Kwenye biashara yoyote unayofanya au unayoingia kufanya, kuna viwango ambavyo waliotangulia kufanya biashara hiyo walishaviweka.
Kuna utaratibu fulani ambao karibu kila mtu anayefanya biashara ya aina hiyo huwa anaufuata. Lakini ukichunguza kwa makini, huoni maana au mantiki yoyote ya kufanya kitu hiko.
Hivi ni viwango ambavyo unahitaji kuviepuka, hivi ni viwango ambavyo vinakurudisha nyuma.
Leo hii ichunguze biashara yako kwa kina, angalia kila unachofanya kwenye biashara yako na jiulize je kina maana na kina mchango kwa biashara yako kuwa bora zaidi? Au unafanya kwa sababu ndiyo umekuta inafanyika hivyo, ndiyo umezoea kufanya hivyo?
Epuka viwango vyovyote ambavyo hujaviweka wewe, na weka viwango ambavyo ni vya juu sana. Halafu pigania kuvifikia, hata kama wengine hawafanyi, hata kama wateja kwa sasa hawaoni umuhimu wa viwango hivyo.
Kuwa mtu wa viwango vyako ambavyo ni vya juu sana na kila siku boresha zaidi. Biashara yako itakua sana bila ya kujali wakati ni mzuri au sio mzuri.
Kila la kheri.