Pale ambapo changamoto haikuhusu ni rahisi sana kutoa ushauri, kwa sababu hujashikwa hisia zako na changamoto hiyo na hivyo kuweza kuona vitu kama vilivyo. Kwa hiyo ni rahisi kuona wapi pa kupita ili kuweza kuitatua.

Changamoto inapokuwa inakuhusu wewe, hisia zako zinakuwa juu na siku zote hisia zikiwa juu basi fikra zinakwenda chini.

Sasa leo nataka nikushirikishe kitu kimoja muhimu sana kitakachokuwezesha kutatua changamoto nyingi unazokutana nazo.

Kwanza ona kama vile changamoto hii haipo kwako, ona ipo kwa mwingine, labda rafiki yako au mtu wa karibu. Jione wewe uko huru kabisa, yaani huna changamoto yoyote.

Pili anza kutoa ushauri kwa yule ambaye umembambikizia changamoto ile. Fikiria ungeweza kumshaurije rafiki yako au mtu mwingine ambaye amekutana na changamoto ya aina hiyo.

Tatu chukua ushauri ule na anza kuufanyia kazi. Uchukue kama ulivyo na ufanyie kazi, usianze kujidanganya kwamba hali yako ni tofauti au unachopitia wewe ni kikubwa sana.

Ukiweza kufanya hivi utaweza kutatua changamoto nyingi sana ambazo unakutana nazo kwenye maisha yako ya kila siku. Jipe ushauri kama vile changamoto uliyonayo anayo mtu mwingine na fanyia kazi ushauri ule.

SOMA; USHAURI ADIMU; Tangaza Kazi Yako, Usione Aibu Wala Kujali Wengine Watakuonaje.

TAMKO LANGU;

Najua ni rahisi kutoa ushauri kama si husiki. Na ni vigumu kujipa ushauri kwa changamoto zangu mwenyewe kwa sababu naruhusu hisia zangu zinitawale. Kuanzia sasa ninapopata changamoto nitaifanya kama siyo yangu na kuipeleka kwa mwingine, kisha nitaanza kumshauri mtu huyu na nitachukua ushauri huo na kuanza kuufanyia kazi.

NENO LA LEO.

When we ask for advice, we are usually looking for an accomplice.

Saul Bellow

Tunapoomba ushauri, huwa tunaangalia ule unaoendana na sisi.

Kwa nini usiwe mshauri wako mwenyewe? Anza kwa kuona tatizo sio lako, kisha toa ushauri na anza kufanyia kazi ushauri huo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.