Kabla hujafungua mdomo wako, kwanza shirikisha akili yako.

Kufungua mdomo kabla ya kushirikisha akili ni chanzo kikubwa cha matatizo yako na watu wengine.

Kabla ya kufungua mdomo ni vizuri ukafikiri kwa kina, ili kile unachokwenda kuzungumza kiwe bora.

Baadhi ya maswali unayoweza kujiuliza kabla ya kufungua mdomo wako;

1. Je hiki ninachokwenda kusema ni muhimu?

2. Je kinaweza kumsaidia mtu ambaye atakisikia?

3. Je kina mchango chanya kwa kila atakayekisikia?

Kama majibu ni ndio kwenye maswali yote, basi unaweza kusema kitu hiko, na hakika kitakuwa msaada kwa wengine.

Ila kama utaongea tu bila ya kufikiri, utajikuta unaongea vitu ambavyo sio muhimu, au visivyo na msaada wowote kwa wengine na mbaya zaidi vinakuwa na mchango hasi.

Na pia unapoongea bila ya kufikiri utajikuta unaongea sana, na ukishakuwa muongeaji sana, jua wewe ndiye utakayepoteza. Wanaopata zaidi ni wale wanaosikiliza na kuangalia zaidi ya wanavyoongea.

Na kumbuka neno likishatoka kwenye mdomo wako huwezi kulirudisha tena. Ni vyema ukaongea kile ambacho unaweza kukisimamia.

Kabla hujafungua mdomo wako kuongea, shirikisha akili yako na hakikisha unaongea kitu chenye mchango mkubwa. Hii ni muhimu sana kwa kupata na kuendelea kuwa na mafanikio makubwa.

SOMA; Usidharau Ushindi Mdogo Mdogo Unaoupata Kila Siku, Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako, SEHEMU YA PILI.

TAMKO LANGU;

Kabla sijaongea nitaishirikisha akili yangu ili kuhakikisha naongea kitu ambacho ni muhimu, kina msaada kwa wengine na kina mchango chanya pia. Sitakubali kuongea tu kwa sababu naweza kuongea, bali nitaongea kwa sababu nataka kutoa mchango muhimu. Hii ni muhimu sana kwa mafanikio yangu.

NENO LA LEO.

“Open your mind before your mouth”

― Aristophanes

Fungua akili yako kabla hujafungua mdomo wako.

Ongea kitu ambacho ni muhimu, kinaweza kuwasaidia wengine na kina mchango chanya kwa kila anayesikiliza.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.