Habari mwanafalsafa mwenzangu?
Ni imani yangu kwamba uko vizuri na kupitia falsafa yetu hii mpya ya maisha, kuna mengi sana umeshaweza kujiepusha nayo. Najua kuna mengi zamani ulikuwa ukifanya tu bila ya kutafakari kwa kina, ila kwa sasa, baada ya kuwa unajifunza kupitia falsafa mpya ya maisha, basi umeanza kutafakari kabla ya kufanya jambo lolote. Hii ni vizuri sana. Na kama hujaanza kufanya hivi basi anza mara moja. Na wala usisubiri, anza leo na hiki muhimu utakachokwenda kujifunza kwenye makala ya leo ya falsafa moja ya maisha.
Dunia ipo ilivyo mpaka sasa kwa sababu dunia ina njia zake za kujilinda. Dunia ina sheria zake za asili ambazo kila mtu ni lazima azifuate. Kushindwa kuzifuata sheria hizi za asili, maisha yako hayataweza kwenda hapa duniani, na hivyo utaondoka na kuiacha dunia. Kama ambavyo tumekuwa tunaona kwenye makala zilizopita za FALSAFA MPYA YA MAISHA, huwezi kuidanganya dunia, kwa sababu yenyewe imekuwepo kabla yako na itaendelea kuwepo baada yako. Imejijengea mfumo mzuri sana wa kujilinda na kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri. Ndio maana mtu anaweza kutafuta njia ya mkato ya mafanikio, lakini baadaye njia hii ikamtesa sana, na ni lazima hilo litokee.
Kama hujasoma makala za nyuma za falsafa mpya ya maisha bonyeza maandishi haya.
Sasa leo tunakwenda kushirikishana sheria nyingine ya dunia ambayo ni muhimu sana kila mmoja wetu akaielewa. Kwa kuielewa sheria hii utapunguza nusu ya matatizo yako na utaweza kutatua sehemu kubwa ya changamoto unazokutana nazo kila siku kwenye kazi zako, biashara zako na maisha yako kwa ujumla. Si unakumbuka hakuna maisha ambayo hayana changamoto? Hivyo kikubwa ni wewe kuwa na maarifa sahihi ya kuweza kutatua changamoto. Leo utajifunza kupitia sheria hii muhimu tutakayojifunza.
Hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya(au hata nzuri).
Mara nyingi tumekuwa tukitoa sababu nzuri sana pale ambapo jambo fulani limetokea. Kama ni jambo baya basi tunaweza kusema ya kwamba ni bahati mbaya, na kama ni jambo zuri basi tunaweza kusema ni bahati nzuri.
Kusema bahati mbaya au nzuri ni njia tu ya kukwepa kuuangalia ukweli wa mambo ulivyo.
Kwa mfano mtu anaendesha biashara, kadiri siku zinavyokwenda biashara inadorora na inafika siku biashara inakufa kabisa. Yeye atakachofikiria ni kwamba biashara yake imekufa kwa bahati mbaya.
Au mtu ameajiriwa na kufanya kazi vizuri mwanzoni, lakini kadiri siku zinakwenda kazi yake inadorora, mahusiano yake na wengine yanadorora na mwishowe anafukuzwa kazi. Anaweza kuwa na sababu nyingi nzuri sana kwa nini hilo limetokea, lakini hawezi kujua jinsi sheria ya asili imeingia hapo.
Mfano mwingine ni watu wanaooana, wanaanza maisha wakiwa na furaha kubwa sana, wanapendana, wanakwenda pamoja, lakini kadiri siku zinakwenda mambo yanaanza kubadilika, upendo unapungua, matatizo yanakuwa mengi na hatimaye ndoa inaishia kuvunjika. Wanandoa hawa wanaweza kuwa na sababu lukuki kwa nini ndoa ile imevunjika, lakini mara zote hawatagusia sababu ya msingi sana ambayo inatokana na sheria ya asili, ambayo walishindwa kuifuata.
Hakuna kitu ambacho kinatokea kwa bahati mbaya au nzuri.
Sheria ya asili, kila kitu kinasababishwa.
Kuna sheria moja ya asili ambayo madhara yake unayajua, ila sheria yenyewe huenda huijui vizuri. Sheria hii inasema kwamba KILA KITU AMBACHO KINATOKEA, BASI KINASABABISHWA. Yaani hakuna kitu kinachotokea chenyewe tu, lazima kuwe na kisababisho ndio kitu fulani kitokee.
Kila kitu kinachotokea kwenye maisha, kinasababishwa, na kinasababishwa na watu, hakuna zaidi ya hapo.
Biashara ambayo inaendeshwa vizuri, haitokei vile kwa bahati mbaya, bali inasababishwa na mfanyabiashara anayejua njia sahihi za kuendesha biashara. Na biashara inayokufa haifi tu bila sababu, bali inauliwa na mfanyabiashara asiye na maarifa ya kuendesha biashara, au asiye makini na biashara yake. Biashara haifi yenyewe, bali inauliwa, na inauliwa na watu.
Mazingira bora ya kazi, ambapo wewe kama mfanyakazi una uzalishaji mzuri na kufurahia kazi yako, hayatokei kama ajali, bali yanasababishwa. Na yanasababishwa na mfanyakazi mwenyewe na wale wanaomzunguka pia. Na hata mazingira haya yanapokuwa magumu na mtu kushindwa kuendelea kuwepo hakutokei kwenyewe, bali kunasababishwa, na kunasababishwa na mfanyakazi mwenyewe na wale wanaomzunguka.
Na tukija kwenye ndoa, ndoa yenye furaha, ambapo wanandoa wanaelewana na kupendana, haitokei kwa bahati mbaya, bali inasababishwa na wanandoa wenyewe. Vile vile ndoa inapofikia hatua ya kuvunjika, hakuna maajabu hapo, bali wanandoa wenyewe wamesababisha ndoa ivunjike.
Umeanza kupata picha jinsi ambavyo sheria hii ya asili inaingia kwenye kila eneo la maisha yako? sasa twende kwenye eneo muhimu sana, ambalo ni wewe mwenyewe.
Wewe ndiye msababishaji mkuu.
Sasa tukirudi kwenye maisha yako wewe, uko hapo ulipo sasa, kutokana na visababisho ulivyotoa awali. Yaani wewe mwenyewe ndiye ambaye umejisababishia kuwa hapo ulipo sasa. Iwe ni mahali pazuri ambapo unapapenda, au ni mahali ambapo sio pazuri na hivyo hupapendi, wewe mwenyewe ndiyo umejipeleka hapo.
Bado huelewi vizuri?
Ni kwamba maisha ambayo umechagua kuishi, iwe kwa kujua au kwa kutokujua ndio yamekufikisha hapo ulipo sasa.
Kama upo kwenye biashara ambayo haikui, kila siku inapata hasara na unazidi kuteseka, jua ya kwamba wewe ndiye umesababisha hayo yote. Wewe mwenyewe umekuwa unaendesha biashara yako huenda kwa mazoea, kwa kukosa maarifa sahihi au kwa kukosa umakini mkubwa. Hakuna cha ziada. Hata kama umeajiri watu ndio wakaua biashara yako, bado ni wewe mwenyewe umeiua, kwani kuna mtu alikulazimisha uwaajiri? Na ulipowaajiri kwa nini hukuweka vigezo vizuri? Na hata baada ya kuwaajiri umekuwa unawasimamia vyema? Na je umekuwa unahakikisha na wao wana maarifa sahihi ya kuendesha biashara yako?
Kama upo kwenye kazi ambayo imekuwa mzigo kwako, unaiona kama kifungo kwako, na haikupi furaha kabisa, wewe ndiye ambaye umejiweka hapo, na wala hakuna mtu mwingine yeyote. Wewe mwenyewe kwa kujua au kutokujua umejisababishia kuwa kwenye kazi hiyo, na kwa mambo unayoendelea kufanya sasa unaendelea kujihakikishia kwamba hutoki hapo. Kwa kutokufikiria njia nyingine mbadala, kuendelea kufanya kazi kwa mazoea, kushindwa kujiendeleza kwenye maeneo mengine, ni kuamua wewe mwenyewe kwamba hapo ndipo kikomo chako. Kwa kutumia kipato chako chote unachopata kwenye kazi hiyo, na kama haitoshi unakopa kupitia kazi hiyo, ni sababu mojawapo ya wewe kuendelea kuwepo hapo zaidi na zaidi na kufunga njia zote ambazo zingeweza kuja kukutoa hapo. Wewe mwenyewe unasababisha.
Hangaika na sababu(chanzo) na sio matokeo.
Nafikiri mpaka sasa tumeshaanza kuwa pamoja, kwa kukiri kwamba wewe umekuwa unasababisha kile ambacho kinaendelea kwenye maisha yako. vizuri sana.
Sasa tuingie sehemu moja ambayo ndiyo ina maajabu makubwa duniani. Pale mtu anapogundua ya kwamba kile kinachotokea ni tatizo, anachukua hatua gani? Hapa ndipo utakaposhangaa.
Watu wanapoona hili sasa ni tatizo, wanaanza kuhangaika na matokeo, si matokeo ni mabaya, basi tuyabadili haya matokeo haraka sana.
Biashara haiendi vizuri, inapata hasara? Labda nichukue mkopo, utanisaidia kukuza biashara yangu.
Au kazi haiendi vizuri? Kuna watu wananipikia majungu, ngoja nianze kupambana nao.
Ndoa imekuwa na changamoto nyingi, hakuna kuelewana? Ngoja nahakikisha nimembadilisha huyu mwenzangu.
Ni hatua za haraka ambazo wengi wamekuwa wanachukua kila siku, huenda na wewe umewahi kuchukua hatua za aina hii.
Lakini hatua hizi zinaleta matunda gani? Zinazidisha tatizo mara dufu, yaani kama ni moto basi hatua hizi zinakwenda kuchochea zaidi. Biashara inayojiendesha kwa hasara, kuchukua mkopo ni kumwaga petrol kwenye moto, kwa sababu sasa utakuwa na matatizo mawili, biashara iliyokufa na mkopo wa kulipa. Kazi inayokupa changamoto kuanza kupambana na watu ndio umejimaliza kabisa, kwa sababu hawa watakupa wakati mgumu kuliko ulivyowahi kufikiri. Na ndoa unayokazana kumbadili wenzako? Mh utaziongeza zile changamoto mara dufu.
Badala ya kuhangaika na matokeo, hangaika na chanzo, hangaika na kile ambacho umesababisha wewe, na mambo yataanza kujipanga vizuri yenyewe, unaweza kutatua changamoto nyingi sana kama utaanza kuhangaika na kile ulichofanya mpaka kikapelekea changamoto hiyo kutokea. Pale utakapojua ni nini umefanya na kikasababisha changamoto kwenye biashara yako, kazi yako na maisha yako kwa ujumla, na kuanza kurekebisha hapo, matokeo yatabadilika yenyewe.
Jinsi ya kuepuka nusu ya matatizo yako.
Kama unataka kuepuka nusu au hata zaidi ya nusu ya matatizo yako, basi fikiria sheria hii ya asili kabla hujafanya kitu chochote. Kabla hujakubali chochote, kabla hujachukua hatua yoyote, jiulize hiki ninachokwenda kufanya, kinaweza kusababisha nini?
Angalia yale matokeo ambayo yanaweza kutokea na jiulize kama ni matokeo ambayo unayapenda, kama sio acha, kama ndio fanya.
Jiulize swali hili kwenye kila kitu cha maisha yako, kabla ya kufikiri, kabla ya kusema na kabla ya kutenda.
Kwa sababu kama tulivyowahi kuona kwenye makala zilizopita, fikra zako pia zinavutia yale yanayotokea kwenye maisha yako. hivyo hata fikra zako zenyewe ni sababisho tosha.
Kuanzia sasa jua ya kwamba kila kitu kinasababishwa, na wewe mwenyewe umekuwa msababishaji mkubwa wa kile ambacho kinatokea kwenye maisha yako. na kama unataka kubadili maisha yako, kama unataka kuyafanya kuwa bora zaidi, basi unahitaji kuanza na kile unachofanya na sio kuhangaika na matokeo unayopata.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi sheria hii ya asili ya maisha.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.