Siku zote katika safari yako ya mafanikio sio kile unachokifanya ndicho kina uhakika mkubwa wa kukupa matokeo makubwa ya mafanikio unayoyahitaji, hapana. Bali uhakika pekee wa kupata matokeo makubwa ya mafanikio mara nyingi sana huwa upo kwenye namna gani unalifanya hilo jambo unalolifanya sasa.
Inawezekana hunielewi vizuri, lakini sikiliza. Kwa mfano kama wewe ni mfanyabiashara, biashara unayoifanya sio tiketi ya kukupa mafanikio ya moja kwa moja. Kitu kitakachokupa mafanikio hapo ni kwa namna gani unafanya biashara yako na kuongeza kitu cha ziada ambacho wengine hawana hadi kujikuta unavuta wateja wengi zaidi.
Na kama kufanya jambo fulani tu peke yake ndio mafanikio yangekuwa yamepatikana basi kila mtu angekuwa tajiri katika hii dunia. Kitu cha kujua hapa na kukielewa vizuri tambua kufanya jambo fulani peke yake bila kuweka mikakati, mbinu na mipango mbalimbali ya kulifanikisha jambo hilo kwa uhakika, huwezi kufanikiwa.
Jaribu kujiuliza hivi ni mara ngapi umewahi kusikia watu wakisema nikifanya biashara hii lazima nitafanikiwa. Na wengine ulisikia wakisema nikifanikiwa kusoma ni lazima nitakuwa na maisha mazuri. Lakini je, baada ya kufanikisha mambo hayo na kuyafanya, mafanikio waliyokuwa wakijipa uhakika waliyapata? Wengi utakuta hawakufanikiwa.
![]() |
JITUME ZAIDI KWENYE KAZI YAKO. |
Ni kitu kinachoweza kuonekana cha kushangaza kidogo lakini huo ndio ukweli. Kufanya jambo fulani kwenye maisha yako, hiyo inakuwa ni kama tiketi ya kukupeleka kwenye mchezo lakini sio ‘gerentii’ ya kufanikiwa au kukupa ushindi wa moja kwa moja. Utawezaje kufanikiwa? Sasa hapo ndio mbinu na mikakati tofauti ya kufanikiwa unatakiwa kuiweka ili kujipa uhakika wa mafanikio.
Kwa hiyo kwa kujua hili acha kuendelea kujidanganyana kujipa matumaini hewa kwamba ‘Aaaah nikifanya biashara hii ni lazima nifanikiwe.’ Ni kweli linaweza likawa jambo zuri sana lakini utafanikiwa ukiwa utaingia kwa kujiandaa huku ukiweka juhudi zote na kuamua kukabiliana na kila changamoto zinazojitokeza, lakini bila kusahau kuweka mikakakti muhimu ya kukusaidia kufanikiwa kama nilivyotangulia kusema hapo awali.
Lakini kitendo cha kukurupuka na kuingia kichwa kichwa kwenye biashara eti kisa umesikia ni nzuri uwe una uhakika upo uwezekano mkubwa wa kupotea. Maandalizi ni muhimu sana kwenye jambo lolote unalotaka kulifanya hasa kwenye nyakati zetu hizi tulizonazo za ushindani. Bila kujiandaa vizuri kushindwa itakuwa ni rahisi sana kwako.
Kwa hiyo kwa vyovyote vile iwavyo acha kujivunia sana au kujaa na kiburi na kile unachokifanya na ukajipa matumaini yote lazima ufanikiwe bila kuweka mikakati na mbinu bora za ushindi. Wewe ni mtu wa tafauti sana, ni mtu wa mabadiliko na hili naamini unaweza kulifanya pia kwa kufanya jambo lako huku ukihusisha na mikakati ya ushindi.
Kila wakati jaribu kujiuliza utafanya vipi kitu hicho unachokifanya sasa ili kikupe mafanikio makubwa. Hili ni jambo ambalo hutakiwi kulisahau kamwe kwenye maisha yako. Kumbuka, uhakika wa mafanikio yako unakuja sio tu kwa kile unachokifanya peke yake, bali je, kitu hicho unakifanyaje? Ipo tofauti na wengine? Hakikisha usisahau jambo hili kamwe litakujengea mafanikio makubwa. Kuwa wa tofauti.
Kwa makala nyingine za mafanikio tembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,