Kitabu THE ART OF LIVING ni kitabu kilichotafsiriwa kutoka kwenye maandiko ya mwanafalsafa wa zamani wa kigiriki aliyejulikana kwa jina la Epictetus. Epictetus alitengeneza falsafa nzuri ya maisha ambao ilimwezesha yeye mwenyewe na wanafunzi wake kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio. Epictetus alikuwa mwanafalsafa wa kistoa ambaye aliamini kwenye maisha ya mtu kuwa bora kutokana na maamuzi yake mwenyewe ya kufanyia kazi maisha yake. Aliamini maisha ya mtu hayawi bora au mabovu kutokana na matendo ya wengine, bali kutokana na matendo na fikra za mtu mwenyewe.
Kitabu hiki THE ART OF LIVING ni kitabu ambacho kinatoa mbinu nzuri na rahisi sana ambazo kama ukizifuata basi utakuwa na maisha bora sana, ya furaha na yenye mafanikio makubwa.
Karibu sasa tujifunze kupitia mambo 20 muhimu niliyokuandalia kutoka kwenye kitabu hiki;
1. Maendeleo binafsi na kuwa na maisha bora sio kitu ambacho kinatokea kwa bahati au kwa ajali, bali ni kitu ambacho kinafanyiwa kazi na ndio kinatokea. Hivyo wewe hapo ulipo sasa, unaweza kuwa bora zaidi kama utafanyia kazi maisha yako. na kumbuka wewe ndiye unayehitaji kuyafanyia kazi maisha yako ili yawe bora zaidi. Hakuna mtu mwingine wa kufanya kazi hii.
2. Lengo kuu la falsafa kwenye maisha yako ni kukuwezesha wewe kutatua changamoto unazokutana nazo kwenye maisha yako ya kila siku. Maisha yana changamoto nyingi, kuna ambazo unasababisha wewe mwenyewe na kuna ambazo zinasababishwa na wengine. Haijalishi ni nani kasababisha changamoto, haijalishi unahusika au huhusiki, kama changamoto ipo kwenye maisha yako, basi wewe ndio wa kuitatua. Unapokuwa na falsafa nzuri unaweza kutatua changamoto yoyote unayokutana nayo.
3. Epictetus aliamini kwamba maisha bora sio kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, au kufanya kitu ili kuwafurahisha wengine. Bali maisha bora ni kufanya kile ambacho kinakuridhisha wewe, kinachokupa amani ya moyo na unachofurahia kufanya. Na aliamini maisha haya bora yanaweza kupatikana kwa yeyote, masikini au tajiri, mwenye elimu kubwa au asiye na elimu kabisa. Ni swala la kujitambua na kuishi kulingana na kile ambacho ni muhimu kwako.
4. Ili uwe na maisha bora na yenye furaha, unatakiwa kujua vitu hivi viwili. Kwanza vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wako, hivi ni vile vitu ambavyo unaweza kuviathiri au kuvibadili. Pili ni vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako, hivi ni vitu ambavyo huwezi kuviathiri au kuvibadili. Hivyo wakati wowote unapokutana na changamoto ambayo inakusumbua, jiulize je hii ipo ndani ya uwezo wangu au nje ya uwezo wako, kama ndani ya uwezo wao chukua hatua. Kama ipo nje ya uwezo wako achana nayo na fanya kile ambacho unaweza kuathiri au kubadili.
5. Weka umakini wako kwenye vile vitu ambavyo vinakuhusu, na ambavyo ni muhimu sana kwako. Na jua ya kwamba mambo ya wengine hayakuhusu wewe, hayo ni yao. Usipoteze muda wako kuangalia wengine wanafanya nini au wanakosea wapi, badala yake tumia muda huo kuboresha kile ambacho unafanya wewe. Kwa njia hii utasonga mbele zaidi kuliko wale wanaopoteza muda kufuatilia mambo ya wengine.
6. Tamaa na chuki ni vitu ambavyo vinatuendesha sana. Tamaa inatusukuma kupata kile ambacho tunakutaka na tukipate sasa. Na chuki inatusukuma tuepuke kile ambacho hatukitaki. Na mara nyingi huwa hatupati kile ambacho tunataka, na hivyo kukata tamaa na tunapata kile ambacho hatukitaki na hivyo kupata msongo wa mawazo. Ili kuwa na maisha bora, hakikisha unaweza kusimamia nguvu hizi mbili.
7. Matatizo yanayotokea hayaharibu maisha yetu, bali fikra zetu na jinsi tunavyochukulia matatizo hayo ndio vinaharibu maisha yetu. Mambo yanatokea kama yanavyotokea, watu wanafanya vitu kama wanavyoamua kufanya. Fungua macho yako na ona vitu jinsi vilivyo na hii itakuondolea maumivu ya kujitakia mwenyewe. Jua kwamba mambo yanatokea na watu wanafanya wanavyotaka kufanya, ni kazi yako kuamua unachukuliaje kila kinachotokea.
8. Usijaribu kutengeneza sheria zako wewe mwenyewe. Bali yapeleke maisha yako kulingana na sheria za asili. Sheria za asili zimekuwepo na huwezi kuzivunja bila ya kuleta madhara. Kwa kujaribu kutengeneza sheria zako ambazo zinakwenda kinyume na sheria za asili, utakuwa na maisha magumu na usiyoyafurahia. Tengeneza maisha yako kwenye misingi inayoendana na sheria za asili na mambo yako yatakwenda vizuri sana.
9. Watu wenye akili ndogo huwalaumu wengine pale wanapopata matatizo. Watu wenye akili za kawaida hujilaumu wao wenyewe pale wanapopata matatizo. Watu wenye hekima wanajua ya kwamba kuwalaumu wengine kwa jambo lolote ni ujinga na hakuna chochote unachoweza kufaidi kwa kulaumu. Badala yake wanachukua hatua kwa kile kilichotokea.
10. Usitegemee sifa za wengine ndio ziwe hamasa ya wewe kufanya kitu. Bali fanya kile kitu ambacho tayari kinakupa hamasa. Kwa kutegemea wengine ndio wakupe hamasa unajiandaa kuanguka. Fanya kile ambacho tayari kinakupa hamasa, kile ambacho ni muhimu zaidi kwako, na usijali wengine wanasema nini, iwe wanasema kwa uzuri au kwa ubaya.
11. Tumia kile ambacho unacho sasa, na hiko ndio kitakupeleka mbali zaidi. Jiulize swali hili kila mara; NI KITU GANI MUHIMU NINACHO? Je una vitabu? Visome na tumia yale maarifa kuboresha zaidi maisha yako na kile unachofanya. Una wazo zuri? Anza kulifanyia kazi mara moja. Una kipaji? Anza kukiendeleza, anza kukifanyia kazi. Tumia kile ambacho unacho sasa, na hiko ndio kitakupeleka mbali zaidi.
12. Hakuna kitu chochote au mtu yeyote anayekurudisha wewe nyuma, hakuna kabisa. Wewe mwenyewe ndiye unayejirudisha nyuma. Kila kitu kipo chini ya usimamizi wako, kwenda mbele, kusimama au kurudi nyuma, vyote vipo chini ya usimamizi wako. Kila kinachokutokea, jua ya kwamba wewe ndiye mwamuzi wa mwisho, kama unaamua kuendelea mbele au unaamua kukata tamaa.
13. Kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha, kila gumu unalopitia, huwa linakuja na fursa kubwa sana ndani yake. Watu wengi wanapokutana na changamoto huanza kutafuta njia za kuikimbia. Lakini kama utaacha hivyo na kuamua kuipangua changamoto hiyo hatua kwa hatua, utaona fursa kubwa na nzuri sana ambazo zimejificha kwenye changamoto hiyo. Wakati wowote unapokutana na magumu, jiulize ni fursa gani naondoka nayo hapa? Na ukifungua macho yako, ni lazima utaziona fursa.
14. Hakuna kitu ambacho kinachukuliwa kwetu, hakuna kitu ambacho tunapoteza. Bali vitu vyote vinarudi vilikotoka. Badala ya kusema nimepoteza kitu fulani, sema kitu fulani nilichokuwa nacho kimerudi sehemu yake. Iwe ni mali ulikuwa nayo ikapotea, jua imerudi sehemu yake. Iwe ni mtu wako wa karibu amekufa, jua amerudi sehemu yake. Kwa kufikiria hivi hakuna jambo lolote ambalo litakusononesha kwenye maisha yako.
15. Elewa maana halisi ya uhuru na jinsi unavyoweza kuufikia, maana hapa ndipo ubora wa maisha yako unapoanzia. Uhuru sio kufanya chochote ambacho unataka kufanya, bali kujua mipaka yako kwenye maisha. Kwa kujua mipaka ambayo maisha yamekuwekea na vile vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako. Na kuweza kufanyia kazi hayo badala ya kupambana nayo, hapo ndio unakuwa umepata uhuru kamili wa maisha yako. na kwa upande mwingine kama unakubaliana na tamaa zako na kutekeleza basi unakuwa umepoteza uhuru wako wote.
16. Angalia sana wale watu ambao wamekuzunguka, angalia sana wale watu ambao unakaa nao muda mrefu. Kwa sababu tabia na mawazo yanaambukizwa. Kama unazungukwa na watu wenye mawazo hasi na wewe utakuwa na mawazo hasi, na kama unazungukwa na watu wenye mawazo chanya na wewe utakuwa na mawazo chanya. Hakikisha unazungukwa na watu wenye zile tabia ambazo ni nzuri kwako.
17. Hakuna mtu mwenye nguvu ya kukuumiza wewe. Hata kama mtu atakuambia maneno makali, hata kama mtu atakudharau, hata kama mtu atakutukana matusi, bado yeye hana nguvu ya kukuumiza. Wewe mwenyewe ndiye unayejiumiza kwa kuchukua kile ambacho watu wamefanya na kujiumiza kwa kitu hiko. Hivyo kama kuna mtu anakuchokonoa, jua ya kwamba wewe ndiye unayeweza kumpa nafasi ya kukuumiza. Na hivyo mchukulie kama ana matatizo yake binafsi na endelea na maisha yako.
18. Huwezi kupata kile ambacho wengine wamepata kama hupo tayari kuweka juhudi na muda kama wao walivyofanya. Kama unaona kuna wengine wamefanikiwa kuliko wewe, jua kwamba kuna vitu wametoa kuliko ulivyotoa wewe. Hivyo badala ya kuwaangalia kwa wivu tu, jua ni kipi ambacho wametoa na anza kukitoa kama unataka kufikia ngazi kama walizofikia wao.
19. Kama mtu angechukua mwili wako na kuwapa watu auchezee kama wanavyotaka ungejisikiaje? Hakika usingekubali, ungekataa kabisa na kulinda mwili wako. Lakini mbona unaruhusu kutoa akili yako kila mtu aichezee anavyotaka mwenyewe? Kwa nini unakubali akili yako ijazwe hofu za wengine, ijazwe taarifa zisizo za msingi kwako? Linda akili yako kuliko hata unavyolinda mwili wako, maana hiki ni kitu cha thamani sana kwako.
20. Kama utaamua kuishi maisha ambayo ni bora kwako, kama umeamua kufuata misingi hii mizuri ya maisha, basi jiandae kuchekwa. Jiandae kudhihakiwa na jiandae kukatishwa tamaa. Kwa sababu watu wengi hawatakuelewa, lakini kumbuka hilo sio tatizo lako, bali ni matatizo yao binafsi.
Je upo tayari kuishi maisha ambayo ni bora sana kwako? Maisha yatakayokupa furaha ya kudumu kwenye maisha yako na kukuletea mafanikio makubwa? Basi jua kitu hiki kimoja muhimu, kila kitu kipo ndani yako. ni wewe kufanya maamuzi leo na kuchukua hatua mara moja.
Kumbuka maisha ni kuchagua, na unaweza kuchagua kuwa na maisha bora au kuchagua kuwa na maisha ya hovyo. Yote haya ni maamuzi unayofanya wewe mwenyewe, hakuna mwingine wa kukufanyia maamuzi haya.
Nakutakia kila la kheri kwenye maisha bora uliyochagua kuishi.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.