Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Wiki hii tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinaitwa The Art of Living. Kitabu hiki kinafundisha falsafa nyingi za maisha ya furaha na ya fanisi. Mafundisho hayo ni kutokana na mwanafalsafa wa Zamani sana wa Kigiriki aliyejulikana kama Epictetus. Katika Kitabu hiki cha The Art of Living mafundisho hayo yametafsiriwa na kufafanuliwa na mwandishi anayeitwa Sharon Lebell.

 
Karibu tujifunze.
1. Fanya kila uwezalo kutawala matakwa/matamanio yako, maana unapotamani kitu kilicho nje ya uthibiti wako ni dhahiri masikitiko yatakufuata, utaishia kuvunjika moyo au kukata tamaa, wakati huku ukitelekeza/ kutupilia mbali vile vitu muhimu ambavyo vipo ndani ya udhibiti wako na vinastahili kutamaniwa. Do your best to rein in your desire.
2. Jitengenezee Sifa yako mwenyewe. Kamwe usitegemee pongezi kutoka kwa wengine, usitegemee kupewa sifa na wengine ili ufanye jambo fulani. Sifa binafsi haiwezi kupatikana kutoka kwenye vyanzo vya nje kama kupongezwa, wala haipatikani kwa kuambatana na watu fulani wenye sifa nzuri. Wewe umepewa kazi yako ya kufanya hapa duniani, itambue kisha fanya kazi hiyo. Hao unaowaona wana sifa nzuri na wamefanya mambo makubwa ni kwa sababu walitambua hili jambo kwamba sifa njema haipatikani kwa watu wa nje bali inapatikana kwao binafsi kwa kuitengeneza, kwa kutimiza wajibu wao vizuri sana. Timiza wajibu wako vizuri kabisa wala usiangalie ni nani anakutazama.
3. Katika maisha usitegemee kila mtu akubaliane na mawazo yako. Ukweli wa maisha ni kwamba watu wengine, hata wale wanaokupenda hawatakua na ulazima wa kukubaliana na mawazo yako, wala hawatakua na ulazima wa kukuelewa wewe, wala kushiriki shauku yako.
4. Ili uwe na Amani, Kubaliana na matukio kama yanavyotokea. Usitegemee matukio yatokee kama ambavyo ungetaka. When something happens, the only thing in your power is your attitude toward it; you can either accept it or resent it.
5. Tumia vizuri kila kinachotokea kwako. Kila tatizo au ugumu wowote katika maisha huambatana na fursa ya kuibua rasilimali za ndani zilizofichika ndani yako. Mitihani (changamoto) tunayokumbana nayo inapaswa kutusaidia kuutambua uimara/uwezo wetu. Unapokumbana na tatizo kabla hujatafuta msaada wa nje, kwanza jitazame ndani yako na jiulize, je ni rasilimali gani uliyonayo ya kukuwezesha kukabiliana na tatizo hilo. Chimba ndani kabisa. Maana ndani yako unayo rasilimali kubwa ambazo unaweza usigundue kama unazo. Find the right one. Use it
SOMA; Mambo 6 Yatakayokufanya Uzidi Kuwa Bora Na Mwenye Mafanikio Makubwa.
6. Yafanye matakwa yako yaendane na uhalisia. Tambua kwamba maisha na asili (nature) vinatawaliwa na sheria ambazo haziwezi kubadilika. Kwa kadiri unavyoweza kukubaliana na hili kwa haraka ndivyo unakua mtulivu zaidi. Utakua mjinga kama utataka mwenzi wako au watoto wako waishi milele. Wao ni binadamu kama ulivyo, na sheria ya kufa ipo nje ya uwezo wako. Pia ni ujinga kufikiri kwamba mwajiriwa, ndugu au rafiki anaweza kuishi bila kukosea kabisa. This is wishing to control things that you can’t truly control.
7. Yakabili maisha kama Karamu. Fikiri maisha yako kama vile upo kwenye karamu au sherehe, na vyakula mbalimbali vinapita mbele yako, kazi yako ni kujipakulia kiasi cha kukutosha na kuweka kwenye sahani yako. Kama kuna aina ya chakula kimekupita hujachukua, unaridhika na kile ulichochukua tayari na kuwa mwenye shukrani kwa ulichopata. Kama chakula fulani hakijapita kwako unakua mwenye subira maana zamu yako inakuja. Hivyohivyo chukua mtazamo huu katika maisha kwa kua mwenye kujizuia kwa upole na kubaki mwenye shukrani pale kile ulichokua unakitaka kinapochelewa au kukupita. You will get your rightful portion when it is your time.
8. Fahamu nini maana ya uhuru na jinsi ya kuupata. Uhuru sio kule kuwa na haki au uwezo wa kufanya chochote unachoona kinakufaa. Uhuru wa kweli unatokana na kufahamu mipaka ya nguvu zako mwenyewe na mipaka ya kiasili iliyowekwa na Mungu. Kukubaliana na mipaka ya maisha na vile visivyoweza kuepukika kwa kufanya navyo kazi badala ya kupambana navyo ndio tunakua HURU. Kwa upande mwingine kama tunakabiliwa na matamanio yetu ya vitu ambavyo viko nje ya uwezo wetu hapo uhuru wetu unapotea. Understand what freedom really is and how it is achieved.
9. Maisha ni kama mchezo wa kuigiza, na sisi ndio waigizaji wa mchezo huo. Kila mtu anayo kipande chake cha kuigiza kwenye mchezo huo na kila mtu amepewa majukumu yake. Kuna wengine wamepewa kazi ya kuigiza kwenye maigizo mafupi wengine marefu. Kinachopaswa hapa ni kila mtu kucheza kwa ustadi sehemu yake ya igizo hili. Kama wewe unapaswa kuwa msomaji, soma kwa ustadi, kama wewe unapaswa kuwa mwandishi, andika bila kukoma, kama wewe unapaswa kucheza kama mfanyabiashara, fanya biashara kwa viwango wa juu. Act Well the Part That Is Given to You
10. Hakuna anayeweza kukuumiza. Watu hawana nguvu au uwezo wa kukuumiza wewe, hata mtu akikutusi hadharani, uchaguzi ni wako wa kuchukulia kama tusi au la. Mtu anapokuudhi, siyo yeye anayekuudhi bali ni ile tafsiri yako uliyonayo juu ya hicho ulichofanyiwa ndiyo inakuudhi. Mtu anapokutukana halafu ukakasirika, tatizo sio lile tusi, bali ni tafsiri yako uliyonayo kuhusu lile tusi ndiyo inayokupa shida. Uwezo wa kuudhika au kutokuudhika upo juu yako, ukiamua kutafsiri kama jambo baya na kuudhika au ukaamua kupuuzia na kufanya yako, yote hayo yapo ndani ya uwezo wako. It is not things that disturb us, but our interpretation of their significance
SOMA; Hatua Sita Za Kubadili Maisha Yako Na Kufikia Mafanikio Makubwa.
11. Epuka kupokea mawazo hasi ya watu wengine. Unapokutana na rafiki au ndugu yako aliyeumizwa moyo au amekumbwa na matatizo, anapokua anakusimulia hizo habari jitahidi sana usizame na wewe na kujikuta wote mpo ndani ya tatizo. Unachopaswa kufanya pale unapokutana na mtu mwenye habari hasi (pengine kakumbwa na matatizo) ni kuweza kutofautisha kati ya tukio (tatizo) lenyewe lililompata na tafsiri yake juu ya tatizo. Kumbuka tafsiri aliyonayo juu ya lile tatizo ndiyo inayomuumiza. Jitahidi na wewe usiingie kwenye mtego huo Kisha ukashindwa kumsaidia. Sio ishara ya huruma au urafiki mwema kwa watu tunaowajali kuungana nao kwenye hisia hasi walizonazo. We do a better service to ourselves and others by remaining detached and avoiding melodramatic reactions.
12. Kutafuta kuwapendezesha watu ni mtego hatari sana. Katika kujaribu kupendeza wengine, tunajikuta tunajipoteza kwenye vile vilivyo nje ya ushawishi wetu. Kufanya hivyo tunapoteza kusudi letu la maisha. Kama unataka kuishi maisha yaliyojaa hekima na busara, ishi kwa kuzingatia vigezo vyako mwenyewe. Jiridhishe mwenyewe kwa kua mtu wa kupenda hekima na mtafuta kweli. Return and return again to what is essential and worthy. Do not try to seem wise to others.
13. Ni kitu kimoja kutaka kua bingwa au kufanya kitu kwa ustadi, na ni kitu kingine kutenda sawasawa na bingwa anavyopaswa kutenda. Usiishie kutaka, maana hatua hii ni wengi wanaoifikia, nenda mbele zaidi kwa kutenda vile vitu vinavyopelekea kua bingwa. Kama unataka kuwa tajiri, usiishie kutaka tu, jifunze na tenda vile matajiri wanatenda.
14. Jali akili yako kuliko unavyojali mwili wako. Watu wengi hutumia muda mwingi kwenye kujali na kutunza miili yao kuliko wanavyofanya kwenye akili. Kwa wanaofahamu, akili ni asset (mali) yenye thamani kubwa sana. Hakikisha unaiendeleza ili kuiongeza thamani. Ukipoteza ulivyonavyo, kitu pekee kinachokuwezesha kupata vingine, ni akili yako. Akili yako inapoongezeka thamani, ndivyo maisha yako yanavyoongezeka thamani. Thamani ya maisha yako inaongezeka kwa kujali na kutunza akili yako na sio mwili wako. Care About Your Mind More Than Your Body
15. Hekima inadhihirishwa kupitia vitendo na si maneno tu. Usitumie muda mwingi kuwashawishi watu kwamba wewe una hekima, Tabia yako iakisi hekima kupitia matendo yako.
16. Kuishi kwa hekima ni muhimu zaidi kuliko kufahamu hekima. Usiishie tu kufahamu hekima, nenda mbele zaidi kwa kuishi hekima. Wengi hua wanapenda kuonekana wanafahamu hekima, lakini hawaziishi, na ndio maana unakuta baadhi ya watu wanachosema au kufundisha sio wanachokiishi. Hujaona walimu wanaofundisha mafundisho mazuri sana, lakini ukiwatazama, unaona utofauti mkubwa kati ya mafundisho yao na wao walivyo. There is a big difference between saying valuable things and doing valuable things.
SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.
17. Imani tunazofunzwa na jamii mara nyingi sio za kutegemewa. Imani nyingi tulizonazo tumezipata kupitia mafunzo mabaya, yasiyo sahihi au ya kijinga. Na asilimia kubwa ya imani hizo zimejikita ndani kabisa ya akili zetu kiasi kwamba zimefichika hata kwetu wenyewe. Yaani inakua ngumu kuzigundua kama ndizo zinatukwamisha katika maisha. Unahitaji kujifunza vitu vipya sana huku ukijichunguza mara kwa mara, ili kuzigundua imani hizo na kuachana nazo kwa kuamini imani nyingine zilizo sahihi. Imani hizo mpya unahitaji kuziweka katika matendo mara kwa mara ili ziweze kujikita kama zile za awali zilizokua sio sahihi. Usipozifanyia kazi imani zilizosahihi, ni rahisi zaidi zile za mwanzo kurudia kwenye nafasi yake.
18. Kama tunavyosafisha nyumba zetu na kuziweka kwenye mpangilio mzuri, vivyo hivyo akili zetu zinahitaji kufanyiwa hivyo ili kusonga mbele vizuri kwenye jambo lolote. Akili zetu zinahitaji kutunzwa, kusafishwa na kuwekwa kwenye mpangilio mzuri muda wote. Kudumisha usafi wa akili yako, ni kwa kujitenga na uchafu kama mazungumzo mabaya, habari hasi kutoka kwa watu au vyombo vya habari. Ondokana na imani potofu ambazo zimejijenga kutokana na maisha ya nyuma. Tafuta kwa bidii kuujua ukweli na kuuishi ukweli. Tunza akili yako.
19. Haiwezekani kwa mtu kujifunza kitu ambacho anafikiri tayari anakijua. Wale wanajiona wanajua kila kitu, hua wanabakia kama walivyo, kwao hawana cha kujifunza, maana hupuuzia kila kitu kwa kujifariji kwamba wanakijua. Wanaopenda kujifunza wana kiu ya kutaka kujua, hata kama kitu wanakifahamu wanatamani kukielewa zaidi na zaidi. Na watu hawa hufanikiwa sana. It is Impossible for a man to learn what he thinks he already knows.
20. Kuwa mwenye shukrani. Ukijizoesha kua na mtazamo wa shukrani utakua mwenye furaha. Kabla hujafikiri na kupata vile usivyonavyo, jifunze kushukuru kwanza kwa vile ulivyo navyo, hii itakusaidia kuvutia vile unavyovitaka. Kushukuru pia kunakusaidia kufurahia vile ulivyonavyo, maana unatambua kwamba hivyo ulivyonavyo si kwamba vilikosea njia vikaja kwako, bali kuna aliyekuwezesha kuvipata (Mungu) na kumshukuru kunamfanya atambue unathamini kile alichokupatia kwanza na Una imani kwamba ana uwezo wa kukupatia zaidi. Kuna wakati wana wa Israeli walikosa kua na shukrani, kwa yale Mungu aliyokua amewatendea, wakawa ni watu wa kulalamika kila walipopatwa na shida. Pamoja na miujiza mingi waliyokua wametendewa na Mungu, kila walipokutana na magumu walisahau na kukosa imani kwamba wanaweza kuokolewa tena, wakawa ni watu wakutupa lawama kwa Musa kiongozi wao. Hii ilimfanya Mungu kutaka kuwafutilia mbali wote. Ila Musa akamsihi sana Mungu asifanye hivyo. Kua mwenye shukrani wakati wote.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com