Ukiiba fedha huwezi kubaki nazo milele, ipo siku utakamatwa kwa wizi wako na hata usipokamatwa basi utazitumia na zitaisha.

Ukiiba uongozi hutakaa nao milele, iko siku utaondoka kwenye uongozi huo na kama usipoondoka basi utaondolewa kwa nguvu.

Ukiiba watu hutaweza kudumu nao milele, iko siku watu hao watakombolewa na hata wasipokombolewa, watajikomboa wenyewe, ni swala la muda tu.

Kwa njia hii inaonekana hakuna unachoweza kuiba na ukabaki nacho milele, na milele hapa namaanisha mpaka unapokufa. Karibu vyote utakavyoiba, ni labda utakamatwa, au utatumia viishe, au itakubidi ubadili maisha yako sana, labda kukimbia au kujificha ili usijulikane.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho unaweza kukiiba na ukaweza kudumu nacho milele. Na ukifanikiwa kuiba kitu hiki una uhakika wa kuwa na maisha bora na yenye furaha na mafanikio.

Ungependa kujua kitu hiki na jinsi ya kukiiba?

Basi kitu hiko ni maarifa na ujuzi. Unaweza kuiba maarifa ya wengine na ujuzi wao na ukautumia kwa siku zote za maisha yako, bila ya mtu yeyote kukughasi. Na kama utaiba maarifa ambayo ni bora na ukayafanyia kazi basi una uhakika wa kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

Na kwa kifupi tunaweza kusema, kama unataka kufanikiwa basi lazima uweze kuiba maarifa na ujuzi wa wengine. Hiyo ni njia nzuri sana.

Ni muhimu kuiba kwa sababu huna muda wa kufanya mwenyewe ukosee ndio ujue kipi sahihi.

Kama lengo lako ni kuwa na biashara kubwa na yenye mafanikio, kuna watu wengi wameshafanikisha hilo, kuiba maarifa yao na ujuzi wao kutakusaidia wewe kuepuka makosa ambayo yangekuchukua muda mrefu kufika pale.

Kama lengo lako ni kuwa mfanyakazi bora, kuna wengi ambao wameweza kufanya hilo. Kwa kuiba maarifa na ujuzi wao kutakusaidia wewe kufika haraka kwenye lengo lako.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, kuna watu ambao tayari wameshakipata na wamejifunza mengi kwenye njia hiyo ya kukipata, kama ukiweza kuiba kile walichojifunza, itakuchukua muda mfupi zaidi.

Kuanzia sasa kuwa mwizi wa maarifa na ujuzi. Huenda ulishaanza na sasa nakusisitiza uendelee zaidi. Kadiri unavyopata maarifa bora na ujuzi wa hali ya juu ndivyo unavyoongeza nafasi zako za kufanikiwa.

Na uzuri ni kwamba hakuna atakayekufungulia kesi kwa nini umejifunza kupitia yeye. Na uzuri zaidi ni kwamba watu wengi wapo tayari sana wewe ujifunze kupitia wao, na wameandika mpaka vitabu. Ni wewe tu kuchukua hatua na kuanza kuboresha maisha yako.

Achana na kuiba vitu ambavyo hutadumu navyo kwa muda mrefu, karibu tuibe vitu ambavyo tutadumu navyo mpaka pale tutakapoondoka hapa duniani, na wala hakuna atakayetughasi.

Maarifa na ujuzi, kila siku iba vitu hivi kutoka kwa wale ambao wamefika mbali zaidi.

SOMA; SIKU YA 7; Tiba Rahisi Kwa Walioacha Shule, Walioacha Kazi na Walioacha Maisha.

TAMKO LANGU;

Kuanzia leo najitangaza mimi kuwa mwizi wa maarifa na ujuzi wa wengine. Najua wizi huu ndio wizi bora na utaniwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Hakuna atakayenifunga na pia nitadumu na maarifa hayo kwa muda mrefu. Nitaiba maarifa na ujuzi na kuvitumia kusonga mbele zaidi.

NENO LA LEO.

“Knowledge is power. Power to do evil…or power to do good. Power itself is not evil. So knowledge itself is not evil.”
― Veronica Roth

Maarifa ni nguvu. Nguvu ya kufanya mabaya au nguvu ya kufanya mema. Nguvu peke yake sio mbaya. Hivyo maarifa peke yake sio mabaya.

Iba maarifa ya wengine na utakuwa na nguvu ya kubadili na kuboresha maisha yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.