Sisi binadamu ni viumbe wa hisia, japo tunapenda kufikiri kwa mantiki, lakini bado maamuzi yetu mengi tunayafanya kwa hisia.
Hisia ni nzuri sana katika kujenga mahusiano mazuri, lakini ni mbaya sana katika kufanya maamuzi.
Mara nyingi maamuzi unayofanya kwa hisia huishia kuwa ni maamuzi mabaya na yanayokugharimu kwakiasi kikubwa, iwe ni kwenye biashara, kazi na hata maisha kwa ujumla.
Biashara zetu zimekuwa zinaathiriwa sana na hisia zetu, pale tunapokubali hisia zitutawale wakati wa maamuzi muhimu, tunaishia kukosea.
Kuna maeneo ambayo hisia zimekuwa zinawasumbua wengi..
1. Kufanya maamuzi juu ya ushirika wa biashara. Unaweza kuingia kwenye ushirika au ubia wa kibiashara na mtu kwa sababu tu ni rafiki au ndugu. Na mnafanya bila ya makubaliano maalumu kwa sababu tu mnajuana zaidi ya biashara. Mara nyingi maamuzi haya huleta matatizo baadae.
2. Maamuzi kuhusiana na taratibu za kibiashara. Huenda kuna utaratibu fulani ambao upo kwenye biashara yako, na utaratibu ule ni kwa nia njema tu ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Ila anakuja mteja na anaomba kwenda kinyume na utaratibu, wewe unajua kabisa kukubali hivyo ni kosa, lakini hisia zako zinakufanya ukubali. Huenda unapata huruma au unaona unapoteza mteja.
Japokuwa tunataka kujenga biashara zetu na kuwaridhisha wateja wetu, fikiri mara mbili kabla hujafanya maamuzi yanayoongozwa na hisia, hasa yale ambayo yanakwenda kinyume na utaratibu uliopo au uliojiwekea kwenye biashara yako. Jua unavyofanya kwa hisia, unatengeneza matatizo.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako. Kama kuna lolote kuhusiana na tulilojadili hapa, nakaribisha majadiliano hapo chini. Kama umewahi kufanya makosa kwa kuongozwa kwa hisia, tushirikishe hapo chini ili tujifunze zaidi.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,