Hakuna mtu ambaye anaamka asubuhi na mara moja tu akawa na mawazo ya kukata tamaa, na kuona mbele hakuwezekani tena.
Hiki sio kitu kinachokuja ghafla kama ajali, bali mtu anakitengeneza mwenyewe.
Na huwa kinaanza na wazo moja hasi, na kwa sababu mawazo hasi yanavutia mawazo mengine hasi, basi unakuja msururu wa mawazo hasi.
Kwa mfano umeweka malengo yako kabisa na kuwa tayari kuyafanyia kazi. Unapoanza kuyafanyia kazi unakutana na changamoto, ambacho ni kitu cha kawaida. Hapa mawazo hasi yanaanza kuja, vipi kama nikishindwa, na wazo hili moja linavutia mawazo mengi sana hasi ambayo yanaunga mkono kwamba lazima utashindwa. Na hapo inafika hatua nguvu zote za kwenda mbele zinaisha na unakata tamaa.
Ili kuondokana na hali hiyo, ili kuhakikisha hufikii kukata tamaa, kuna kitu kimoja muhimu unaweza kufanya.
Kitu hiki ni kutokukubali wazo moja hasi liingie kwenye akili yako. najua huwezi kuyakwepa kabisa mawazo hasi, ila wazo linapokuja usilikaribishe, usiliruhusu lipate nafasi ndani ya akili yako. badala yake liondoshe mara moja.
Na unawezaje kuliondosha mara moja?
1. Kwa kufikiria zaidi kile ambacho utafanikisha kama utaendelea kufanyia kazi malengo yako. kupata ile picha ya mafanikio.
2. Kwa kujifunza kutoka kwa mshauri au washauri wako. Hawa ni wale watu ambao unawakubali sana kwa yale wanayofanya. Hapo unaweza kujiuliza kama angekuwa yeye angefanya nini, na kufanya hivyo.
3. Kwa kusoma makala, vitabu na kusikiliza vitabu ambavyo vitakupa mawazo chanya. Hapa utahamasika zaidi na lile wazo hasi litakosa nafasi ndani yako.
Usikubali wazo moja hasi liingie kwenye akili yako na kupata nafasi, litakaribisha mawazo mengine mengi na hatimaye utashindwa kuendelea na utakata tamaa.
SOMA; Hiki Ni Kitu Kimoja Nakuhakikishia Utakutana Nacho Mara Kwa Mara.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kukata tamaa hakutokei ghafla, bali ni zao la wazo moja hasi, ambalo linavutia mawazo mengine hasi na hatimaye mtu unashindwa kuendelea kabisa. Kuanzia sasa nitakapopata wazo hasi, nitaliondoa mara moja kwa kufikiria mafanikio ninayotaka kufikia, kuangalia washauri wangu na pia kusoma vitabu na makala zitakazonipa mawazo chanya.
NENO LA LEO.
Once you replace negative thoughts with positive ones, you’ll start having positive results.
Willie Nelson
Unapoyabadilisha mawazo hasi kwa kuwa na mawazo chanya, utaanza kuona matokeo chanya kwenye maisha yako.
Unapopata wazo moja hasi, hakikisha unaliondosha haraka kwa kukaribisha mawazo chanya.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.