mfanyabiashara anapofanya biashara yake akijua ya kwamba kuna kesho pia. Mfanyabiashara wa aina hii anamjali sana mteja wake na anajua huduma bora sana kwa mteja leo ndio zitamvutia kurudi tena kesho. Wafanyabiashara hawa wanaangalia zaidi ya faida. Ndio wapo kwenye biashara ili kupata faida, ila hawaruhusu faida kuwazuia kutoa huduma bora zaidi.
Wale wanaojenga biashara, wanakuwa na uhusiano mzuri sana na wateja wao. Wanakuwa hawawauzii tu wateja, bali pia wanawashauri kipi ni bora kwao. Wafanyabiashara hawa wanayajua vizuri matatizo ya wateja wao na wanawapatia suluhisho la matatizo yao. Kwa njia hii wateja wanaichukulia biashara sio kama sehemu ya kwenda kutoa fedha, bali sehemu ya kwenda kupata suluhisho la matatizo yao.
Wanaojenga biashara wanajua kabisa ya kwamba mteja bora kabisa wa biashara ni yule waliyenaye sasa. Na wanajua kwa kuwapatia huduma bora, wateja hawa wataleta wateja wengi zaidi kupitia sifa nzuri watakazokuwa wanatoa kuhusu biashara zao.
Pale mteja anapopata tatizo kwa bidhaa au huduma aliyopewa, wajengabiashara wanakuwa tayari kumsaidia mteja ili aweze kunufaika vizuri. Wako tayari kufanya hivi hata kwa gharama zao binafsi kwa sababu wanajua kujenga biashara ni muhimu kuliko faida ya mara moja tu.
Kwa njia hizi biashara inajengwa na hata kama imeanzia chini kiasi gani, ni lazima itakua kadiri siku zinavyozidi kwenda.
Baada ya kupitia maelezo hayo ya kufanya biashara na kujenga biashara, wewe umejikuta kwenye kundi gani kwa sasa? Unajenga au unafanya?
Na je baada ya kujua upo kundi lipi, je unaona ni kundi lipi sahihi kwako kuwepo? Kufanya au kujenga.?
Kama unataka biashara ambayo ni ya kawaida na itakayokupatia faida kiasi bila ya kukua, basi unaweza kuendelea kufanya biashara. Kama unataka biashara ambayo itakuwa inakua kila siku na kukuletea faida kubwa baadae basi anza kujenga biashara. Anza kuwajali zaidi wateja, anza kutoa huduma bora na hayo ya faida wala hayatakuwa tatizo kwako.
Wafanya biashara ni wengi sana, ndio maana kuna biashara nyingi za kawaida. Wajenga biashara ni wachache sana ndio maana kuna biashara chache sana zenye mafanikio makubwa. Kuwa mjenga biashara na biashara yako itasimama zaidi ya hapo ilipo sasa.
Nakutakia kila la kheri katika ujengaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,