Kitabu Cha Kujisomea Januari 2016; THE 10X RULE (Sheria Ya Mara Kumi), Tofauti Pekee Kati Ya Kufanikiwa Na Kushindwa.

Karibu tena mpenzi msomaji katika utaratibu wetu mzuri wa kushirikishana vitabu vya kusoma kila mwezi. Kupitia utaratibu huu kila mwezi umekuwa unatumiwa kitabu kimoja cha kujisomea. Kwa mwaka jana 2015, kila mwezi ulitumiwa kitabu cha kujisomea. Kama ulisoma vitabu vyote, na kufanyia kazi yale uliyojifunza, nina hakika maisha yako hayapo kama yalivyokuwa mwanzo. Kuna mabadiliko ambayo utakuwa umeanza kuyaona kwenye maisha yako, hata kama ni madogo kiasi gani.
Mwaka huu 2016 tunaanza na kitabu kizuri sana kinachoitwa THE 10X RULE, yaani sheria ya mara kumi. Kitabu hiki kimeandikwa na mwandishi Grant Cardone. Nikiri kwamba kabla ya kusoma kitabu hiki nilikuwa naweka malengo, lakini nilikuwa siweki makubwa ipasavyo. Kwa kusoma kitabu hiki kumenifungua na kunionesha kwamba huenda nilikuwa nazuia uwezo mkubwa uliopo ndani yangu.

 
Kitabu hiki kimegusia kwa kina sana swala la kuweka malengo na kuyafanyia kazi, ili kuweza kupata kile ambacho mtu unakitaka kwenye maisha yako.
Na msingi mkuu ambao mwandishi anatupatia kwenye kitabu hiki ni kwamba malengo yoyote unayotaka kufikia utakuwa na uhakika wa kufikia kama utazidisha mara kumi. Na ukishazidisha malengo hayo mara kumi unahitaji kuanza kufikiria mara kumi zaidi ya unavyofikiri sasa na hata unapochukua hatua unahitaji kuchukua hatua mara kumi ya unavyochukua sasa.
SOMA; KITABU CHA SEPTEMBA; Guide To Investing(Muongozo Wa Uwekezaji).
Kwa mfano kama lengo lako ni kutengeneza milioni 10 kwa mwaka huu 2016, unahitaji kuweka lengo lako liwe kutengeneza milioni 100 kwa mwaka huu 2016. Na chochote ambacho ulikuwa umepanga kufanya ili kupata kiasi hiko cha fedha basi zidisha mara kumi, na hata unavyofikiri, fikiri mara kumi zaidi. Kama unataka kupata wateja watano wa kununua kile unachotoa, jiulize unawezaje kupata wateja 50, na ongea na watu 50 na kati ya hao hutakosa watano na zaidi.
Haya hapa ni baadhi ya mambo ambayo mwandishi ameyaeleza kwa kina sana ndani ya kitabu hiki.
Mwandishi ameeleza maana halisi ya mafanikio kwako na kukuonesha kwa nini mafanikio ni wajibu wako. Ndio mafanikio ni wajibu wako wewe binafsi, sio bahati wala kupendelewa, bali ni wajibu wako na unahitaji kufanyia kazi ili kuyapata.
Mwandishi pia amevunja ile dhana potofu kwamba mafanikio yapo kwa uhaba, kwamba kuna wachache ambao wamepangiwa kufanikiwa na wengine wataendelea kushindwa tu hata wafanye nini. Mwandishi anakuonesha ni jinsi gani mafanikio yako mengi ya kumtosha kila mtu. Ni mtu tu aamue kuchukua hatua na kujipatia mafanikio yake.
Mwandishi anaeleza ni jinsi gani kuweka malengo ya kawaida kulivyo sumu ya mafanikio. Watu wengi sana wameshindwa kufikia maisha ya mafanikio waliyokuwa wanatarajia kutokana na kuwa kawaida, kufanya kawaida na kuweka malengo ya kawaida. Kama kuna kitu chochote unakifanya kwa kawaida kwenye maisha yako, tayari umeshashindwa.
SOMA; KITABU CHA JULY; THE SECRET CODE OF SUCCESS(Siri Ya Mbinu Ya Mafanikio)
Mwandishi pia ametoa mbinu bora sana ya wewe kuwa bora bila ya kushindana. Kwanza kabisa mwandishi atakuonesha kwa nini kushindana na wengine ni kujichimbia kaburi lako mwenyewe. Halafu anakuonesha ni njia ipi nzuri ya wewe kuwa bora bila ya kushindana. Kwa kifupi mwandishi anakutoa kwenye kushindana na kukupeleka kwenye KUTAWALA.
Mwandishi anakuongoza bega ka bega katika kuweka malengo yako kwa sheria ya 10X RULE, yaani malengo uliyonayo kuyafanya mara kumi. Na pia anakutoa hofu kwa mawazo uliyonayo kwamba kama utaweka malengo yako mara kumi na ukashindwa kuyafikia si itakukatisha tamaa sana? Mwandishi anakuambia haitakukatisha tamaa kwa sababu hata kama hutafikia hiyo mara 10, bado utapata kikubwa kuliko unachopata sasa, na hii itakupa moyo zaidi.
Nisimalize utamu wote wa kitabu hiki kizuri hapa, bali nikupe wewe nafasi ya kujisomea kitabu hiki mwenyewe. Hiki ni kitabu kizuri sana sana sana, na ni kitabu kizuri zaidi kwenye mwanzo huu wa mwaka. Nakushauri na kukusihi sana wewe rafiki yangu, hata kama huna mpango wa kusoma kitabu chochote kwa mwaka huu 2016, basi soma kitabu hiki kimoja pekee.
Kisome na chukua yale mazuri, yafanyie kazi na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Nikusisitize tena, soma kitabu hiki rafiki yangu, ni kitabu kizuri sana na hakitakuacha kama ulivyo sasa, hata kama upo kwenye hali ya chini sana au ya juu sana.
Kupata kitabu hiki bonyeza maandishi haya ya kitabu THE 10X RULE na utakipakua kitabu hiki bure kabisa kwa na uweze kujisomea.
Nakutakia kila la kheri kwenye kufikia malengo yako makubwa uliyoweka na unayokwenda kuweka kwa mwaka huu 2016. Nina hakika utakwenda kuyafikia kwa kiasi kikubwa sana.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: