Ni vizuri kusifia hasa pale ambapo kuna mtu au watu wamefanya jambo ambalo ni jema na linafaa kuigwa.
Ila kuishia kusifia tu hakutakuwa na msaada kwetu, msaada utakuja pale ambapo tutajiuliza wao wamefanyaje halafu na sisi tukaanza kufanya.
Hadithi za watu wenye mafanikio makubwa duniani zinapatikana kila mahali, wengi tunazijua na tunawasifia. Walianzia chini sana, waliambiwa hawawezi, walikatishwa tamaa lakini walivuka yote hayo na hatimaye wakafanikiwa. Tunaweza kutumia muda mwingi kuwasifu, lakini kuishia hapo maisha yetu yataendelea kuwa kama yalivyo sasa.
Kama tunataka maisha yetu kweli yabadilike, ni lazima tuanze kufanya kama wao walivyofanya, na sio hivyo tu, bali kwenda mbele zaidi.
Kwa mfano unasifia mtu fulani alianzia chini kabisa, amekazana na biashara na sasa ni tajiri mkubwa, halafu wewe hujaanza hata biashara, unasubiri nini?
Na wakati mwingine huku kusifia kunafanya tujidhalilishe kabisa. Mfano mtu umepanga kukutana na mtu au watu sehemu fulani kwa muda fulani, halafu wanachelewa. Ni rahisi kusema ingekuwa wazungu wangewahi sana, wenzetu wako vizuri kwenye muda. Unatoka hapo, kesho wewe unachelewa!!
Wakati mwingine tunashindwa kuchukua hatua na kuishia tu kusifia kwa kuwa tunajipa sababu, ambazo zinatufanya sisi tuonekane hatuwezi. Sababu kama mazingira yangu hayaruhusu, nategemewa na wengi, umri wangu umekwenda, sikupata elimu. Sababu hizi na nyingine nyingi kwanza ni za uongo, pili hazikusaidii kwa lolote.
Ni wakati sasa wa kusifia na kuangalia ni kipi cha kuchukua na kufanyia kazi.
Huwa tunafikiri ili kuanzia kufanyia kazi basi tunahitaji kujipanga sana, tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yetu, lakini hii sio kweli pia. Kwa sababu unaweza kuanza popote ulivyo na vyovyote ulivyo. Kikubwa ni kuanzia kufanyia kazi machache, na kutengeneza utaratibu rahisi wa maisha yako.
Kwa mfano mwaka huu tunaishi kwa falsafa ya NIDHAMU, UADILIFU, KUJITUMA. Kwa hayo matatu, unaweza kufika popote unapotaka. Weka nidhamu kubwa kwenye maisha yako na kile unachofanya, kuwa na uadilifu kwenye kila jambo kwenye maisha yako, na jitume sana. Ukiweza kusimamia hayo matatu, hutabaki kama ulivyo sasa.
SOMA; Mbinu Za Kisaikolojia Za Kuidanganya Akili Yako Ili Uweze Kufanya Kazi Zaidi Hata Kama Umechoka
TAMKO LANGU;
Umefika wakati sasa niache tu kusifia na badala yake nichukue hatua. Kuanzia leo nimeamua ya kwamba pale ninapomsifia mtu, ni lazima niangalie ni jambo na mimi ninaweza kubadili au kuanza kufanya kwenye maisha yangu ili niweze kupata matokeo bora kwangu na kwa wengine pia. Sitaishia tu kusifia, bali nitakazana kufanyia kazi ili maisha yangu yawe bora pia. Na ninaanza na NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA kwenye kila jambo ninalofanya kwenye maisha yangu.
NENO LA LEO.
The way to get started is to quit talking and begin doing.
Walt Disney
Njia ya kuanza ni kuacha kuongea na kuanza kufanya.
Usiishie tu kusifia wengine kwa yale mazuri wanayofanya, bali angalia ni jinsi gani na wewe unaweza kufanya mazuri na anza kufanyia kazi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.