Ndiyo, dunia inakuhujumu.

Na mambo mengi yanayofanyika hapa duniani, sio kwa faida yako, hasa ya muda mrefu.

Fikiri kila unapopita kuna biashara nyingi sana, na zote zinakusisitiza wewe ununue. Wanatumia kila mbinu kukushawishi ununue, bila ya kujali kama unachonunua ni muhimu kwako au la.

Simu uliyoibeba, nayo imejaa vitu vingi vinavyokuhujumu. Kuna mitandao ya kijamii ambayo inataka sana muda wako, kuna jumbe ambazo kila mara zinakushawishi ufungue na kusoma, bila ya kujali ni muhimu sana kwako, au kile unachoacha kufanya ni muhimu zaidi.

Dunia nzima ni kama imejipanga kukumaliza wewe, kila mtu anakusubiri ukosee ili aweze yeye kunufaika, au uchukue hatua ambayo sio bora sana kwako.

Na rasilimali zako mbili muhimu sana ndio zinawindwa na kila mtu, muda na fedha. Kila mtu anafikiria jinsi ya kuitoa fedha mfukoni mwako, iwe ni kwa jambo muhimu kwako au la. Na wengine wanakazana kupata muda wako, kwa kukuondoa kwenye yale muhimu na kukufanya ufuatilie yasiyo muhimu sana kwako.

Ufanye nini sasa?

Usikubali kuendeshwa na hisia,

Usikubali kuendeshwa na kundi au kulifuata kundi.

Jua ni mambo yapi muhimu sana kwako na yape hayo msisitizo, chochote ambacho sio muhimu sana kinaweza kusubiri.

Wewe kuwa ndio mwamuzi wa mwisho kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, na hakikisha ni kitu muhimu kwako unachokwenda kufanya.

SOMA; Kwa Nini Usimsikilize Anayekwambia HUWEZI….

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba dunia imejipanga kunihujumu, kila mtu ananiwinda, kupata fedha zangu au muda wangu, rasilimali mbili muhimu sana kwangu. Kuanzia sasa nitakuwa mwamuzi wa mwisho wa jinsi gani natumia rasilimali hizi, sitakubali kuendeshwa na hisia au kundi la watu. Bali nitatafakari mwenyewe kabla ya kufanya maamuzi ili kuhakikisha maamuzi ninayofanya ni bora kwangu na sio tu kuwanufaisha wengine.

NENO LA LEO.

Time is the coin of your life. It is the only coin you have, and only you can determine how it will be spent. Be careful lest you let other people spend it for you.

Carl Sandburg

Muda ni sarafu ya maisha yako. ni sarafu pekee uliyonayo, na ni wewe pekee unayeweza kuamua matumizi yake. Kuwa makini vinginevyo utawapa wengine ruhusa ya kuitumia watakavyo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.