Kuna wakati katika maisha yetu ya kila siku huwa tunajikuta katika wakati mgumu sana, hasa kutokana na kile tunachokifanya kinakuwa hakileti yale matokeo tunayoyataka. Hii ni hali ambayo karibu kila mtu ameshawahi kukutana nayo kwa namna moja au nyingine. Wengi wanao kabiliana na hali hii hujikuta wakiwa njia panda wakiwa hawajui ni nini cha kufanya.
Kiuhalisia hapa ndipo ambapo umakini na uvumilvu wa hali ya juu sana huwa unahitajika ili kuweza kufanikiwa. Uvumilivu na umakini huu ninao uongelea ni lazima uhitajike kwa sababu mambo yanakuwa yanakwenda hovyo. Pasipo umakini na uvumilivu huu wengi huishia kukata tamaa na kuamua kuachana na kila kitu.
Swali la kujiuliza hapa je, hawa wanaoamua na kuachana na hicho wanachokifanya kwa sababu ya magumu au kushindwa na changamoto ni kweli huwa wapo sahihi? Je huo ndio ulikuwa wakati wao wa kuachana na kile wanachokifanya? Mara nyingi wengi huwa wanaachana kile wanachokifanya kwa wakati sio sahihi kwao.
Inawezekana hujanielewa vizuri, ngoja nikwambie kitu kimoja. Upo wakati wa kuacha kile unachokifanya na sio kila tu wakati unaweza ukaacha. Kama utakuwa mtu wa kufanya jambo hilo na kuacha bila kujua wakati wako kama ni sahihi au sio sahihi, na kuhakikishia utaacha mambo mengi sana na hutaweza kufanikwa kwa lolote.
Kitu kikubwa hapa ni kuelewa siri hii, itakayokusaidia wewe kutambua wakati wako sahihi wa kuacha kile unachokifanya kama hakikupi mafanikio makubwa. Maana yake nini hapa? Ni kweli kama kitu hicho hakikuletei mafanikio na ukaendelea kuking’ang’ania sana kwanza kitakupotezea muda wako na pili, hutafanikiwa kabisa.

Sasa je, ni muda upi wa wewe kuacha kile unachokifanya? Ipo sheria ya kukongoza kuaacha jambo hilo unalolifanya kama halikuletei matokeo unayoyata. Nafikiri mpaka hapo tupo pamoja ila najua una shauku ya kutaka kujua ni wakati gani ambapo unatakiwa kuacha lile jambo ambalo halikupi matokeo unayoyataka au faida?
Kama kweli jambo unalolifanya umeona halikunufaishi, halikupi faida kama unavyotaka, unaruhusiwa kuliacha pale ambapo ikiwa kila unapolifanya huoni akilini mwako kuwa kama kweli utafanikiwa. Hapa naamanisha yaani huna uhakika kabisa na huoni hata tumani la kufanikiwa. Kama upo katika wakati huo hicho ni kipindi cha kuacha jambo hilo mara moja.
Kumbuka sisi ni matokeo ya kile tunachokifikiria. Sasa kama kweli picha inayokujia kichwani mwako ndio hiyo ya kukosa tumaini, haina haja ya kuendelea tena na jambo hilo kwa sababu tayari umeshashindwa. Hata ikatokea uweke juhudi vipi kiuhalisia huwezi kufanikiwa, pengine labda utoe picha au fikra hizo kichwani kwanza.
Pia wakati mwingine wa kuacha jambo unalolifanya ni pale inapofikia mahali ambapo unakuwa umevunjwa moyo kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba unakosa ile hamasa kubwa ya kusonga mbele. Inapofika wakti huu kwako ni wakati sahihi wa kuacha kile unachokifanya. Sasa utawezaje kuendelea mbele kama huna hamasa wala moyo wa kukuendelea mbele? Kwa hali hiyo, dawa pekee ni kuacha tu.
Kuachana na jambo hilo hata hivyo kumbuka si maanishi kuacha moja kwa moja hapana. Inapokutokea hivyo ukawa umeacha, kitu kikubwa kwako ni kujipanga na kuanza upya tena mpaka kufanikiwa. Unapokuja kuanza tena unakuwa una nguvu kubwa ya kukufanikisha kufikia mafanikio yako makubwa.
Kwa hiyo kwa vyovyote vile kabla hujaacha jambo lolote, acha kuacha kienyeji hata siku moja. Uwe na tabia ya kujiuliza mara kwa mara kwamba je, huu ni wakati sahihi kwangu wa kuacha jambo hilo? Au ninataka kukurupuka? Kwa maswali kama hayo yatakusaidia sana kujua wakati wako ni upi wa kuacha jambo hilo.
Kwa makala nyingine nzuri kumbuka kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,