Mbinu za kuongeza ufanisi wako kwenye biashara ili kuongeza faida.

Kitu kimoja kizuri sana kuhusu biashara ambacho wengine hawakipati ni kwamba unapofanya mabadiliko ya juhudi unazoweka kwenye biashara, unaweza kuona athari ya mabadiliko hayo haraka sana kwenye faida ya biashara. Kama utaanza kuzembea haitachukua muda utaanza kuona faida ikishuka na biashara kuingia kwenye matatizo mengi. Na kama utaanza kuongeza juhudi utaona biashara inakua na faida kuongezeka.
Kipimo kizuri sana cha juhudi unazoweka kwenye biashara yako ni ufanisi wako. Haijalishi ni juhudi kiasi gani unaweka, kama hazileti matokeo chanya kwenye biashara, hazina maana kwenye biashara yako. hivyo kabla ya kusema wewe unaweka juhudi sana lakini huoni mafanikio, ni vyema ukajiuliza kama juhudi unazoweka zina ufanisi mzuri kwenye biashara yako. 

 
Juhudi zako zinazalisha ufanisi mzuri pale ambapo unafanya yale muhimu sana kwa biashara yako na kuacha kupoteza muda. Pia kutumia vizuri muda unaoupata kuhakikisha unafanya yale majukumu muhimu ya biashara yako.
Changamoto kubwa sana ambayo kwa sasa tunapitia ni ukosefu wa muda. Muda unaonekana kuwa mdogo sana kuliko majukumu tunayotaka kutekeleza, na kadiri siku zinavyokwenda ndivyo majukumu yanavyoongezeka na muda ni ule ule. Hivyo bila ya kuwa na mbinu nzuri utajikuta unakimbizana na muda bila ya kuweza kuzalisha kitu chenye faida kwenye biashara yako.
Mbinu muhimu kabisa ya kuongeza ufanisi wako kwenye biashara yako ni kuweza kumiliki muda wako. Inaweza kuonekana rahisi kusema lakini ni kitu ambacho kigumu na chenye changamoto kubwa sana, hasa kwa dunia ya sasa ambayo ina changamoto nyingi. Wewe kama mfanyabiashara unahitaji sana kuwa na nidhamu ya muda, na nidhamu hii utaipata pale ambapo utaweza kuumiliki muda wako.
Umiliki wa muda wako unaanza pale ambapo unajua ni yapi majukumu muhimu sana kwenye biashara yako, ambayo wewe tu ndio unaweza kuyafanya kwa ufanisi mkubwa. Ndio, kuna majukumu mengi kwenye biashara yako, lakini kuna ambayo wengine wanaweza kufanya. Ni vyema ukayaepuka hayo na kuchagua yale ambayo wewe tu ndio unaweza kuyafanya vizuri.
Ukishayajua majukumu haya muhimu sana kwako, yapangie ratiba ni wakati gani wa siku unayafanya. Na mpango huu unaufanya mapema sana kabla ya kuianza siku, au kabla ya kulala usiku, kupangilia ya siku inayofuata. Kwa kuwa na ratiba ambayo imeandikwa itakuwa rahisi kwako kuifuata.
Baada ya kujua ratiba yako ya siku ni nini unatakiwa kufanya, ianze siku yako kwa kufanya yale majukumu ambayo ni makubwa na magumu. Hapa ndipo penye changamoto kubwa sana, kwa sababu majukumu haya makubwa na muhimu huwa yanatisha na ni rahisi sana kuahirisha na kujiahidi utafanya baadae. Lakini ukishaahirisha na kuianza siku kwa majukumu ambayo sio muhimu sana, hutakuja kurudi tena kwenye majukumu yale ambayo ni makubwa na muhimu.
Jijengee utaratibu wa kwamba kitu cha kwanza kabisa kwenye siku yako ni kutekeleza yale majukumu ambayo ni makubwa na muhimu sana. Na katika wakati huu ambapo unayafanya usikubali usumbufu mwingine wowote. Muda huu utenge na ulinde sana usije ukapotea. Hakikisha hauanzi siku yako kwa kufuatilia mambo ya kwenye mitandao, au kufanya mawasiliano ambayo sio muhimu. Kwa sababu ni rahisi kuanza vitu hivi lakini ni vigumu sana kuacha, na unapoacha unajikuta huna tena nguvu ya kuendelea na majukumu mengine muhimu.
Mwanzo wa siku, yaani asubuhi ni wakati mzuri sana wa kutekeleza majukumu makubwa na muhimu. Hii ni kwa sababu kwa watu wengi asubuhi bado wanakuwa na nguvu na akili zinafanya kazi bila ya uchovu. Lakini kadiri siku inavyokwenda nguvu inapungua na akili inachoka. Ndio maana mwisho wa siku unakuwa umechoka sana na huwezi kufanya maamuzi makuba kwa usahihi.
Mbinu bora kabisa ya kuongeza ufanisi wako kwenye biashara yako, ni kujua yale majukumu muhimu sana ambayo wewe tu ndiye unayeweza kuyafanya, na kuyafanya asubuhi na mapema kabla ya kuendelea na majukumu mengine ambayo sio makubwa sana na pia sio muhimu sana.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: