Heri ya mwaka mpya mwana falsafa mwenzangu.

Ni siku nyingi hatujakuwa pamoja hapa kwenye falsafa. Hii ni kwa sababu mwishoni mwa mwaka nilikuwa kwenye likizo ya wiki moja na wiki ya kwanza kabisa ya mwaka huu nilikuwa naandaa semina ya mwaka 2016 ambayo inaendelea kwa njia ya mtandao. Kama umepata nafasi ya kushiriki semina hii nina imani itakuwa sehemu ya wewe kujitengenezea falsafa bora sana na kukuwezesha kuwa na maisha ya furaha na mafanikio.

Katika mwaka huu mpya, sehemu muhimu sana unayohitaji kuifanyia kazi ni ukuaji wako wa kiroho. Tumekuwa tunaweka malengo ya fedha na kazi au biashara, tumekuwa tunaweka malengo ya afya kwa uchache, lakini tumekuwa hatuweki malengo ya ukuaji wa kiroho.

Mwaka huu 2016 tumia falsafa mpya ya maisha kukua kiroho. Ukuaji wa kiroho ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu, kwani huu ndio unaotuwezesha kukabiliana na changamoto za maisha na hata kuweza kuzishinda. Pia ni ukuaji wa kiroho unaotuwezesha kuyafurahia maisha yetu licha ya kuwa hayajakamilika kama tunavyotaka.

Moja ya jukumu kubwa la dini ni ukuaji wa kiroho kwa wewe muumini. Lakini sio dini zote ambazo zinatoa nafasi hii kwa waumini kukua kiroho na hivyo watu kuwa na wakati mgumu wanapokutana na changamoto kwenye maisha yao. Kutokana na kukosa ukuaji wa kiroho watu wengi wamekuwa wakichukua hatua hatarishi kwao pale wanapokutana na changamoto. Wapo ambao wamekuwa wakitumia vilevi kujaribu kuondokana na changamoto hizo, lakini navyo havisaidii badala ya kuleta tatizo jipya la ulevi. Na pia wapo ambao wanakata kabisa tamaa na maisha na kuamua kujiua.

Matatizo karibu yote tunayoyaona kwenye jamii zetu, yanaanzia kwenye matatizo ya kiroho. Watu wengi wamekosa ukuaji wa kiroho na hii imewafanya kuwa na maisha ya hovyo ambayo sio mazuri kwao wala kwa wale ambao wanawazunguka. Chuki, wivu, kusengenya, kulipa kisasi yote haya ni mazao ya ukosefu wa ukuaji wa kiroho.

Katika malengo utakayoweka mwaka huu 2016, ni muhimu kuweka lengo la ukuaji wa kiroho, kwa sababu hili ni muhimu sana kwa wewe kuwa na maisha bora.

Kama dini yako inakusaidia kukua kiroho vizuri sana na endelea kuzingatia yale mafunzo mazuri unayopata yanayokusaidia kukua kiroho. Kama unakosa ukuaji wa kiroho kwenye dini yako basi unaweza kufanya juhudi zako wewe binafsi na kuhakikisha unapata ukuaji wa kiroho.

Hizi hapa ni njia tano za kukuwezesha kukua kiroho bila ya kujali unaamini dini gani. Zifanyie kazi kila siku.

1. Kuwa mtu wa shukrani.

Shukuru kwa kila jambo ambalo linatokea au kuendelea kwenye maisha yako. shukuru kwa maisha uliyonayo, hata kama sio mazuri kama ulivyotarajia, kwa sababu wakati wewe unalalamika huna viatu, kuna mwenzako hana miguu kabisa.

Shukuru kwa watu wazuri ambao unao kwenye maisha yako, watu wanaokupenda na unaowapenda, wanaokujali na wanaokutakia mema. Shukuru kwa kazi au biashara ambayo unayo sasa. Hata kama siyo ile ambayo ulitaka, ni muhimu kushukuru. Kwa sababu popote unapotaka kufika, ni lazima uanzie hapo ulipo sasa.

Unapokuwa mtu wa shukrani maana yake unaacha kulaumu wengine kwa kitu kinachotokea au kutokutokea. Unajua ya kwamba kila kinachotokea kina sababu na kuangalia njia bora ya kunufaika na kitu hiko.

Zoezi hili la shukrani lifanye kila siku, kabla ya kulala au unapoamka. Kwa kushukuru unakaribisha yale yaliyo bora zaidi kwenye maisha yako. pia kunakufanya kuwa chanya zaidi na watu chanya wana maisha ya furaha na mafanikio.

2. Samehe.

Hii ni hatua muhimu sana kwako kukua kiroho. Hata kama mtu alikukosea kiasi gani, hata kama mtu alitaka kukuua ila hakufanikiwa, bado unastahili kumsamehe. Kuna nguvu kubwa sana kwenye kusamehe na unaposamehe unajipa wewe uhuru mkubwa sana.

Unaposhikilia kinyongo kwenye roho yako maana yake unachagua kufungwa na mambo yaliyopita. Unakubali makosa aliyokufanyia matu huko nyuma yaendelee kukurudisha nyuma, yaendelee kukufanya wewe kuwa mtumwa wa makosa hayo.

Samehe kila anayekukosea, na samehe kwa moyo mmoja, achulia na songa mbele na maisha yako. usikubali kabisa maisha yako yavurugwe na makosa ya wengine, wasamehe kwa sababu huenda walifanya makosa hayo bila ya kujua ni kiasi gani yangekuathiri, au hawakuwa na uelewa sawa sawa wa jinsi ya kutatua changamoto walizokuwa wanapitia.

Usifanye mwaka huu kuendelea kuwa mwaka wa vinyongo na visasi, samehe na sahau na songa mbele na maisha yako, huku ukiwa na somo la kuepuka hali kama hizo kutokea baadaye.

3. Tafuta ukweli.

Moja ya changamoto kubwa tunayopitia kwenye dunia ya sasa ni kwamba kila mtu ana maoni yake. Na watu wengi wamekuwa wakichukua maoni wanayopewa na kufikiri ndio ukweli. Lakini ukweli haupo karibu kama wengi tunavyofikiri.

Watu wengi wanapindisha ukweli kwa manufaa yao binafsi. wanakupa maoni ambayo yatakufanya wewe kuchukua hatua ambayo itawanufaisha wao. Mara zote tafuta ukweli, jiulize kila mara kama unachosimamia ni ukweli au maoni tu ya wengine.

Kabla hujafanya maamuzi yoyote makubwa kwenye maisha yako, hakikisha umetafuta na kujua ukweli kwenye jambo hilo. Kushindwa kuujua ukweli utajikuta kwenye changamoto kubwa sana baadaye, maana ukweli huwa hauzikwi, unafichwa tu kwa muda ila baadae utajitokeza wenyewe.

Moja ya njia za wewe kukua kiroho ni kutafuta ukweli, hoji kila kitu, hoji kila unachofanya, hoji kila kinachofanywa na wengine na hoji kila unachoamini. Je kinasimamia ukweli? Au ni maoni tu ya watu ambayo wanataka na wengine wayaamini?

Nakuambia kama utatafuta na kusimamia ukweli, nusu ya matatizo yote kwenye maisha yako utayakwepa.

4. Pata muda wa utulivu, wa kuwa wewe mwenyewe.

Kama kuna changamoto kubwa kwenye dunia ya sasa, basi ni kupata muda binafsi, muda wa kukaa wewe mwenyewe, kuyatafakari maisha yako na kujua ni wapi unatoka, wapi unakwenda, ni wapi unakosea na wapi unafanya vizuri.

Kuna hizi simu zinaitwa smartphone zimetutenga kabisa na maisha yetu binafsi. zimekuwa zikinyonya kila dakika yetu, kwani pale ambapo huna la kufanya unatoa simu na kuanza kubonyeza, mara umeingia wasap, mara facebook, mara instagram, ukimaliza unarudia tena, mpaka muda uliokuwa nao unakwisha kabisa.

Huwezi kukua kiroho kama hupati muda wako binafsi, muda wa kukaa na wewe mwenyewe na kuangalia maisha yako yanakwendaje. Na muda huu hauhitaji kuwa mkubwa, inaweza kuwa dakika tano, kumi, robo saa, nusu saa na hata saa moja. Na hili ni zoezi la kufanya kila siku.

Hakikisha kila siku unatenga muda huu kwako binafsi, hakikisha kwenye muda huu hupati usumbufu wowote, unakuwa mbali na simu na mbali na watu. Katika muda huu sahau kuhusu matatizo au changamoto zinazokusonga kwa sasa na jitafakari wewe binafsi, yatafakari maisha yako kwa kina, yaangalie kama mtu mwingine na ona ni wapi panahitaji marekebisho.

Hata kama unakosa muda kiasi gani, tenga angalau dakika tano tu, na kama huna mazingira mazuri basi anza kwa kuamka asubuhi na mapema na tumia muda huo kutafakari kuhusu maisha yako.

5. Jiandae kwa changamoto.

Jua kabisa ya kwamba jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako ni lazima utakutana na changamoto. Hata kama umejiandaa kiasi gani, bado utakutana na changamoto. Ni vyema ukajua hili mapema na kujiandaa nalo, ili unapokutana na changamoto usikimbilie kukata tama ana kuacha.

Kujua kwamba maisha sio rahisi, maisha yana changamoto zake na kuvuka changamoto hizi ndio kufikia mafanikio makubwa, ni ukuaji mkubwa sana wa kiroho.

Ufanye mwaka 2016 kuwa mwaka wa ukuaji wako wa kiroho, na tutaendelea kushirikishana hili kupitia makala zijazo za FALSAFA MPYA YA MAISHA na hata makala za KURASA ZA MAISHA.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya ukuaji wa kiroho.

TUPO PAMOJA,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz