Kama unataka kujua watu wanaopoteza muda kwenye maisha yao, wakidhani ya kwamba wanaokoa muda, ni watu ambao wanataka kufanya vitu viwili, kwa wakati mmoja na wanavifanyia sehemu moja. Ni rahisi sana ukifikiria juu juu kwamba unaokoa muda. Lakini ukweli ni kwamba unapoteza muda mwingi sana.
Akili yako ina uwezo mkubwa sana wa kufanya kitu chochote, lakini kama akili hii itapewa uwezo w akuweza kufikiri na kufanya kitu kimoja kwa wakati. Hapa akili hii inapeleka rasilimali zote muhimu katika kushughulikia tatizo lililopo mbele yako na kuhakikisha unapata ufumbuzi.
Hapo ni kufanya kitu kimoja kwa wakati, unatumia muda mchache na unafanya kwa usahihi, tofauti na kama ungefanya zaidi ya kitu kimoja kwa wakati. Pale akili yako inapokazana kuhamisha mawazo kutoka kwenye kitu kimoja kwenda kwenye kingine, unapoteza muda mwingi sana. Ni bora zaidi kufanya kila kimoja kwa wakati wake.
UPANDE WA PILI.
Vitu viwili vinavyopingana, sehemu moja kwa wakati mmoja.
Huwezi kuwa mtu mwema na mtu asiye mwema kwa wakati mmoja. Huwezi kuwa na imani mbili zinazopinga na kwa wakati mmoja. Ni lazima kwa wakati fulani utakuwa kwenye hali fulani moja kati ya hizo mbili. Usijidanganye kwamba uko kati kati, maana hapo hakuna chochote unachopata zaidi ya kupoteza muda.
Chagua kuwa upande mmoja, na amua huo uwe upande wako. Kama unapenda kuwa mwema basi hakikisha kila unachokifanya unakifanya kwa misingi ya wema. Usijidanganye kwamba kuna wakati unaweza kuwa mwema na pia usiwe mwema.
Chagua upande mmoja katika pande mbili za maisha, na fanya upande huo ndio utambuliwe nao.
Na fanya jambo moja kwa wakati, utaokoa muda na kuongeza ufanisi.
TAMKO LANGU;
Nimejifunza ya kwamba naweza kufanya kitu kimoja kwa ufanisi kwa wakati husika. Na pia nahitaji kuchagua upande mmoja wa kuwepo kwenye pande mbili za kila jambo. Siwezi kufanya vitu tofauti kwa wakati mmoja na siwezi kuwa kwenye pande zote mbili za wakati mmoja. Kung’ang’ania zaidi ya kimoja ni kupoteza muda wangu na kupunguza ufanisi wangu. Kuanzia sasa nitakwenda na moja.
NENO LA LEO.
“Do one thing at a Time, and while doing it put your whole Soul into it to the exclusion of all else.”
― Swami Vivekananda
Fanya kitu kimoja tu kwa wakati, na wakati unakifanya, weka moyo wako wote kwenye kitu hiko na sahau vingine vyote.
Unaweza kufanya jambo moja kwa ufanisi ndani ya wakati, unaweza kuchagua kuwa upande mmoja pekee, using’ang’anie vingi, utapoteza muda na ufanisi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.