Hakuna ubishi kwamba ili uweze kufikia mafanikio makubwa sana ni lazima uweze kufanya kazi zaidi ya kawaida. Ni lazima uweze kujitoa zaidi, kufanya kazi kubwa na kuwa tayari kwenda hatua ya ziada hata kama wengine hawawezi kufanya hivyo. Kama bado unakataa hili, kama bado hujalichukua hili kwenye nafsi yako, ninachoweza kukuambia ni kwamba hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kwa sababu kufanya kazi kawaida, ni sawa sawa na kufanya kazi hovyo. Na kwa dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa, kila unachofanya kuna wengi wanaweza kufanya, ukiwa kawaida unajipoteza mwenyewe. Hivyo wewe kama mtu wa mafanikio ya WORLD CLASS, mafanikio ya juu kabisa ambayo hayawezi kulinganishwa na kitu kingine, ni lazima uwe tayari kufanya kazi sana.

Ubinadamu ni changamoto.

Pamoja na kujua ya kwamba unahitaji kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana ili ufanikiwe, bado ubinadamu unakuwa changamoto hapo. Kuna wakati unataka kabisa kufanya kazi lakini mwili unakuwa umechoka, yaani huwezi kabisa kufanya chochote. Unajaribu kujisukuma lakini wapi. Katika hali kama hii unashindwa kutekeleza yale uliyopanga na hivyo kushindwa kufikia mafanikio uliyotarajia.

Moyo u radhi lakini mwili ni dhaifu, huenda umewahi kutumia kauli hii na unaielewa sana. Pale ambapo unajua kabisa ni nini unataka kufanya na unajua kabisa ni muhimu kufanya, lakini huwezi kufanya.

Sasa leo tutakwenda kujifunza mbinu za kisaikolojia zitakazokuwezesha wewe kuondokana na hali hii na hivyo kuweza kufanya kazi kwa juhudi bila ya licha ya kuwa na hali ya kuchoka.

Umewahi kushangaa inawezekanaje wengine hawawezi kuchoka, yaani wanaonekana wanaendelea kuweka juhudi wakati wewe umechoka kabisa? Na ukiangalia wote mnafanya kitu kimoja? Basi leo utajua ni nini kinaweza kuwasukuma wao zaidi.

Nikushirikishe mfano mmoja kabla hatujaendelea, wakati nasoma kidato cha sita, tulikuwa tunakaa chumba kimoja wanafunzi watatu, sasa mmoja wa wanafunzi tuliokuwa tunakaa naye tulikuwa tunaweza kumaliza wiki hatujakutana pamoja chumbani. Mimi nilikuwa napenda kusoma zaidi mchana, yeye alikuwa anasoma zaidi usiku. Sasa cha kushangaza muda wa kupumzika mchana alikuwa hanioni chumbani. Hivyo akawa ananiita TURBO INTERCOOLER, yaani sawa na gari yenye nguvu na ambayo inaweza kujipooza yenyewe. Alikuwa anashangaa nawezaje kwenda muda mrefu nikisoma bila ya kupumzika. Alikuwa hajazijua mbinu za kisaikolojia nitakazokwenda kukushirikisha leo.

Akili yako haina akili kukushinda wewe.

Wote tunajua kwamba tunatumia akili zetu kufanya mambo yote ambayo ni muhimu kwetu. Lakini sisi ndio tunaziongoza akili zetu. Hivyo akili yako haina akili kukuzidi wewe, lakini wengi hawajui hili ndio maana wanakubali kuongozwa na akili zao.

Akili yako haipendi kuumia, akili yako haipendi kuteseka hivyo ikiona dalili zozote za kuumia au kuteseka inatuma taarifa haraka kwenye mwili wako… ‘umechoka sasa, pumzika’ na wewe unasema nimechoka na unapumzika.

Sasa akili yako ikishazoea kwamba ikituma tu taarifa wewe unachukua hatua, basi kila unapofikia uchovu hata kama ni kidogo tu, inatuma taarifa na wewe unaipokea na kuifanyia kazi. Ndio maana ya usemi MOYO U RADHI LAKINI MWILI NI DHAIFU, yaani wewe upo tayari kufanya, lakini akili yako inauambia mwili sasa hivi umechoka, usikubali kufanya, basi na mwili nao unakugomea.

Hapa ndipo mahali pazuri sana pa kutumia mbinu za kisaikolojia, ampapo wewe unaipelekea akili yako taarifa za uongo na akili yako inapeleka taarifa za kufanya kazi kwenye mwili;

MUHIMU; Kama mambo haya matatu yanakuchanganya, wewe(spirit), akili(mind) na mwili(body), weka maoni hapo chini na nitaandaa makala ya kuelezea utofauti wa vitu hivi vitatu.

Tuendelee, kwa hiyo sasa, wewe unaweza kuidanganya akili yako na akili ikaudanganya mwili na mwili ukafanya kazi kwa juhudi sana.

Unawezaje kufanya hivyo?

Hapa sasa ndio inapokuja nafasi ya mbinu za kisaikolojia. Na nitakushirikisha mbinu hizi pamoja na mifano halisi ya nyakati unazotumia mbinu hizi bila ya wewe kujua.

Mbinu ya kwanza; taka kitu kwa hamu kubwa sana.

Kama kuna kitu unakitaka kwa hamu na shauku kubwa sana, basi unaweza kutuma taarifa za uongo kwenye akili yako na ikaendelea kufanya kazi hata kama ulikuwa unajiona umechoka.

Kwa mfano kila mmoja wetu amewahi kufanya kitu ambacho alikuwa anafikiria hawezi kufanya. Fikiria kama umewahi kukimbizwa na mbwa, ni nini kilitokea? Huenda uliruka ukuta ambao hujawahi kujaribu kuuruka na hata baadae hukuweza kuuruka tena. Hapa uliweza kuisukuma akili ichukue hatua mara moja bila ya kujali mwili unaweza au la.

Au fikiria kama umewahi kuogelea kwenye maji na ukawa unazama, ulifanya kila kitu kuhakikisha unarudi juu na kupata pumzi. Taka kitu kwa shauku kubwa sana na akili yako haitajua ni wakati gani mwili umechoka na hivyo upumzike.

Mbinu ya pili; jua kwa nini unafanya.

Unapojua ni kwa nini unafanya kitu, na maana ile ikawa inaendana na kile ambacho unathamini sana kwenye maisha yako, basi hutajua ni muda gani wa kuchoka.

Kwa mfano unaweza kuwa umetoka kwenye shughuli zako na umechoka sana, na mtu akakuambia inabidi ubebe mfuko wa sementi na kuupeleka mahali, utakataa kabisa, hata kama anakulipa. Lakini katika hali hiyo hiyo mtoto wako ambaye ana uzito sawa na mfuko wa sementi akaanguka na anahitaji kuwahishwa hospitali haraka na usafiri hakuna karibu, utakuwa tayari kumbeba na kukimbia naye bila ya kujali uchovu uliokuwa nao awali.

Sasa niambie ni nini kimeondoa ule uchovu ambao ulikuwa nao awali? Maana kubwa ya kile ambacho unakifanya. Hivyo basi weka maana kubwa kwenye chochote unachofanya, na maana hiyo iwe inaendana na kile ambacho unathamini sana kwenye maisha yako na hutajua ni wakati gani wa kuchoka.

Mbinu ya tatu; penda sana kile unachofanya.

Kwa kupenda sana kile unachofanya, huwezi kujua ni wakati gani wa kuchoka, yaani unaweza kuwa umemezwa na kazi unayofanya, ukija kustuka muda umekwenda sana na hata hujaona kama muda umekwenda.

Kwa mfano chukulia unapokuwa unashiriki kwenye kitu kingine unachopenda, labda kuangalia tamthilia, unaweza kujikuta umekaa muda mrefu bila hata ya kustuka.

Ifanye kazi yako iwe kitu ambacho unakipenda sana na hutaona kuchoka hata kidogo, badala yake utahitaji kupata muda zaidi wa kufanya kazi yako.

Mbinu ya nne; ifanye kazi yako kuwa sehemu ya mchezo.

Hakuna mtu ambaye hapendi mchezo. Kwa mfano kama umetoka kwenye shughuli zako na umechoka sana, mtu akikuambia uende kumsaidia kazi fulani utasema umechoka sana na huwezi kufanya hivyo. Lakini mtu mwingine akikuambia mwende kucheza mchezo unaoupenda sana au kuangalia mchezo huo, utakuwa tayari kwenda kwenye mchezo huo.

Angalia ni jinsi gani unaweza kuigeuza kazi yako au baadhi ya maeneo yako kuwa mchezo ambao unaufurahia. Labda kugawa majukumu yako kwa njia ambayo kuyamaliza kunakupa dhana ya ushindi.

Mbinu ya tano; jipe motisha.

Kitu kingine kinachoweza kuidanganya akili yako na ikaweka juhudi kubwa sana ni kujipa motisha. Kwenye kazi yako angalia ni jinsi gani unaweza kujipa motisha wa kukusukuma kufanya zaidi.

Labda unaweza kuweka lengo fulani na ukilifikia ndio unapata nafasi ya kufanya au kununua kitu ambacho unakipenda sana. Kama unapenda kusafiri basi weka malengo ambayo kama ukiyafikia utajipa zawadi ya kusafiri. Kwa njia hii utajikuta unakazana sana ili uweze kukamilisha malengo yale na ufanye hiko ambacho unakipenda sana.

Sasa unaweza kuisimamia au tunaweza kusema kuidanganya akili yako na ikaulazimisha mwili kufanya kazi hata kama ulikuwa unaona umechoka. Fanyia kazi mbinu hizo tano na utaanza kuona ufanyaji kazi wako ukiongezeka.

Angalizo; mbinu hizi nilizokupa hapa ni kali sana hivyo kuwa makini sana unapozitumia. Hakikisha unapata ule muda wa kawaida w akupumzika ili usifike mahali mwili ukajifunga kabisa, kuna kitu kinaitwa BURN OUT, hiki hutokea pale ambapo mwili unakuwa umekosa mapumziko kwa muda mrefu. Tutajadili BURN OUT siku nyingine na kuangalia njia za kuepuka hilo. Sijawahi kupata burn out na nimekuwa nikijitahidi nisifike huko maana itakuwa tatizo kubwa sana. Nimeona wengi waliofikia burn out, ni changamoto kubwa sana.

Fanyia kazi hayo uliyojifunza, ili uweze kufikia mafanikio ya kiwango cha juu sana, ambayo ni watu wachache sana hapa duniani wanaoyafikia.

Kama ungependa tujadili tofauti ya mwili, roho na akili, weka maoni hapo chini(comment). Nahitaji maoni ya watu wasiopungua 20, watu tunaosoma makala hizi za WORLD CLASS tupo zaidi ya 60. Kwenye maoni andika chochote.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz