Mtego Uliotengeneza Unajua Kinachotakiwa Kunaswa?

Habari za siku msomaji wangu wa Amka Mtanzania, nafikiri unaposikia neno AMKA kuna kitu kinajengeka kichwani mwako. Ikiwa hujawahi kufikiri hili neno naomba ujue kwamba, tunapaswa kuamka watanzania.
Asilimia kubwa tulipolalia sio sahihi na asilimia ndogo sana imelalia sehemu sahihi.
Ndio hiyo hiyo asilimia ndogo inayohangaika usiku na mchana kujiletea mafanikio makubwa zaidi, na sisi wa asilimia kubwa tumeendelea kutazama watu fulani labda watatimiza ndoto zetu huku sisi tukiendelea kupumzika na kulalamika.

Tunapaswa kujua kwamba giza lina masaa yake na mwanga una masaa yake. Lazima ujue kucheza na haya majira, isiwe wakati wa giza wewe unalipuzia na kuendelea kupoteza muda wako kwa vitu visivyofaa na wakati wa kupambazuka wewe ndio unakumbuka kulala.

 
Baada ya salamu hizo, naamini umejiandaa kujifunza somo letu la leo, elewa siku zote mwingiliano wa mahitaji ya mwanadamu ni mengi.
Kila mmoja anatamani kuwa katika hali fulani ya kumvutia yeye kama yeye, na hapo hapo wengine hatujui tunataka nini ila tunajaribu kugusagusa kila kitu ilimradi siku ipite, tuonekane na sisi tulikuwepo katika kuwajibika.

SOMA; Sheria 12 Kwa Wanaoanza Biashara Kutoka Kwa Bilionea Mark Cuban.
Maisha ya sasa na ya zamani hayakuwa hivyo, japo tunaweza sema kuna mabadiliko makubwa sana ukilinganisha sasa na zamani.
Amini kwamba hata hiyo zamani ilikuwa na changamoto yake, mfano mwaka uliopo leo ukija kujikumbusha miaka 10 au 20 ijayo kama Mungu atakupa uzima. Utaona mambo ya leo ni ya kizamani sana.
Kwa hiyo tuelewe kwamba jinsi maisha yanavyoenda mbele utaona nyuma ilikuwa afadhali wakati upo hapo uliona ni pa gumu sana.

Nikupe mfano kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, akiwa hilo darasa anaona mambo magumu sana. Ila baada ya kuvuka hilo darasa anaona mambo magumu yapo kidato cha pili na si cha kwanza. Vivyo hivyo mpaka anafika kidata cha nne, tano na sita anaona hali ile ile.
Iweje maisha yanakuwa hivi, ni kwa sababu leo yetu huwa tunaiona ya kawaida na ngumu. Laiti kama tungekuwa tunapambana na kuitazama leo yetu kama ni ya pekee, tungeiandaa kesho yetu vyema sana.
Lazima tungekuwa na furaha na mapambano makali sana ya kuilinda leo yetu kuliko kuisubiria kesho usiyoijua, ukifikiri kwamba inaweza ikawa afadhali kuliko leo.

Wawindaji wa nyama, huwa wana mitengo yao ya kuwanasa wanyama/ndege kwa ajili ya kitoweo chao. Mwindaji siku zote huwa yupo makini sana katika kutega, haijalishi kile anachokitenga kitakuja muda gani, ila yeye anachojua ni kwamba hilo eneo lina kile anachokitaka.
Huyu mtegaji hutega halafu hukaa pembeni kusubiri mtego unase mnyama/ndege, macho yake huwa makini sana kutazama mtego.
Pindi inapotokea ameona kuna kitu kile alichosubiria kimenasa, hukimbia haraka sana. Huwa hatafuti njia ya mzunguko, yeye hupita katikati, anachojua afike tu kwenye mtego wake hata kama kuna miiba, itokee ameanguka bahati mbaya kwa kujikwaa, yeye macho yake huwa kwenye mtego ulionasa kitoweo chake.

Maisha ndio yanavyotaka, lazima utazame kile ulichopanga kiwe katika maisha yako, lazima uongeze bidii ya uvumilivu katika kusubiri huku ukiendelea kuongeza ubunifu na nguvu kwa kile unachokifanya leo.
Mwindaji alitumia akili ya kutengeneza mtego na nguvu wakati wa kunaswa mnyama/ndege aliyemtarajia, hukimbia kwa nguvu zote.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Kijana Wa Kitanzania(kama una miaka kati 20 mpaka 30 soma hapa)
Nikusihi kwamba; chochote unachokitaka katika maisha yako kinawezekana kama utakuwa unajua ulichotega. Huwezi kutega swala akanasa fisi ukafurahia kupata kitoweo, lazima utamwondoa kwa hasira halafu utarudishia mtego wako mpaka pale utakaponasa kile ulichokitaka.
Umenasa kitu usichokitaka, nasua uendelee kusubiri kile unachokitaka kinase. Usipoteze lengo, endelea kuongoza umakini katika kukitazama, kama upo kazini na unatamani kufika nafasi fulani. Hakuna wa kukuzuia, endelea kuongeza bidii katika ufanyaji wako wa kazi, endelea kuonyesha uwezo wako kwa nafasi uliopo huku ukilinda mtego wako kwa umakini.
Pindi itakapotokea nafasi hiyo unayoitaka uwe wa kwanza kuiona na uwe wa kwanza kupendekezwa wewe, hutakuwa na mshangao wala hutazubaa kama alivyo mwindaji.

Umejua kinacholeta kile unachokitaka, ni wewe kujua unataka nini, sasa kuanzia leo jua mtego wako, jua unahitaji nini.
Unahitaji kitoweo au unafuata watu waliotega ila hujui unachokihitaji, nakwambia utanasa fisi na wewe ulihitaji swala. Kuepuka hilo lisikutokee, acha kufuata mkumbo bali jua kile unachotaka.

Makala hii imeandikwa na rafiki yako Samson Ernest.
BLOG;
www.mtazamowamaisha.blogspot.com
EMAIL; samsonaron0@gmail.com
SIMU; 0759808081.
Endelea kutembelea mtandao huu kila siku kwa makala nzuri zaidi, maana kujifunza ni kila siku na si siku moja.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: