Kitabu 10X RULE, yaani sheria ya mara kumi ni kitabu ambacho kinaelezea msingi mmoja muhimu sana wa kufikia mafanikio makubwa. Msingi huo ni kuchukua hatua kubwa sana katika kile ambacho unafanya. Mwandishi anaeleza mpango wowote ambao unao sasa kwenye amisha yako, basi uzidishe mara kumi. Na anza kufanyia kazi mara kumi hiyo. Hata kama hutafikia hiyo mara kumi, bado utakachopata kitakuwa kikubwa kuliko ambacho ungepeta kwa kuchukua hatua za kawaida.
Kitabu hiki kimeandikwa na Grant Cardone ambaye anatumia mifano yake binafsi jinsi sheria hii ya mara kumi ilivyomwezesha kuanzia biashara nyingi na kufikia mafanikio makubwa licha ya kuanzia chini kabisa na kutokujulikana na yeyote. Hiki ni kitabu kizuri sana kusoma wakati kama huu ambapo wengi wanaweka malengo, kwani lengo lolote unaloweka sasa unahitaji kulizidisha mara kumi, na kuchukua hatua mara kumi, na fikra zako ziwe mara kumi ya ulivyo sasa. Pale kila kitu kinapokuwa mara kumi, utaona mafanikio makubwa sana.
Karibu tujifunze mambo 20 muhimu kutoka kwneye kitabu hiki.
1. Kitakachokuwezesha wewe kufikia malengo yako na kufikia mafanikio makubwa siyo elimu uliyonayo, si vipaji vyako, sio mtandao ulionao, siyo bahati, siyo fedha. Kuna wengi wana vyote hivi ila bado hawajaweza kufikia mafanikio. Msingi muhimu kabisa wa mafanikio ni MARA KUMI, zidisha malengo na mipango yako mara kumi, hatua unazochukua zidisha mara kumi na fikra ulizonazo zidisha mara kumi. Sheria ya mara kumi ndio tofauti ya uhakika kati ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
2. Ili uweze kufika hatua ya juu zaidi ya hapo ulipo sasa, ni lazima uanze kufikiri tofauti sana na unavyofikiri sasa, na uanze kuchukua hatua kwa utofauti na unavyochukua sasa. Uko hapo ulipo sasa kutokana na fikra ulizonazo na hatua unazochukua. Kama unataka kwenda mbele zaidi ni lazima ubadili vyote viwili.
3. Mafanikio sio kitu ambacho unafikia mara moja halafu umemaliza. Mafanikio ni kitu ambacho unapigania kila siku. Unaweza kuweka juhudi sana na ukafanikiwa, lakini kama utajiona ndio umemaliza kila kitu utaanza kuporomoka kwa kasi sana. Kufikia mafanikio ni hatua moja, kuweza kuendelea kuwa na mafanikio ni hatua nyingine muhimu sana, ambayo inawashinda wengi. Ili ufikie mafanikio ni muhimu kuweka MARA KUMI, na ili uendelee kubaki na mafanikio unahitaji kuendelea kuweka MARA KUMI. Ukiona umefanikiwa na kusahau mara kumi, ni lazima upotee.
4. Ili uweze kuitumia vyema sheria ya MARA KUMI, kwenye maisha yako na kile unachofanya, hitaji moja la msingi sana ni uwe unapenda kile unachofanya, uwe unapenda maisha yako na hivyo kuwa tayari kujitoa zaidi. Kama hupendi unachofanya, sheria ya MARA KUMI itakuwa adhabu kubwa sana kwako, na itakuwa rahisi kukata tamaa hasa pale unapokutana na changamoto. Chagua kitu ambacho unapenda sana kufanya, kisha weka kila kitu ulichonacho, MARA KUMI ya kila mtu anavyoweka juhudi kwenye kile wanachofanya. Kama utakuwa na uvumilivu, hakuna kitakachoweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa.
5. Hakuna mtu ambaye hataki kilicho bora kwenye maisha yake. Kila mmoja wetu anataka kuwa na maisha bora, kuwa na mahusiano bora, kuwa na afya bora, kuwa na maarifa zaidi na kuwa na mchango chanya kwenye jamii inayomzunguka. Lakini ni wachache sana wanaochukua hatua stahiki za kufikia ubora huo, wengi hawapo tayari kujitoa na ni kwa sababu hawapo tayari kuweka juhudi mara kumi ya walivyozoea kuweka.
6. Sababu moja kubwa kwa nini watu wengi wanashindwa kufikia malengo yao na kushindwa kufanikiwa ni kushindwa kuweka juhudi zinazohitajika. Wengi hawapo tayari kujitoa kweli na kuweka juhudi mara kumi ya vile walivyozoea kuweka na hatimaye biashara zinakufa, afya zinazorota, mahusiano yanavunjika na fedha zinapotea. Chochote unachotaka kwenye maisha yako, zidisha mara kumi, halafu chukua hatua mara kumi zaidi, huku ukifikiri mara kumi zaidi.
7. SHERIA YA MARA KUMI ni sheria ya utawala, ni sheria ambayo inakuweka wewe mbali sana na wengine, inakuweka wewe juu sana kiasi kwamba hakuna hata anayefikiria kushindana na wewe. Hufanyi kabisa kile ambacho kila mtu anafanya, na hata wengine wanapokuangalia kwa kile unachofanya, wanaona hakiwezekani kwao kufanya. Hufanyi hivi kwa sababu unataka kuwaonesha wengine unaweza zaidi yao, bali kwa sababu una shauku kubwa ya kupata kile unachotaka kiasi kwamba hutaki chochote kikuzuie.
8. Pale ambapo watu wanashindwa kutumia sheria hii ya MARA KUMI, au wanapojaribu na wakashindwa, basi huishia kunasa kwenye mtego wa NJIA YA KUTAJIRIKA HARAKA. Mtego huu umepoteza wengi ambao hawajui kwamba hakuna njia ya haraka ya kufikia utajiri au mafanikio. Njia ya uhakika ni kuweka juhudi kubwa sana, ambazo hujawahi kuweka hapo awali, na kufikiri kwa utofauti mkubwa na ulivyokuwa unafikiri hapo awali. Na kujitoa kweli kiasi kwamba hakuna chochote kinachoweza kukuzuia. Mtego wa njia ya kutajirika haraka umewafanya wengi sana kutapeliwa.
9. Lengo lolote utakalojiwekea kwenye maisha yako, litakuwa gumu kufikia, utakutana na changamoto ambazo zinaweza kukukatisha tamaa. Sasa kwa nini usiweke malengo yako juu zaidi ya unavyoyaweka sasa? Lengo lolote unaloweka sasa litahitaji juhudi, nguvu na uvumilivu ili kufikia. Sasa kwa nini usifanye lengo hilo mara kumi na ukaweka juhudi na nguvu mara kumi? Ni MARA KUMI pekee ndio unaweza kujua uwezo mkubwa ulio ndani yako. huenda mpaka sasa hujajua uwezo huu mkubwa kwa sababu hujapata nafasi ya kujisukuma zaidi. Anza kujisukuma sasa kw akuweka malengo yako mara kumi.
10. Hata iwe una mpango mzuri kiasi gani wa biashara, hata uwe na bidhaa bora kiasi gani, bado katika mipango yako kuna vitu ambavyo hutakadiria sawa. Huenda utafikiri unahitaji mtaji kiasi fulani ukakuta unahitaji zaidi. Au ulifikiri itakuchukua muda fulani kuanza kufurahia faida lakini ikachukua muda mrefu zaidi. Na hapo bado kuna mabadiliko yatakayotokea ambayo yatakuwa nje ya uwezo wako, mabadiliko ya kisheria, mabadiliko ya kiuchumi na mengine mengi. Hivyo kuweka mipango ya kawaida ni lazima kutakuingiza kwenye matatizo makubwa. Njia ya uhakika ya kuepuka hili ni kuweka malengo na mipango yako MARA KUMI ya unavyoweka sasa, kwa njia hii chochote ambacho kitatokea hakiwezi kukuathiri kwa njia yoyote ile.
11. Unapoweka makadirio ya chini ya muda, nguvu, na juhudi unazohitaji kuweka ili kupata kitu fulani, ni rahisi sana kukata tamaa na kuacha pale unapoona haiwezekani tena kupata kile ulichokuwa unataka kwa mipango yako ya mwanzo. Ndio maana ni muhimu sana kwako kutumia sheria ya mara kumi, kwani hapa kila kitu utakizidisha mara kumi na huwezi kuangushwa kwa makadirio ya chini.
12. Fanya chochote unavyofanya kama vile kila tendo lako linarekodiwa na kamera na kuna watu anaangalia vile unavyofanya. Fikiria kama unarekodiwa na watoto na wajukuu zako wataoneshwa jinsi ulivyokuwa unafanya mambo yako, kila siku na kila mahali. Kwa njia hii utalazimika kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana, hutapoteza muda na wala hutafanya mambo ambayo sio muhimu kwako. Hapa utaweka juhudi mara kumi na kwa hakika utafikia chochote unachotaka kufikia.
13. Unapoweka malengo na ukaona huwezi kuyafikia kadiri muda unavyokwenda, kosa baya kabisa unaloweza kufanya kwenye maisha yako ni kupunguza malengo hayo. Hapa utakuwa umejimaliza kabisa, na itakuwa vigumu sana kwako kuweka juhudi wakati mwingine. Kama umeweka malengo na unaona huwezi kuyafikia, unachohitaji kufanya ni kuanza kufikiri mara kumi zaidi na kuweka juhudi mara kumi zaidi.
14. Mafanikio yoyote utakayofikia kwenye maisha yako, hayakufaidishi wewe tu, bali yanawafaidisha wale wote ambao wanakuzunguka. Utafanya vitu ambavyo vina msaada kwa wengine na hivyo kuwawezesha kuwa na maisha bora. Na pia kuweza kwako kutakuwa hamasa kwa wengine kwamba inawezekana. Hivyo ni muhimu sana wewe kufanikiwa, na tumia sheria ya MARA KUMI, itakuhakikishia mafanikio.
15. Mtu yeyote anayelaumu wengine au chochote kuwa ndio sababu ya wao kutofanikiwa au kutopata kitu fulani, kamwe hawawezi kufanikiwa kwenye maisha yao, na badala yake wataendelea kuwa watumwa kwenye dunia hii. Unapolaumu wengine maana yake umewapa mamlaka ya maisha yako, na hivyo wewe unakuwa mtumwa wao, na unakosa kabisa nguvu ya kuchukua hatua. Kama unajiona wewe ni mtu ambaye umekuwa unaonewa, unaweza tu kusahau kitu kinachoitwa mafanikio. Mafanikio hayaendi kwa watu laini, ni lazima uchukue hatamu ya maisha yako, ujue chochote kinachotokea kwenye maisha yako ni juu yako, kama kuna ambacho hujapata ni uzembe wako binafsi. Na anza kuweka juhudi kubwa kupata chochote unachotaka.
16. Ili kufikia mafanikio makubwa, ni lazima uamue kumiliki maisha yako kabisa. Amua kwamba chochote kinachotokea kwenye maisha yako ni wewe umesababisha. Kama umepata hasara kwenye biashara ni wewe umesababisha, hata kama kuna mtu kaiba, ona kwamba hukuwa makini kiasi cha kutosha, na amua kuchukua hatua kurekebisha chochote ambacho kimetokea. Lakini kama wewe utasema umepata hasara kwa sababu mfanyakazi wako hakuwa makini, unajidanganya, wewe ndio hukuwa makini, ni nani aliyeajiri mfanyakazi huyo?
17. Katika maisha kuna aina nne za kuchukua hatua linapokuja swala la mafanikio. Aina ya kwanza ni kutokuchukua hatua kabisa, hapa mtu hafanyi chochote kikubwa kwenye maisha yake, mtu anajua anachotaka, lakini hachukui hatua ya kuweza kukifikia, na hivyo anaishia kushindwa kukipata.
18. Aina ya pili ya kuchukua hatua ni kuchukua hatua kinyume, yaani kukimbia. Hapa ni pale ambapo mtu badala ya kukabiliana na hali ngumu anayokutana nayo, ambayo kama akiivuka atafikia mafanikio makubwa, yeye anaikimbia. Hapa mtu hawezi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
19. Aina ya tatu ya kuchukua hatua ni kuchukua hatua za kawaida. Hapa ni kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kujituma na kukazana kufanya kwa kiwango cha chini sana ambacho hakitakuumiza. Hapa ni pagumu zaidi kufikia mafanikio kwa sababu mara nyingi mtu anakuwa ameridhika na kawaida, ila anapokutana na changamoto ndiyo anaona kumbe mambo sio rahisi.
20. Aina ya nne ya kuchukua hatua ni kuchukua hatua kubwa sana, hapa ndipo unapochukua hatua MARA KUMI ya watu wengine wanavyochukua, au ulivyokuwa unachukua hapo awali. Na katika kuchukua hatua hizi kubwa unatengeneza matatizo makubwa pia. Hapa unahitaji kufanya vitu ambavyo umekuwa unahofia kufanya, kuenda maeneo ambayo hujawahi kufikiri unaweza kwenda. Na hii ndio inayoleta mafanikio makubwa.
Mwandishi anasema kama unaona haya ni makubwa sana kwako kuweza kufanya, kama unaona ni kiu ya mafanikio iliyopitiliza, kama unaona ni tamaa ya mafanikio, basi jua mafanikio hayawezi kukutana na wewe. Kupata tu hilo wazo kwamba hii ni zaidi ni dalili tosha kwamba hujajitoa kwa ajili ya mafanikio.
Nina hakika wewe rafiki yangu umejitoa kweli kwa ajili ya kufikia mafanikio, kwa kufanya yale ambayo yatawasaidia wengine pia. Ongeza sheria hii ya MARA KUMI katika sanduku lako la vifaa vya mafanikio na nina hakika itakusaidia sana.
TUPO PAMOJA.