Hebu pata picha ungekuwa unaishi mwaka 1950, ambapo hakukuwa na mtandao wa intaneti na hivyo chochote ambacho unataka kujua inahitaji uende maktaba, uanze kupekua vitabu ndio upate.

Lakini hatupo zama hizo tena, sasa hivi tunaishi kwenye dunia ya sekunde sita, kama kuna kitu hujui unaweza kujijua ndani ya sekunde sita tu. Unachukua simu yako, unaingia google na kuandika kile unachotaka kujua. Tena google ikihisi umekosea itakuletea maelezo ambayo inafikiri ulikuwa unamaanisha.

Kuwepo kwa google kumerahisisha sana mambo na kujifunza kwa sasa kumekuwa rahisi mno, mno. Lakini pia uwepo wa google umekuja na changamoto mpya, ambayo ni watu kuwa na utegemezi mkubwa sana kwenye mitandao ya aina hii.

Watu wanapokutana na changamoto wamekuwa hawafikiri tena, badala yake wanakwenda google na kuuliza swali, majibu yanakuja na wanayachukua na kufanyia kazi. Sasa ingekuwa vizuri sana kama kila kitu kingewezekana hivi, lakini sio vyote vinawezekana.

Kuna maswali ambayo google haiwezi kujibu kabisa, hata ungeuliza mara ngapi, hata ungeuliza kwa lugha gani. Na ni maswali haya ambao ni muhimu sana kwako ili kufanya maamuzi bora kwako na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Kama unataka kujifunza kupika pilau nenda google na andika, JINSI YA KUPIKA PILAU, na utaletewa maelezo ya kutosha ya jinsi ya kupika pilau. Kama unataka kujua historia au data zozote uliza tu google na utaletewa majibu.

Ila sasa tuseme umepata kazi maeneo mawili tofauti, na yote unaona kama uanakufaa, uchukue kazi ipi na ipi uiache, uliza google mara kumi hutapata jibu. Au upo kwenye mahusiano ambayo yamekuwa yanakupa changamoto kubwa, unafikiria kuyamaliza mahusiano hayo na usonge mbele, na wakati huo pia unafikiria kuendelea kuwepo kwenye mahusiano hayo. Google haiwezi kukupa jibu la uhakika hapo.

Maswali yote ambayo yanahusu hali fulani unayopitia wewe kama wewe, google haiwezi kuyajibu, kabisa. Ni maswali haya ambayo yanakuhitaji wewe ukae chini na ufikiri kisha uje na majibu ambayo yatakufaa wewe kulingana na hali unayopitia.

Yote haya ni kusema kwamba japo teknolojia imerahisisha sana utafutaji wa majibu, bado tunahitaji kutumia akili zetu kufikiri kwa kina kuhusu jibu lolote tunalolitaka au tunalolipata. Maana kutegemea teknolojia moja kwa moja kwa kila jibu unalotaka, utafika kwenye hali ambapo huwezi kupata majibu zaidi ya kufikiri wewe mwenyewe.

Jenga uwezo wako wa kufikiri kwa kina, utakusaidia kwenye maeneo mengi ya maisha yako.

SOMA;SIRI YA 34 YA MAFANIKIO; Unakuwa Kile Unachofikiria.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba japo teknolojia inarahisisha sana upatikanaji wa majibu, bado nahitaji kujenga uwezo wangu w akufikiri kwa kina. Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya maswali na changamoto nahitaji kufanya maamuzi mimi mwenyewe na teknolojia haiwezi kunisaidia kwenye hilo. Kuanzia sasa nitajenga uwezo wangu wa kufikiri kwa kudadisi na kuuliza maswali.

NENO LA LEO.

“If there was one life skill everyone on the planet needed, it was the ability to think with critical objectivity”
Josh Lanyon

Kama kuna ujuzi mmoja wa maisha ambao kila mtu kwenye dunia hii anatakiwa kuwa nao basi ni uwezo wa kufikiri kwa kina.

Watu wengi wamekuwa hawafikiri kwa kina, badala yake wanapokea kila wanachoambiwa au kuona.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.