Katika safari yetu hii ya kuhakikisha maisha yetu yanakuwa bora sana kila siku, tumezungukwa na mitego mingi sana. Bila ya kuwa makini ni rahisi sana kunasa kwenye mitego hii, ukifikiri unafanya maamuzi sahihi kumbe unajipoteza wewe mwenyewe.
Kama ambavyo mpaka sasa wote tunajua, safari hii sio rahisi, ina changamoto na vikwazo vingi. Na katika changamoto hizi ndipo mitego inapokaa, na ndio maana wengi wananasa kirahisi sana.
Baadhi ya mitego unayotakiwa kuijua haraka na kuikwepa ni hii;
1. Wakati mambo yanakuwa magumu, kutafuta njia rahisi na kuitumia. Ni rahisi sana kuiona njia hii, na inashawishi sana kutumia, lakini tatizo sasa, haikufikishi kule unakotaka kwenda, inakupoteza.
2. Kutafuta njia ya mkato, hii ni tofauti na njia rahisi. Hapa unashawishika kwamba kuna njia ya kukufikisha kule ambako unataka kufika, na haitakutesa kama njia unayopita sasa. Tatizo ni kwamba njia ya mkato inakuacha na mikato mingi, yaani itakukatakata, na hata kama utafika, hutadumu.
3. Kushindana, na kujilinganisha na wengine, kuona kwamba wewe ni bora kuliko wengine na hivyo kuridhika. Au kuona wengine ni bora kuliko wewe na hivyo kukata tamaa. Ukishaanza tu kujilinganisha na wengine, jua umeipa kisogo safari yako ya kuwa na maisha bora.
4. Kufanya kwa kawaida. Huu mtego umemaliza wengi, na unashawishi kweli. Kwa nini nijitese wakati naweza kuwa na maisha yangu ya kawaida tu? Kwa nini nijitume zaidi kwenye kazi wakati hata nikifanya kawaida napata mshahara wangu? Kawaida ni tamu mpaka itakapoacha kuwa kawaida. (nimeipenda hiyo sentensi, nitaiandikia kwenye makala ya ukurasa wa 387 kesho)
5. Kuiga, na sio kuiga tu kwa kawaida, bali kukopi na kupaste. Pale unapofanya kinakuletea changamoto, unajiuliza kwani nahangaika nini, si niige wanachofanya wengine? Unaiga na unaishia kuwa kawaida, unajikuta unajilinganisha na uliowaiga, baadae unashindana nao na unakwisha.
Mitego inatega hasa, na usipokuwa makini hutaweza kufikia yake mafanikio unayotaka. Pamoja na kwamba una jukumu kubwa la kufikia mafanikio, pia una jukumu kubwa la kujua upi ni mtego na uuepuke. Kila siku angalia upi ni mtego na epuka.
SOMA; Hii Ndio Sababu Kwa Nini Watu Wanafurahia Pale Unapoanguka…
TAMKO LANGU;
Nimejifunza ya kwamba safari yangu ya mafanikio ina mitego mingi sana. Na mitego hii inaninyemelea ili kuniondoa kwenye safari hii. Mitego hii inavutia sana hivyo bila ya kuwa makini ni rahisi kushawishika na kuiacha safari yangu. Kuanzia leo ninahakikisha naiona mitego hii mapema kabla sijanasa na kunipoteza kabisa kwenye safari hii niliyochagua.
NENO LA LEO.
Man is the only kind of varmint sets his own trap, baits it, then steps in it.
John Steinbeck
Binadamu ndiye kiumbe pekee ambaye anatengeneza mtego wake mwenyewe, anaweka chambo mwenyewe halafu ananasa kwenye mtego huo yeye mwenyewe.
Epuka mitego mitego mingi iliyopo kwenye safari yako ya mafanikio, bila hivyo hutaweza kuyafikia mafanikio.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.