Sayansi kidogo leo, ila lengo letu kubwa ni kujifunza, na kuondoka hapa na kitu cha kufanyia kazi kwenye maisha yetu, ili yapate kuwa bora zaidi.
Kila mmoja wetu anajua ya kwamba dunia inalizunguka jua, hii ni sayansi ya darasa la sita kama unakumbuka. Na maisha yanawezekana hapa duniani kwa sababu ya umbali ambao dunia ipo kutoka kwenye jua, sayari nyingine ziko mbali zaidi kutoka kwenye jua na hivyo kuwa baridi sana, na nyingine ziko karibu sana na dunia na hivyo kuwa na joto sana. Lakini dunia ipo kwenye eneo sahihi la kuwezesha maisha kuendelea.

Kinachofanya dunia izunguke jua, ni nguvu ya mvutano iliyopo kati ya dunia na jua. Lakini pia dunia ina nguvu za mvutano na sayari nyingine zilizopo kwenye mfumo wetu huu wa jua. Lakini pamoja na nguvu hizi nyingine nyingi za mvutano, bado dunia imeendelea kuwepo kwenye eneo lake muhimu.
Hili ndio somo ambalo nataka tuondoke nalo hapa, dunia imeweza kuwepo mpaka leo kwa sababu imekuwa na adabu. Imejua ni kipi muhimu sana ambacho kwa dunia ni kukaa kwenye umbali wake ule ule kutoka kwenye jua, ndio maana imeendelea kuwepo. Sayari zote ambazo zinashindwa kutii hili zinavunjika vunjika na kupotea kabisa, na ndio tunaziona kama vimondo.
Dunia haichanganywi na nguvu nyingine za mvutano, bali inajua ni mvutano upi ni muhimu zaidi kwa yenyewe kuendelea kuwepo na inauheshimu mvutano huu, ina adabu kwenye hilo na ndio maana mpaka leo imeweza kuwepo.
Maisha yako pia yanahitaji adabu kubwa sana kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. kuna nguvu nyingi sana zitakuvuta, kuna vitu vingi vitakuvutia kufanya, lakini kama utavipa uzito sawa, ni lazima utapotea. Ni lazima ujue kipi ni muhimu zaidi kwako, ambacho kitakufanya wewe uwe na maisha bora na yenye mafanikio kisha weka nguvu zako zote pale.
Kuwa na dabu, kuwa na nidhamu ukishajua kile ambacho ni muhimu sana kwako, na usikubali mtu yeyote akutoe kwenye kitu hiko. Tangaza vita kabisa na wewe mwenyewe, ya kwamba utang’ang’ana na kitu hiko kwa sababu hapo ndipo mafanikio yako yalipo. Dunia imeweza, na wewe utaweza, ni swala la wewe kuanza kufanyia kazi.
SOMA; Uhusiano Wa Nidhamu Binafsi Na Mafanikio Makubwa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kinachoiwezesha dunia kuwepo mpaka sasa ni adabu na nidhamu ya kujua ni nguvu ipi muhimu na kuifuata. Licha ya kuwepo kwa nguvu za mvutano nyingi, dunia inajua nguvu muhimu ni lazima ipewe kipaumbele. Na mimi pia nimejua ni kitu gani muhimu zaidi kwangu na nitaweka nguvu zangu kwenye kitu hiko. Sitakubali kabisa vitu vingine vinavyoonekana ni vizuri ila sio muhimu sana kwangu kuchukua muda wangu mzuri.
NENO LA LEO.
With faith, discipline and selfless devotion to duty, there is nothing worthwhile that you cannot achieve.
Muhammad Ali Jinnah
Kwa imani, nidhamu na kujitoa kweli kwa kile unachofanya, hakuna kitu cha thamani utakachoshindwa kupata/kufikia.
Jua ni kipi muhimu sana kwako, jitoe kukifanyia akzi na weka nidhamu na adabu ya hali ya juu sana, kama dunia inavyozunguka jua kwa nidhamu na adabu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.