Maisha ni darasa ambapo kila siku tunajifunza mambo mbalimbali. Tunajifunza ni njia zipi bora za kuishi, mambo gani tuwekee mkazo, na mambo gani tuyaepuke kwenye maisha yetu.

Tofauti na madarasa mengine ya kwenye mfumo wa elimu, ambapo unafundishwa kwanza halafu mtihani ndio unakuja, kwenye maisha unapata mtihani kwanza halafu somo ndio linakuja.

Unakutana na changamoto kwanza halafu ndio unakaa chini na kutafakari changamoto ile. Imekuwaje ikatokea, umechangiaje kwa changamoto hiyo, umejifunza nini kwenye hiyo changamoto na ufanye nini ili isijirudie kwenye maisha yako.

Hivi ndivyo tunavyojifunza kila kitu tangu tukiwa wadogo. Ulipokuwa mdogo na hukuwa na uelewa, ulishika moto ukaungua na kujifunza kwamba moto huwa haushikwi na mikono mitupu, na kadiri unavyokwenda, kila changamoto unayopitia ni somo kubwa na muhimu kwenye maisha yako.

Swali ni je vipi kama hujaelewa somo?

Jibu ni kwamba utaendelea kupata mtihani mpaka pale utakapolielewa somo. Kwenye mfumo wa elimu ukifeli mtihani unaweza kurudia kusoma tena kisha ukafanya tena mtihani. Kwenye darasa la maisha, kama hujaelewa somo, mtihani unajirudia tena na utaendelea kujirudia mpaka pale utakapolielewa somo.

Kama unapata hasara kwenye biashara, utaendelea kupata mpaka pale utakapojifunza ni kitu gani kinaleta hasara kwenye maisha yako.

Kama umefukuzwa kazi moja na kwenda nyingine, utaendelea kufukuzwa kazi hiyo nyingine na nyingine pia kama hutaelewa somo la kufukuzwa kazi ya kwanza.

Kama mahusiano yako yamevunjika, au ndoa yako imevunjika, utaendelea kuvunja ndoa na mahusiano mengine utakayoingia mpaka pale utakapolielewa somo linalokuja na mahusiano yako kuvunjika.

Kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha yako haiji tu kwa bahati mbaya, bali inakuja na somo muhimu sana kuhusu maisha yako. kama hutatafuta somo hili na ulielewe, utaendelea kukutana na changamoto hiyo mara kwa mara.

Kila unapokutana na changamoto, usiishie tu kulalamika, usiishie tu kusema kwa nini mimi, bali itafakari kwa kina na jiulize ni somo gani unaloondoka nalo kwenye changamoto hiyo. Ni kwa namna gani ufanye baadae ili changamoto kama hiyo isijitokeze tena.

Na ukishalielewa somo moja sio kwamba darasa limeisha, bali unajiandaa kwa darasa kubwa zaidi, yaani changamoto kubwa zaidi. Usiogope unapokutana na changamoto hizi, jua ni sehemu muhimu ya ukuaji wako kwenye maisha.

SOMA; Umuhimu wa changamoto kwenye maisha yako.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba maisha ni darasa, na kila changamoto ninayopitia ni somo muhimu sana kwenye maisha yako. na kama sitajifunza na kuelewa somo hilo, litaendelea kujirudia tena na tena na tena mpaka pale nitakapolielewa. Kuanzia sasa nitahakikisha changamoto yoyote ninayoipitia naichunguza kwa kina ili nione ni somo gani naondoka nalo kwenye changamoto hiyo.

NENO LA LEO.

“Life is a classroom. Only those who are willing to be lifelong learners will move to the head of the class.”

— Zig Ziglar

Maisha ni darasa. Wale pekee ambao wapo tayari kuwa wanafunzi wa kudumu wa maisha, ndio watakaokuwa mbele kwenye darasa hili.

Kila changamoto unayopitia kwenye maisha yako ni somo muhimu unalotakiwa kujifunza. Usipojifunza utaendelea kukutana na changamoto hiyo mpaka utakapojifunza.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.