Moja ya maswali ambayo huwa napokea kila mara kutoka kwa wasomaji ni biashara gani mtu afanye kwa mtaji fulani ambao anao. Huwa napokea ujumbe labda nina mtaji wa milioni moja, nifanye biashara gani? Hili ni swali ambalo huwa linawatatiza wengi hasa wale ambao ni wageni kabisa kwenye biashara. Pamoja na swali hili kuwa sawa kwa watu wengi, bado hakuna jibu moja linaloweza kuwafaa watu wote. Kwa swali hili kila mtu ana jibu lake. Yaani kama mpo watu wawili, na kila mmoja ana milioni moja kama mtaji, biashara ya aina moja inaweza kuwa bora kwa mmoja na ikawa mbaya kwa mwingine.

Leo katika makala yetu ya KONA YA MJASIRIAMALI tutachambua hili kwa undani ili mpaka kufika mwisho ujue ni biashara gani inayoweza kukufaa kulingana na mtaji ulionao, mazingira uliyopo na kile unachopendelea kufanya.

Ili kujua ni biashara ipi bora kwako kufanya, kuna vitu vitatu muhimu sana ambavyo tutakwenda kuvichambua hapa kwa kina.

Kitu cha kwanza; wewe mwenyewe unapendelea nini?

Hapa ndipo wazo lako bora la biashara linapoanzia. Biashara inayoendana na vile vitu ambavyo unavipenda, au umekuwa unapenda kufuatilia inakuwa bora kuliko biashara ambayo hujui undani wake. Mara zote ambapo nakutana na watu kwa ajili ya ushauri wa biashara, huwa tunaanzia hapo. Napenda kumuuliza mtu anapendelea nini, na mara zote watu huwa kuna vitu wanavyopendelea ambavyo vinafaa kugeuza kuwa biashara.

Kwa mtu ambaye anapenda kufuatilia mambo ya mitindo, atafanikiwa zaidi iwapo ataanzisha biashara inayohusiana na mavazi au mitindo. Kwa mtu anayependa kufuatilia mambo ya kilimo, atafanikiwa zaidi kama ataanzisha biashara inayohusisha mambo ya kilimo. Kama unapenda kufuatilia mambo ya vyakula na mapishi mbalimbali, ukianzisha mgahawa utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza biashara yenye mafanikio.

Angalia ni vitu gani ambavyo unapenda kufuatilia, au unapenda kuvifanya, hata kama kwa sasa hakuna anayekulipa. Ukishajua kile unachopenda kufuatilia jiulize je kuna mtu yeyote anayelipwa kutokana na kufanya kile ambacho na wewe unapenda kufanya? Au pia jiulize je kuna njia ambapo unaweza kuwasaidia watu kwa kile unachofanya halafu wakakulipa? Kwa njia hii unaweza kupata biashara nzuri sana kwako kufanya.

Kitu cha pili; muda wako wa kuwepo kwenye biashara hiyo.

Kitu cha pili muhimu sana kuangalia ni muda ambao wewe unaweza kufuatilia biashara yako. kuna biashara ambazo zinahitaji muda wako sana, na kuna nyingine hazihitaji muda wako mwingi. Ni muhimu kuangalia upatikanaji wako na hii itakusaidia kujua kama biashara unayokwenda kuanza itakwenda vizuri.

Kama unataka kuanza biashara na wakati huo bado umeajiriwa, ni lazima uwe makini sana kwenye biashara unayochagua. Kwa sababu kuna baadhi ya biashara zinakuhitaji sana, hasa mwanzoni na hivyo kama bado umebanwa na mwajiriwa, itakuwa changamoto kwako na itakuwa rahisi kwa biashara hiyo kufa.

Biashara nyingi, hasa mwanzoni, zinahitaji sana uwepo wako. Hata kama una uwezo wa kuajiri watu wa kuisimamia, hata kama una ndugu au mtu wa karibu wa kuisimamia, bado unahitajika sana hasa mwanzoni ili kujenga misingi mizuri ya biashara hiyo.

Kwa mfano kama unapendelea sana mambo ya upishi, ila pia bado umeajiriwa, akuwa vizuri zaidi kwako kama utaanza biashara labda ya duka la kuuza vitu mbalimbali vya upishi kuliko kuanzisha mgahawa. Hii ni kwa sababu kwenye duka ni rahisi kusimamia kwa muda wako mchache, ila mgahawa unahitaji ukaribu wako kwa muda mwingi wa siku na hata usiku.

Kitu cha tatu; mtaji.

Unaona hapa mtaji ni kitu cha tatu, lakini wengi wamekuwa wakichukua mtaji ndio kitu cha kwanza, na wanapoupata wanaingia kwenye biashara na mwishowe kupata hasara. Ukishajua ni biashara ipi inaendana na wewe, na ukajua una muda kiasi gani wa kuwekeza kwenye biashara hiyo, sasa ndio unakuja kufanya maamuzi, ni mtaji kiasi gani unao kwa kuanzia biashara hiyo. Hapa sasa ndiyo utaamua mtaji ulionao uugaweje ili uweze kuanza biashara na iweze kukua. Na hata kama una mtaji kidogo, unaweza kuanza kwa kiwango kidogo na ukaendelea kukua kutokea hapo.

Mtaji pekee hautoshi kujua kama biashara itakuwa na mafanikio au la, mapenzi yako binafsi na muda ulionao kuwekeza kwenye biashara yako ni muhimu sana kwa mafanikio ya biashara hiyo.

Zingatia mambo hayo matatu na utaweza kujua biashara bora kwako kufanya. Na ukishachagua ni biashara ipi unafanya, weka juhudi na endelea kujifunza. Usikubali kubaki chini, panga kukua zaidi na utafikia mafanikio makubwa kibiashara. Kila la kheri.