Tunaishi kwenye dunia ambayo kuna machaguo mengi sana. Kwa kitu chochote unachotaka kufanya, kuna njia nyingi mbadala za kukuwezesha kufanya au kufikia kitu hiko.
Kwa jicho la kawaida unaweza kusema kwa kuwa na machaguo haya mengi ni maendeleo na inaturahisishia maisha. Lakini ukiangalia kwa jicho halisi, huo sio ukweli. Kuwepo kwa machaguo mengi, kuwepo na njia nyingi mbadala kunakuchosha hata kufanya tu maamuzi, na hivyo mtu kuchukua hatua.
Unapotaka kufanya kitu, halafu kuna njia nyingi mbadala, changamoto itaanzia nitumie njia ipi. Hapo utalinganisha kila njia kwa faida na hasara zake. Kwa kufanya hivi unaanza kuchoka kabla hata hujaanza kufanya kitu husika. Na hali hii inapelekea wewe kutokuchukua hatua.
Hii pia inakwenda kwenye malengo na mipango yako binafsi. kadiri unavyoweka machaguo mengi kwenye mipango yako, ndivyo unavyopunguza uwezekano wa wewe kufanyia kazi. Kama umeweka mlolongo mrefu wa kupita kabla hujaanza kufanyia kazi mipango yako, utaishia kwenye milolongo hiyo kabla hata hujaanza kutekeleza.
Kuepuka hali hii ya machaguo mengi kukuzuia kuchukua hatua, jipange mapema kabisa, hakikisha unajua ni nini unataka na utakifikiaje. Wakati wengine wanahangaika kujaribu njia mbalimbali mbadala, wewe chagua njia moja ambayo utaitumia mara zote. Na inapofika wakati w akuchukua hatua, fuata njia ile. Utakuwa mbali zaidi pale wengine watakapostuka kwamba kuchagua tu kunawapotezea muda.
Habari zinasema kwamba raisi wa marekani Barack Obama, huwa anavaa suti za aina mbili tu, kijivu au bluu nyeusi. Kwa hali hii hana haja ya kufikiria anavaa nini asubuhi. Habari pia zinasema mmiliki wa mtandao mkubwa wa kijamii, facebook Bwana Mark Zukerberg huwa anavaa tisheti na suruali ya aina moja. Hivyo inampunguzia yeye muda anaopoteza kufikiria avae nini kwenye siku husika.
Ni juhudi zipi unazifanya wewe kuokoa muda na uchovu unaopata wakati wa kufanya maamuzi? Punguza machaguo, na utakuwa na hamasa ya kuchukua hatua.
SOMA; KUJISOMEA; Unapata Wapi Muda Wa Kujisomea Na Unapataje Vitabu Vya Kujisomea?
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kadiri kulivyo na njia nyingi mbadala za kufanya kitu, ndivyo inavyokuwa vigumu kwangu kufanya kitu hiko. Hii ni kwa sababu napoteza muda na nguvu nyingi kwenye kufanya tu maamuzi ni njia ipi nitumie. Kuanzia sasa kwa yale mambo ambayo ni muhimu kwangu, nitapunguza machaguo ili iwe rahisi kwangu kuanza kuchukua hatua na sio kuanza ubishani wa ndani kwamba nitumie njia ipi.
NENO LA LEO.
When people have too many choices, they make bad choices.
Thom Browne
Watu wanapokuwa na machaguo mengi, wanafanya uchaguzi mbaya.
Hakikisha unakuwa na machaguo machache kwenye utekelezaji wa mipango yako, hii itakusaidia kuepuka kupoteza muda na nguvu kufanya maamuzi ya uchaguzi upi ni sahihi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.