Kama kuna kitu kimoja ambacho kila mmoja wetu anakipigania, basi ni kuwa na maisha bora. Ndio tunahitaji sana kuwa na maisha bora, tunapenda kuona maisha yetu yana maana kwetu na kwa wengine pia. Na tunapenda kuona tuna mchango chanya kwa wengine kupitia maisha yetu.
Pamoja na hitaji hili kubwa la kuwa na maisha bora, bado wengi wetu hatujaujua msingi wa maisha haya bora. Na kwa kutokujua, tumekuwa tukijaribu mambo mbalimbali na hatimaye kuja kugundua ya kwamba hayatupi maisha bora kama ambavyo tulikuwa tunafikiri mwanzo.
Ndio maana kumekuwa na lawama nyingi sana kwa vitu ambavyo hata havikupaswa kulaumiwa. Kwa mfano mtu anafikiri kuwa na fedha nyingi ndio kuwa na maisha bora, na hivyo anajitoa kweli kuzitafuta fedha hizo, anasahau maeneo mengine muhimu kwenye maisha yake, anazipata kweli, lakini anagundua maisha yake bado sio bora kama alivyofikiri. Na hivyo yeye mwenyewe na wanaomzunguka kuishia kulalamika kwamba fedha haileti furaha au maisha bora.
Hapa fedha haina uhusiano wowote, yenyewe imekuja kwa sababu imetafutwa, ila haikuja kumwambia mtu afanye nini. Mtu mwenyewe ndio anayechagua kuwa na maisha bora au kuwa na maisha ya hovyo, iwe ana fedha au hana.
Leo katika makala yetu hii ya FALSAFA MPYA YA MAISHA tutajadili hitaji moja muhimu sana ili kuwa na maisha bora. Kwa kuweza kutimiza hitaji hili, maisha yako yatakuwa bora na kuendelea kuwa bora kadiri siku zinavyokwenda.
Ni hitaji gani ambalo ni muhimu sana?
Mahusiano yetu na watu wengine. Hiki ndio kitu muhimu sana kama tunataka kuwa na maisha bora.
Kila kitu ambacho unakitaka kwenye maisha yako, kinatoka kwa watu wengine. Ubora wa maisha yako unategemea sana mahusiano yako na watu wengine. Kadiri mahusiano yako yanavyokuwa bora, ndivyo maisha yako yanavyokuwa bora pia.
Watu wote wanaokuzunguka ni muhimu sana kwako ili kuweza kuwa na maisha bora. Na hawa wanaanza na wale watu ambao ni wa karibu sana kwako, familia, ndugu jamaa na marafiki. Na baadae wale watu wengine unaokutana nao kwenye shughuli zako. Watu wote hawa wana mchango mkubwa kwako kuwa na maisha bora.
Familia, ndugu, jamaa na marafiki.
Familia ndio msingi wa maisha bora, hakuna mtu anayeweza kufurahia maisha ikiwa hayupo vizuri na familia yake. Kama hakuna maelewano kwenye familia, chochote ambacho unafanya hakitakuwa na maana kubwa. Ni muhimu sana kuweka mahusiano haya ya familia vizuri ili uweze kufurahia maisha.
Ndugu, jamaa na marafiki ni watu muhimu pia kwako. Hawa ni wale watu wanaokujua vizuri na ambao huenda mmetoka mbali kwa pamoja. Hawa pia wana mchango mkubwa sana kwa maisha yako kuwa bora. Mahusiano mazuri na watu hawa yatakupa wewe nafasi ya kufanya mambo yako kwa amani na pia kupata mahali pa kuanzia kama mambo hayatakwenda kama unavyotarajia. Kuwa na marafiki ambao mna mahusiano mazuri, ni sehemu nzuri sana ya kuanzia pale unapoanguka.
Watu unaukutana nao kwenye shughuli zako.
Hawa pia ni watu muhimu sana, kwa sababu kadiri unavyokuwa na mahusiano mazuri nao, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufanya shughuli zako kwa ubora.
Kama umeajiriwa basi kuna watu wengi ambao unakutana nao, kwanza unakutana na mwajiri wako au bosi wako. Huyu ni mtu ambaye yupo juu yako kwenye nafasi hiyo ya ajira, na hivyo unahitaji kujenga naye mahusiano bora ili uweze kufanya kazi yako kwa ubora, lakini sio mahusiano ya woga, kama tutakavyoona hapo chini. Pia kuna wafanyakazi wenzako au wale ambao mpo ngazi sawa, hawa nao wana mchango mzuri sana wa kufanya kazi yako iwe bora, na hivyo unahitaji kuwa na mahusiano mazuri nao. Halafu kuna wafanyakazi ambao wako chini yako, kama wapo. Hawa nao ni watu muhimu sana kwako ili wewe uweze kufanya kazi yako kwa ubora, jenga nao mahusiano mazuri ili kwa pamoja muweze kuwa na kazi bora. Mwisho kabisa kuna wale ambao wanahusika moja kwa moja na kile ambacho unakifanya, kile ambacho unakizalisha. Kama unapata nafasi ya kukutana nao moja kwa moja basi jenga nao mahusiano mazuri sana, hawa pia wana mchango mkubwa kwa wewe kwenda mbele zaidi.
Kama umejiajiri au unafanya biashara, hapa napo mahusiano mazuri yanahusika sana. Na hapa mahusiano yanaanza na mteja wa bidhaa au huduma unayotoa. Kwa dunia ya sasa mteja anaweza kuamua kununua kwako au kununua kwa mwingine. Ushindani ni mkubwa sana na anayepata wateja wengi ni yule aliyejenga mahusiano mazuri na wateja wake. Mahusiano mazuri na wateja wako ndio njia nzuri ya kukuza biashara yako zaidi. Pia unahitaji mahusiano mazuri sana na wale wanaokusaidia kwenye biashara hiyo, kama wapo. Maana hawa ndio wateja wa kwanza kabisa, kwa kuwa na mahusiano nao mazuri watajitoa kufanya kazi bora sana na biashara yako kufanikiwa zaidi. Na mwisho unahitaji mahusiano mazuri na wafanyabiashara wenzako. Kwa kuwa huwezi kuwa unafanya biashara peke yako, unahitaji mahusiano mazuri na wafanyabiashara wenzako, na hapa ndipo unapotakiwa kuachana na ile dhana ya ushindani wa kufa na kupona. Mnaposhirikiana kwa pamoja kama wafanyabiashara, mnazipata fursa nyingi na nzuri zaidi kwa kila mmoja wenu.
Unawezaje kujenga mahusiano bora na wengine?
Njia ni moja tu, kujali kuhusu wengine, hii ndio njia moja ya uhakika ya kujenga mahusiano bora sana na wale wanaokuzunguka. Kujali kuhusu wewe tu, yaani ubinafsi ndio kitu ambacho kimekuwa kinaharibu mahusiano mengi. Pale unapojifikiria wewe mwenyewe tu, unasahau kuhusu wengine na hili linaharibu mahusiano yenu.
Anza kujali kuhusu wengine, kabla hujafanya jambo lolote fikiria ni kwa kiasi gani linawanufaisha wengine. Na kama halina manufaa basi achana nalo, hata kama lina faida kwako. Kwa sababu haina maana kufanya kitu ambacho kina faida kwako halafu kinawaumiza wengine, kwa sababu faida yoyote utakayoipata, huwezi kuilinganisha na mahusiano mazuri uliyoyavunja.
Jiweke kwenye viatu vya wengine, jaribu kuvaa ile hali wanayopitia na jiulize ungependa mtu wa karibu achukue hatua gani, kisha chukua hatua hiyo. Jitahidi kadiri ya uwezo wako kuhakikisha kwamba kile unachofanya kinakuwa na manufaa kwa wengine, na pale ambapo kuna mtu anapitia magumu basi uweze kumsaidia kuyavuka, kadiri unavyoweza.
Kujenga mahusiano mazuri kusikufanye wewe kuwa mtumwa.
Moja ya changamoto ambayo watu wengi wamekuwa wakipitia katika kujenga mahusiano mazuri ni kuishia kuwa watumwa wa wengine. Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba ili wawe na mahusiano mazuri na wengine, ni lazima wawakubalie kila wanachotaka na waishi kaisha yao ili kuwapendeza watu hao. Wanapofanya hivi wanajikuta wanakuwa na maisha mabovu zaidi na watu wale wanazidi kuwataka kukubaliana nao zaidi.
Usiingie kwenye mtego huu, kujenga mahusiano mazuri kusikufanye wewe kuwa mtumwa wa wengine, kukubaliana nao kwa kila kitu au kufanya mambo ili kuwafurahisha hata kama hutaki kufanya mambo hayo.
Katika kujenga mahusiano mazuri, kwanza kabisa kuwa wewe, yaani usijaribu hata kidogo kuigiza ili kukubalika na wengine. Kuwa wewe na simamia kile unachoamini, hata kama kuna wengine hawafurahishi na hilo, kama huvunji sheria na sio kinyume na taratibu za maisha, basi endelea. Na wale ambao ni muhimu sana kwako, ambao ndio unahitaji kujenga nao mahusiano bora zaidi, watakuelewa.
Kwa vyovyote vile unavyochagua kuishi maisha yako jua ya kwamba hutaweza kuwafurahisha watu wote, na hivyo kuliko kuishi kama mtumwa na huku bado kuna wengine hawaridhiki, ni heri kuishi yale maisha yako, na ukawa na wachache ambao wanakuamini kweli na ambao utajenga nao mahusiano bora.
Hakikisha mahusiano yote unayokuwa nayo, yanajengwa kwa ile misingi ambayo wewe unaiamini na sio kujengwa kwa misingi ya woga au kutaka kuwaridhisha wengine. Na pale unapojenga mahusiano kwa misingi ya woga au kuridhisha wengine mahusiano hayo huwa sio bora. Ila unapojenga mahusiano kwa kile unachoamini, yanakuwa mahusiano bora sana.
Kipimo cha mahusiano sio idadi, bali ubora.
Watu wengi wamekuwa wakifirikia kuwa na mahusiano mengi ndio vizuri, yaani kuwa na marafiki wengi, kuwa na ndugu wengi au kuwa na wateja wengi. Lakini unaweza kuwa nao wengi na bado wakawa sio wa karibu sana.
Badala ya kuhesabu mahusiano kwa namba hesabu kwa ubora. Hapa unahesabu ule ukaribu ambao unao na wale ambao una mahusiano nao. Hata kama ni wachache ila wakawa ni watu ambao kweli wako upande wako, mahusiano hayo ni mazuri sana kwako.
Mahusiano yanahitaji uwekezaji.
Mahusiano yoyote bora sio kitu ambacho kinatokea tu, bali ni kitu ambacho kinatengenezwa. Hiki ni kitu ambacho mtu unafanya uwekezaji mkubwa ili kuweza kukitengeneza. Na uwekezaji huu unahitaji muda ndio uweze kuyaona matunda makubwa ya mahusiano uliyotengeneza vizuri.
Hata kwa yale mahusiano ambayo tayari yalikuwepo, kama mahusiano ya kindugu, bado unahitaji kuwekeza ili kuyafanya kuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda.
Ni muhimu sana kujenga mahusiano bora kwa sababu haya ndio yanayotuwezesha kuwa na maisha bora. Mahusiano yote, yale ya karibu na hata ya kikazi/kibiashara ni muhimu sana kwenye maisha yako. kwani mafanikio yako yanategemea mahusiano hayo na kuharibika kwa mahusiano yoyote hapo hupelekea mahusiano mengine yasiwe mazuri.
Anza sasa kuwekeza kwenye mahusiano yako, jali kuhusu wale wanaokuzunguka na hakikisha mahusiano hayo unayajenga kwenye misingi unayoiamini na sio woga au kutaka kukubalika.
Nakutakia kila la kheri katika kujenga mahusiano bora.
MUHIMU; Kwenye semina ya MWAKA 2016 itakayoanza mapema januari, moja ya malengo tutakayojifunza na kuweka ni malengo ya mahusiano. Hapa utapata nafasi ya kuyaangalia mahusiano yako vizuri na kuchukua hatua ya kuyafanya kuwa bora zaidi. Kama utashiriki semina hii na kufanyia kazi yale utakayojifunza, mwaka 2016 utakuwa na mahusiano bora sana na hatimaye kuwa na maisha bora. Kupata maelezo zaidi ya kujiunga na semina hii muhimu fungua hapa; Karibu Kwenye Semina; 2016 NI MWAKA WANGU WA UBORA WA HALI YA JUU.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.