Kila mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka ni kipindi ambacho watu wengi wanakuwa na mapumziko. Ni wakati ambao watu wengi wanakuwa na sikukuu na pia wengi hufanya sherehe zao katika kipindi hiki. Kutokana na hali hii ya mapumziko na sikukuu, watu wengi huwa kwenye hali ya kufanya manunuzi mengi.
Watu wanakuwa wamefanya kazi mwaka mzima na huu ni wakati mzuri kwao kupumzika. Na katika kupumzika huku kuna mahitaji mengi ambayo wanataka kununua. Msimu wa sikukuu ni kipindi ambacho watu wananunua sana kuliko kipindi kingine. Kwa mfanyabiashara makini huu ni wakati bora sana kwako kuikuza biashara yako.
Leo kupitia makala hii ya KONA YA MJASIRIAMALI tutaangalia ni mambo gani unayoweza kufanya kwenye msimu huu wa sikukuu na ukaiwezesha biashara yako kukua sana. Karibu sana tujifunze mambo hayo na uanze kuyafanyia kazi mara moja kabla msimu huu haujapita.
1. Hakikisha wateja wanajua upo na unafanya nini.
Wateja wana mahitaji yao ambayo wanataka kuyatimiza. Na wengine wana shida zao wanataka kuzitatua. Wateja wanapojua wanapoweza kupata kile wanachotaka, inakuwa rahisi zaidi kukifuata. Kwa hapo biashara yako ilipo, bado kuna watu wengi ambao bado hujawafikia, hivyo unaweza kutumia msimu huu wa sikukuu kuitangaza biashara yako zaidi.
Unaweza kuitangaza biashara yao kwa njia ya matangazo ya vyombo vya habari, kwa matangazo mengine ya kawaida au kwa kuwatumia wateja ulionao sasa, nao wakawaambia wengine wengi zaidi. Hakikisha ujumbe kuhusu biashara yako unasambaa kwa wengi zaidi na kuna baadhi watahitaji kuja kujaribu.
2. Toa ofa kwa wateja wako.
Msimu huu wa sikukuu watu wengi wapo kwenye hali ya kununua. Watu wapo tayari kununua kama watapewa sababu nzuri kwa nini wafanye hivyo. Ni rahisi sana kumshawishi mteja kununua kwako au kununua zaidi kwenye msimu huu wa sikukuu.
Katika msimu huu toa ofa ambayo itamsukuma mteja kununua zaidi. Ofa inaweza kuwa punguzo la bei, au nyongeza kama mtu akinunua kiasi fulani, au kusafirishiwa kwa vitu vinavyohitaji usafiri. Kwa kutoa ofa kwenye msimu huu utawavutia wateja wengi zaidi kwenye biashara yako.
3. Watumie wateja salamu za sikukuu.
Katika msimu huu wa sikukuu ni wakati mzuri sana wa kukumbuka wateja wako wa zamani. Wateja ambao walikuwa wananunua kwako ila kwa sasa hawanunui tena. Katika kipindi hiki unaweza kuwatumia salamu za sikukuu na kupitia salamu hizi wakakukumbuka na huenda wakaja tena kwenye biashara yako.
Unaweza kuwatumia salamu hizi kwa ujumbe wa simu kama una namba zao, barua pepe kama unazo au hata kuwatumia kadi za salamu za sikukuu kama una anwani zao. Kwa wateja wengi utakaowatumia salamu hizi kuna ambao watakuja kwenye biashara yako tena, usiache kutumia fursa hii.
4. Hakikisha vile vitu muhimu vinapatikana.
Katika msimu huu wa sikukuu ni vyema ujue mahitaji makubwa ya wateja wako ni nini, na hakikisha yanapatikana yote. Mara nyingi wateja hupenda kufanya manunuzi yao kwa wakati moja, hivyo wakija kwenye biashara yako na kukuta kuna vitu huna, wanaweza wasinunue hata vile ambavyo unavyo. Hakikisha mteja anapata kila anachotaka, na kwa njia hii utaweza kupata wateja wengi na kukuza biashara yako.
Na ili kuepuka usumbufu ni vyema kujiandaa mapema kabla wakati wa manunuzi haujafikia kilele, maana wakati huo kama utaishiwa na bidhaa inakuwa vigumu kupatikana.
5. Toa huduma bora sana kwa wateja wako.
Kama kuna jambo moja la kusisitiza, basi ni kutoa huduma bora sana kwa wateja wako, hasa kwenye msimu huu wa sikukuu. Hii ni kwa sababu katika msimu huu utapata wateja wengi wapya, na kadiri watakavyopata huduma bora kwa mara ya kwanza, watashawishika kuendelea kuja kwenye biashara yako.
Kwenye msimu huu wa sikukuu wateja wanaweza kuwa wengi sana kiasi cha kushindwa kuwahudumia wote vizuri, lakini wewe usikubali hili, kazana kutoa huduma bora kwa wateja wote, wengi watafurahia hilo na wataendelea kuwa na wewe.
Msimu huu wa sikukuu ni fursa kubwa kwako wewe mfanyabiashara kuikuza biashara yako zaidi. Tumia mbinu hizo tano tulizojifunza kuhakikisha biashara yako inakua zaidi kipindi hiki. Nakutakia kila la kheri na heri ya msimu wa sikukuu.