Natumai hujambo ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA na unaendelea kufanya harakati ili uweze kufikia malengo yako uliyojiwekea. Uwekezaji wa majengo ni jambo nzuri, lakini jambo lolote nzuri huwa na changamoto zake. Uwekezaji wa majengo hukabiliwa na hatari nyingi sana ambazo humfanya mmiliki apate hasara na hata kupoteza kabisa alichowekeza kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa. Ni hatari sana endapo mmiliki hataweza kuweka mikakati sahihi ya namna gani atapambana au kukabiliana nayo endapo itatokea dharura yoyote na wakati wowote. Lengo la makala hii ni kukuwezesha kutambua hatari zinazoikabili uwekezaji wa majengo, haya ni mambo ambayo watu wengi hawayazingatii sana kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuchukua tahadhari katika yale tuyafanyayo kama sehemu ya maisha yetu na hata mamlaka husika nahisi bado ziko usingizini katika kuhakikisha usalama wa raia kwenye makazi yao. Haya ni mambo hatari sana yanayoweza kukupotezea uwekezaji wako kwa muda mfupi endapo hutazingatia.1. Majanga ya moto
Katika maisha ya mwanadamu moto ni sehemu ya hitaji lake muhimu sana ili maisha yaendelee. Kwa hiyo moto ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu. Mwanadamu hutumia njia mbalimbali za kuzalisha moto katika shughuli zake za kila siku kwa kuwa ni nishati muhimu endapo itatumika kwa ufasaha katika lengo husika. Haijalishi uwe moto wa majumbani, viwandani, sehemu za biashara au starehe, utofauti huwa ni vyanzo vya moto huo lakini matokeo huwa ni yaleyale. Moja ya mambo muhimu sana yanayozingatiwa katika ubunifu wa majengo ni usalama wa wakazi au watumiaji wa majengo hayo. Wataalamu wa majengo hushauri wateja wao kutumia baadhi ya malighafi za ujenzi zenye uwezo wa kupambana na moto kwa muda kadhaa kuruhusu watumiaji na mali zao kuweza kuepuka endapo watapata wasaa wa kufanya hivyo. Uwezo huo hutegemea aina ya majengo husika na hasa matumizi yake. Zaidi ya asilimia 99.7 ya malighafi za ujenzi huathiriwa na moto na kuharibiwa kwa namna tofauti. Ni muhimu sana kutumia wataalamu kabla na wakati wa ujenzi ili waweze kutathmini mazingira, ubora na umaridadi ili kukidhi mahitaji ya mmiliki.
Vipo vyanzo mbalimbali vya moto ambavyo hutumika na kuhifadhiwa kwenye majengo, kama vile majiko ya mkaa, gesi na mafuta, vimiminika vya milipuko kama vile petrol, dizeli na baadhi ya mafuta, pia ni muhimu kuwa mwangalifu sana na vyanzo vya nishati mwanga kama vile mishumaa na chemli ili kuepukana na uzembe wa kuwa chanzo cha majanga ya moto. Vyanzo hivi huwa tuna mahitaji navyo na mara nyingi tunahifadhi kwenye majengo, lakini huwa ni vyanzo vya majanga ya moto ikiwa vitachochewa pasipo utayari. Katika ubunifu wa majengo Wataalamu huzingatia aina na mpangilio wa vyumba na milango, ubora wa malighafi zinazotumika, na hatimaye hubuni aina gani ya vifaa vitakavyowekwa kwenye majengo ili kutoa ishara na taarifa au kupambana na majanga ya moto. Zingatia sana usalama wa mali na watumiaji kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya moto vinatumika na kuhifadhiwa kwa umakini sana. Inashangaza sana kutembea na vyombo vya kupambana na moto kwenye vyombo vya usafiri na kusahau kuweka vyombo kama hivyo nyumbani au sehemu ya kazi. Pia zingatia kuwaelimisha wakazi namna ya kutumia vyombo vya kupambana na moto endapo utathamini umuhimu wake.
SOMA; Faida Za Uwekezaji Wa Majengo Kwenye Maeneo Salama Na Yaliyopimwa Na Wataalam Wa Ardhi

2. Mafuriko ya maji
Mafuriko ya maji ni hali ya maji kuzidi kingo zilizopo na kusambaa nje ya mfumo wake wa kawaida. Hali hii husababisha matokeo hasi kwa viumbe hai wakiwamo binadamu, mazao na wanyama. Wataalamu wa ujenzi huzingatia sana mandhari ya eneo husika kabla ya kufanya ubunifu na uchoraji wa ramani za majengo husika. Hii husaidia kubuni mfumo wa msingi wa jengo hilo ili ikidhi mahitaji ya mtumiaji na mazingira halisi ya mahali husika. Katika fani ya uhandisi ujenzi nimefundishwa na kuaminishwa kuwa ujenzi unaweza kufanyika mahali popote chini ya anga la ulimwengu, muhimu ni kuzingatia ubora na vigezo husika ambavyo hutokana na tafiti kabla ya ujenzi. Mahandaki, meli, madaraja, minara ni mfano wa majengo yaliyo katika mazingira tofauti. Tatizo kubwa linalotukabili watanzania ni kutokuwa na usimamizi mzuri wa mipango miji na utekelezaji wake. Kushindwa kutambua, kuratibisha na kusimamia “master plan” za miji na majiji kumesababisha kila aina ya matokeo hasi ya kijamii, sayansi na uchumi kuwa katika hali ya mkwamo. Watu wamejenga kiholela na mbaya Zaidi wameshindwa kuainisha mazingira na wengine kujikuta wakijenga kwenye mabonde na mikondo ya maji. Katika mazingira haya mafuriko ya maji wakati wa majira ya mvua hayaepukiki kutokana na kuvamiwa kwa mikondo ya maji. Maeneo yaliyojengwa kiholela ujenzi wa miundombinu ya maji huwa ni mgumu sana kutokana na kutokuwa na mpangilio maalumu wa ujenzi. Njia pekee ya kuzuia mafuriko ni kuruhusu maji yapite katika njia rasmi itakayowekwa na kujengewa vizuri na wewe kutokuwa chanzo cha maji kutuama kwenye eneo lako. Zipo njia nyingi za kupambana na hali hiyo ambazo hutegemea mandhari ya eneo husika. Epuka kujenga kwenye mikondo ya maji ikiwa hautotoa njia mbadala. Mtafute mtaalamu akushauri kabla na wakati wa ujenzi.
SOMA; Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa”

3. Kunyang’anywa Umiliki
Moja ya mambo hatari ambayo nimekutana nayo kwenye ujenzi ni umiliki halali wa eneo la ujenzi. Nasikitika sana baada ya kubaini kuwa maeneo mengi ya ardhi yanamilikiwa na Zaidi ya mtu mmoja pasipo kufahamiana. Sekeseke na utata huanza endapo mmoja wao ameanza harakati za ujenzi. Ukifuatilia kwa undani utagundua kuwa urasimu, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi na wasimamizi wa halmashauri na wizara ya ardhi kuwa ni sehemu ya tatizo hili. Inashangaza kuona eneo moja linamilikiwa na zaidi ya watu wawili na wote wana viambatanisho halali vya umiliki, ni hatari sana. Lengo langu ni kukufanya uwe mfuatiliaji wa mara kwa mara ili kuepuka migogoro kama hii. Hakiki mara kwa mara umiliki wako wa eneo na mali nyingine. Katika ujenzi tunakutana na changamoto nyingi sana za kiutendaji, lakini changamoto nyingi zinatokana na uelewa mdogo wa wananchi na mapungufu mengi ya uwajibikaji katika sekta na taasisi za serikali. Hali hii hukatisha tamaa sana na kudumaza maendeleo. Epuka tabu na dhahma hizi kwa kujenga sehemu salama na uweze kufurahia maisha ya uwekezaji wako.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888,
Email: kimbenickas@yahoo.com